Serikali yasema mirungi sasa basi, operesheni ijayo kuondoka na wengi

NA DIRAMAKINI

SERIKALI kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imetoa mwezi mmoja kwa wananachi wa vijiji vya Kata ya Tae kuhakikisha mashamba yote ya mirungi inakatwa, kug'olewa na visiki vyote kutolewa.

Operesheni Tokomeza Mirungi ikiendelea katika vijiji vya Kata ya Tae wilayani Same mkoani Kilimanjaro ambapo zaidi ya hekari 535 ziliteketezwa kwa siku nane.

Maagizo hayo yametolewa na Mkuu wa Wilaya ya Same, Mheshimiwa Kasilda Mgeni katika kikao cha pamoja na wananchi wakiwemo viongozi wa Tae ambacho kimelenga kuwapa elimu ili kuachana na kilimo cha mirungi na kujikita katika mazao mbadala kwa ustawi bora wa uchumi wao na Taifa kwa ujumla.

"Kuna mashamba ambayo hayajafikiwa, si ndiyo? Na sisi si tunayajua? Mmeyapana mbali kileleni kule, jamani Serikali ipo kila mahali. Hayo mashamba yote tunayajua, sasa ninawaagiza viongozi wa Serikali wa Tae ndani ya mwezi mmoja kwa kushirikiana na wananchi wenu wa Tae ahakikisheni mashamba yale yote mmeng'oa, mmekatakata, na visiki mmevitoa.

"Tumeelewana?...tumeelewana ndugu zangu? Tutakapokuja wakati mwingine hatutakuja na sura hii tena, mmenielewa? Mmeshaambiwa mazao mbadala ambayo mnatakiwa kuyalima, kuanzia sasa naomba mnisumbue kuhusiana na mazao gani ambayo mnaona yatafaa hapa.

"Lakini, afisa kilimo ameshayasema, ninyi huku mnalima mihogo, ninyi huku viazi vinastawi, ninyi huku maharage yanastawi, yaani hakuna mazao ambayo huku juu hayastawi si mnalima huku, si ndiyo? Sasa kwa sababu mlipunguza kile kilimo cha mazao halali, mkaamua kujikita na kilimo cha mirungi. Mirungi sasa basi, naomba mrejee tena kwenye kilimo halali.

"Limeni sana, mimi kama mkuu wa wilaya kazi yangu kubwa ni kuhakikisha kuwa, ninawatafutia masoko, lakini kuhakikisha barabara inakuwa nzuri ili mtakapokuwa mmezazisha? Mnafika kwa urahisi kwenye masoko kwa maana ya kwamba barabara ni nzuri, tumeelewana (ndiyooo).

"Baada ya huo muda kuisha, operesheni itarudi kama kawaida, na ili operesheni isiendelee ni kuhakikisha visiki vyote vilivyobaki kule, vyote vinag'olewa.

"Watu wapande mazao mengine, yeyote tutakayemkuta na visiki vile bado anavyo anavyimwagilia ili vikue, tunamkamata.

Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Aretas Lyimo amefafanua kuwa, operesheni ijayo haitamuacha mtu yeyote wakiwemo viongozi wa eneo husika.

"Yeyote tutakayemkuta ana shamba la mirungi, tunamkamata, na watu wamesema kwamba, wapo viongozi mbalimbali ambao wapo huku, kwa nini na wao wanaona hiyo mirungi hawachukui hatua? Kuanzia sasa hivi tutakapofanya operesheni hatutachagua.

"Tutakamata kuanzia mwenyekiti wa kitongoji na watu wake, tutakamata mwenyekiti wa kijiji na watu wake, tutakamata na mtendaji wa kijiji husika kwa sababu mtendaji wa kijiji ni mwakilishi wa Serikali katika eneo hili, anatakiwa ahakikishe wananchi wake wanaishi katika mazingira mazuri, wananchi wake wanapata huduma, Serikali kuna huduma mbalimbali inazitoa huko wananchi wake wanazipata.

"Lakini, pia na mtendaji husika na yeye ni mwakilishi wa Serikali katika eneo hili, kwa hiyo hao wote na afisa tarafa ambaye ndiye anatakiwa kusimamia watendaji wa vijiji na watendaji wa kata kuhakikisha kwamba wananchi waliopo katika eneo lao, hawafanyi uhalifu,"amefafanua Kamishna Jenerali Aretas Lyimo wa DCEA.

Awali hekari 535 za mashamba ya mirungi zimeteketezwa katika oparesheni maalum ‘Tokomeza Mirungi’, iliyoanzia kutekelezwa ndani ya Vijiji vya Rikweni, Heikondi, Tae na Mahande wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro kwa muda wa siku nane kuanzia Julai 2 hadi 9,2023.

Oparesheni hiyo imefanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ikishirikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama likiwemo Jeshi la Polisi Tanzania.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo alisema katika oparesheni hiyo jumla ya watuhumiwa saba wamekamatwa huku akisema mirungi ni moja ya dawa za kulevya zilizokatazwa nchini kwani ina athari nyingi kwa binadamu, kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiafya.

“Inasababisha saratani ya koo, utumbo na uraibu, mtindio wa ubongo, kiuchumi inasababisha nchi inakosa mapato kwa sababu wengi wanaolima mirungi kata hii na eneo hili la Same hawaingizii mapato yoyote Serikali.

“Nawashukuru wote ambao tunashirikiana nao katika oparesheni hii, tuwaombe wananchi wote kama alivyoagiza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, viongozi wote wa Serikali, mkoa, wilaya, kata na vijiji tushirikiane kutokomeza dawa za kulevya.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news