NA FRESHA KINASA
MKURUGENZI wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania linalojishughulisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia mkoani Mara, Rhobi Samwelly ameihimiza Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Butiama kuendelea kukemea vitendo vya ukatili wa kijinsia bila kuvifumbia macho.
Pia amewasihi kujiepusha na vitendo vya ushoga na matumizi ya dawa za kulevya ambayo yanaathiri nguvu kazi ya taifa na kwa kiwango kikubwa vijana ni tegemeo katika ujenzi wa uchumi wa nchi na kuleta maendeleo na hivyo kawataka wajitambue na kujisimamia.
Hatua hiyo, amesema itawezesha kuimarisha ustawi bora na usawa wenye tija katika kuchochea kasi ya maendeleo kuanzia ngazi ya familia, jamii na taifa kwa ujumla.
Rhobi ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza kuu wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa Mkoa wa Mara ameyasema hayo Julai 15, 2023 wakati akitoa semina ya ukatili wa Kijinsia kwa wajumbe wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) Wilaya ya Butiama.
Rhobi amebainisha kwamba, vitendo vya ukatili wa Kijinsia vinarudisha nyuma maendeleo. Hivyo Jumuiya hiyo inawajibu wa kukemea mila ambazo ni mbaya ukiwemo ukeketaji, ndoa za utotoni, vipigo kwa wanawake, ajira za utotoni na mila zote mbaya ambazo ni kinyume cha sheria za nchi na haki za binadamu.
Amesema zipo sababu mbalimbali za ukatili ukiwemo, mfumo dume, madawa ya kulevya, mila na desturi, tamaduni na ulevi wa kupindukia na tamaa ya kupata mali na hivyo.
"Kuna ukatili wa kimwili hapa Kuna ukeketaji na vipigo pili kuna ukatili wa kingono ukiwemo ubakaji, ulawiti na tatu Kuna ukatili wa kisaikolojia inahusisha kutoa lugha chafu na matendi ambayo yanamsababishia mtu maumivu. Pia tunao ukatili wa kiuchumi hapa mfano mama haruhusiwi kumiliki mali wakati wote wamehusika kupata mali,"amesema Rhobi.
"Yapo madhara ya ukatili mengi ambayo ni pamoja na kupoteza maisha, kuongezeka kwa Watoto wa mitaani, mimba za utotoni, kujeruhiwa Kijinsia, mauaji ya vikongwe haya yote ni madhara kwa hiyo lazima tushiriki kupinga ukatili kusaidia Jamii yetu kuwa imara," amesema Rhobi.
Ili kutokomeza vitendo vya ukatili amesema zipo njia zinaweza kutumika ikiwemo kutumia majukwaa kuhamasisha jamii, kutoa elimu mashuleni, Ushirikishwaji wa wanaume ili kupata mwitikio wa kuzuia ukatili wa kijinsia, ushirikishwaji wa Mamlaka wa serikali za mitaa, Viongozi wa dini, pamoja na vyombo vya Ulinzi na usalama na wazee wa mila.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Butiama Christopher Marwa Siagi amewataka vijana wa Jumuiya hiyo kukisemea Chama kwa mema na kuwa waadilifu na wasikubali kugawanywa na watu kwa maslahi yao binafsi.