MOROGORO-Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe amesema, ugawaji vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) vikiwemo vishikwambi kwa walimu wote nchini na mafunzo yanayotolewa ni muendelezo wa jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
Profesa Mdoe amesema hayo mkoani Morogoro wakati akifungua mafunzo ya TEHAMA kwa Walimu wa Shule za Awali na Msingi Tanzania Bara yaliyofadhiliwa na Programu ya BOOST inayosimamiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Amesema, katika zama za maendeleo ya Sayansi na Teknolojia, matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji ni nyenzo muhimu itakayorahisisha utoaji elimu bora kwa ufanisi na ndio maana Serikali imeandaa mafunzo hayo ili kuwajengea walimu uelewa katika matumizi sahihi ya vifaa hivyo vya TEHAMA.
"Vifaa vingi vya TEHAMA katika baadhi ya shule za msingi zilizowahi kuboreshwa na kuwekwa vifaa hivyo haviko katika hali nzuri inawezekana ni kutokana na changamoto ya matumizi sahihi ya vifaa hivyo yanayotokana na mabadiliko ya teknolojia na utunzaji wake hivyo niwaombe mzingatie mafunzo haya ili muelewe namna ya kutumia vifaa hiyo na utunzaji wake,”amesema Prof. Mdoe.
Aidha, amesema Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itaendelea na mchakato wa kununua vifaa vya tehama kwa ajili ya vituo vya walimu (Teacher's Resources Center) na vingine maalumu vitakavyoteuliwa viweze kutumika na walimu kwenye ufundishaji na ujifunzaji kwa lengo la kurahisisha utoaji elimu bora na yenye ufanisi nchini.
Prof Mdoe ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongongwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi inavyoendelea kuboresha Sekta ya Elimu hapa nchini kwa kujenga na kukarabati miundombinu yakiwemo madarasa, nyumba za walimu na ofisi za walimu, kutoa mafunzo kazini kwa walimu na kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Pia ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuwezesha utekelezaji wa Mradi wa Kuimarisha ujifunzaji kwa wanafunzi wa elimu ya Awali na Msini (BOOST Primary Student Learning).
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia Elimu ya Awali na Msingi kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Suzana Nusu amesema kufanyika kwa mafunzo hayo kwa walimu ni utekelezaji wa afua za Mradi wa BOOST kukusu uimarishaji wa walimu kwenye matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji.
Amesema, mafunzo hayo yatafanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza yana washiriki 148 kutoka kutoka mikoa kumi ya Tanzania Bara. Katika Awamu hii mafunzo yatajielekeza katika kujenga uelewa katika matumizi sahihi ya vifaa vya TEHAMA na vishikwambi, jinsi ya kutunza na kuhifadhi na jinsi ya kufanya maboresho madogomadogo katika vifaa hivyo.
Akizungumzia Awamu ya pili ya mafunzo amesema yatalenga kuwajengea uwezo walimu katika kukuza ujuzi na stadi anuai za kidigitali ili kuwawezesha kuwa na stadi za kutosha katika matumizi ya TEHAMA ili kurahisisha ufundishaji.