Serikali yatoa maagizo kwa waganga wafawidhi nchini

SONGWE-Serikali imewataka waganga wafawidhi wote nchini kuboresha utendaji kazi ili kuweza kuendana na thamani ya uwekezaji uliyofanyika kwenye vituo vya kutolea huduma.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt.Charles Mahera wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea Kituo cha Afya cha Isansa na Hospitali ya Wilaya ya Mbozi –Vwawa Mkoani Songwe.

Dkt. Mahera amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa pesa nyingi katika kuboresha sekta ya afya nchini ambapo maboresho hayo ni ujenzi wa majengo mapya, ukarabati wa vituo vya afya, ununuzi wa vifaa tiba na dawa.

“Tukifanya kazi kwa kufuata miongozo iliyotolewa na Wizara ya Afya, weledi, maadili na ushirikiano kwa kuzingatia muda wananchi wataweza kupata huduma bora za afya kutoka ngazi ya msingi itakayo kuwa sambamba na uwekezaji uliofanywa na serikali yao" ameeleza Dkt. Mahera

Dkt. Mahera ameongeza kuwa watumishi wa Afya wanatakiwa kuzingatia miongozo ya huduma ya afya pamoja na kujali muda wa kazi ili kuleta ufanisi katika kutoa huduma bora

Ameeleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kuangalia maendeleo ya vituo vya huduma za afya kwa kushirikiana na Wizara ya Afya ambao ndio watunga sera ili kuboresha huduma bora kwa wananchi.

“Naomba watumishi wa Afya muendelee kujituma katika kuwahudumia wananchi kwani serikali iko bega kwa bega na nyinyi katika kuboresha maslahi yenu ili kuwa na mazingira mazuri ya kazi”, amesema Dkt. Mahera.

Aidha, amemuelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Boniface Kasululu kuhakikisha anashirikiana na Timu za usimamizi na uendeshaji wa huduma za Afya ngazi ya Mkoa na Halmashauri (RHMT na CHMT) kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa dawa, vifaa tiba na huduma zinazotolewa katika vituo vya kutolea huduma ili kuleta ufanisi wa kazi na kupata takwimu sahihi za mahitaji kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe ametoa wito kwa watumishi wa afya nchini kutofanya kazi kwa kwa mazoea bali kufuata taratibu za kazi kwa kuzingatia maadili, weledi na viapo vya taaluma zao.

"Sisi wateja wetu ni wananchi wanaokuja kupata huduma, hivyo wahudumiwe kwa wakati, wapate huduma bora, kama mpo na kazi nyingi wapeni taarifa sahihi wagonjwa na ndugu wanaosubiri", amesisitiza Dkt. Magembe

Naye Mkuu wa Programu kutoka Wizara ya Afya kutoka Wizara ya Afya Dkt.Catherine Joachim, amesisitiza watumishi hao kutumia mifumo kwa ufasahaa ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi na kwakufanya hivyo itasaidia kusimamia mapato ya vituo vyao

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news