Rhobi Samwelly atoa ombi kuhusu ukatili wa kijinsia

NA FRESHA KINASA

MKURUGENZI wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samwelly ameziomba jumuiya za Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mara kuendelea kushiriki kikamifu katika mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Rhobi ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa Mkoa wa Mara ameyasema hayo Julai Mosi, 2023 Mjini Musoma wakati akitoa semina ya ukatili wa kijinsia kwa wajumbe wa baraza la Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Mara.

Rhobi amebainisha kwamba, vitendo vya ukatili wa kijinsia vinarudisha nyuma maendeleo hivyo Jumuiya za chama hicho zinanafasi ya kukemea mila ambazo ni mbaya ukiwemo ukeketaji, ndoa za utotoni, vipigo kwa wanawake, ajira za utotoni na mila zote mbaya ambazo ni kinyume cha sheria za nchi na haki za binadamu.

Amesema, zipo sababu mbalimbali za ukatili ukiwemo, mfumo dume,dawa za kulevya, mila na desturi, tamaduni na ulevi wa kupindukia na tamaa ya kupata mali.

"Kuna ukatili wa kimwili hapa kuna ukeketaji na vipigo pili kuna ukatili wa kingono ukiwemo ubakaji, ulawiti na tatu kuna ukatili wa kisaikolojia inahusisha kutoa lugha chafu na matendo ambayo yanamsababishia mtu maumivu. 

"Pia tunao ukatili wa kiuchumi hapa mfano mama haruhusiwi kumiliki mali wakati wote wamehusika kupata mali,"amesema Rhobi. 

"Yapo madhara ya ukatili mengi ambayo ni pamoja na kupoteza maisha, kuongezeka kwa watoto wa mitaani, mimba za utotoni, kujeruhiwa kijinsia, mauaji ya vikongwe haya yote ni madhara kwa hiyo lazima tushiriki kupinga ukatili kusaidia jamii yetu kuwa imara,"amesema Rhobi. 
Ili kutokomeza vitendo vya ukatili amesema zipo njia zinaweza kutumika ikiwemo kutumia majukwaa kuhamasisha jamii, kutoa elimu mashuleni, Ushirikishwaji wa wanaume ili kupata mwitikio wa kuzuia ukatili wa kijinsia, ushirikishwaji wa Mamlaka wa serikali za mitaa, Viongozi wa dini, ushirikishwaji wa asasi za kiraia, pamoja na vyombo vya Ulinzi na usalama na wazee wa mila.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Mara, Magubo Kambarage amepongeza shughuli zinazofanywa na Shirika hilo katika kupambana na ukatili wa kijinsia na kuwasaidia watoto ambao hupatiwa hifadhi na vituo vya nyumba salama vinavyomilikiwa na shirika hilo sambamba na Kuwaendeleza kitaaluma na kifani ili wafikie ndoto zao. 

Ameongeza kuwa, jumuiya hiyo itaendelea kuunga mkono kwa dhati juhudi za serikali katika kupambana na ukatili wa Kijinsia ikiwemo kutoa elimu kwa jamii. 
Naye Christopher Mwita Sanya aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara ameishauri jumuiya hiyo kuendelea kusimamia malezi ya watoto na kuwalea vijana wa Chama Cha Mapinduzi katika misingi bora ili kuandaa viongozi bora wa baadae watakaolitumikia taifa kwa uadilifu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news