MTWARA-Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) imetoa misaada ya kibinadamu kwa kaya 184 za Kata ya Kitaya Halmashauri ya Wilaya ya Nanyamba na kaya 160 kwa kata ya Michenjele Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu), Mhe.Jenista Mhagama akimkabidhi Bw.Abdalah Mbwana msaada wa vifaa vya kibinadamu, tukio hilo limefanyika katika kata ya Michenjele iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba Mkoa wa Mtwara.
Zoezi hilo limeongozwa Julai 17,2023 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu), Mhe.Jenista Mhagama mkoani Mtwara.
Amesema, kwa kutumia Sheria Na. 6 iliyotungwa mwaka 2022 ya usimamizi wa maafa, kazi yao ni kufanya tathimini na kutoa mkono wa pole kwenye majanga yanayohusu binadamu mahali popote.
“Nitoe wito kila yanapotokea majanga na maafa, kwanza liwe jukumu letu kufarijiana kwa karibu na kutoa taarifa za dalili za majanga yanapotokea, na kuangalia ni mambo gani ya msingi yafanyike ili kurudisha hali katika utaratibu wa kawaida,”amesema.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu), Mhe.Jenista Mhagama akimkabidhi Bi. Sophia Athumani Rajabu msaada wa vifaa vya kibinadamu, tukio hilo limefanyika katika Kata ya Kitaya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Nanyamba Mkoa wa Mtwara.
Waziri Mhagama amesema,wamepokea tathimini iliyowakilishwa ikionesha madhara yaliyojitokeza kwa wananchi katika eneo hilo katika maeneo kadha kwa kadha katika makazi, chakula,na nyenzo za kufanyia shughuli za kiuchumi
Amefafanua kwamba, Serikali imekuja kutoa mkono wa pole ili waweze kushirikiana na wao katika kujibadilishia hali katika kipindi hiki chote.
"Ni kweli Serikali imeendelea kuwa na nyie kwa nguvu kubwa na ya ziada zaidi,”alisema Mheshimiwa Waziri Mhagama.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwashika mkono wananchi yanapotokea majanga ya kibindamu, yanapotokea mafuriko, na vinapotokea vimbunga, "tunajisikia faraja.
"Tumepokea magodoro 190, tumepokea ndoo kubwa 380, na ndoo kubwa za lita ishirini 190, tumepokea blanketi za watoto 190 na blanketi za watu wazima 380 na mikeka 380 na mabati 5700 na kaya zinazostahiki ni 184 zilizoordheshwa kwa sasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Nanyamba."
Kanali Ahmedi ameongeza kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba ilipokea vifaa vya msaada wa kibinadamu kwa waathirika 160.
"Tuna mabati 4800, kuna magodoro 160, mikeka 320 na mablanketi 320, ndoo kubwa za lita ishirini 320 na tayari zimeundwa kamati mbalimbali kwa ajili ya kuhakiki."
Naye Mbunge wa Nanyamba, Mhe. Abdallah Chikota amesema, "Tunashukuru kwa msaada wa kibinadamu na kipekee nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt, Samia Suluhu Hassan kwa sababu asiyeshukuru kwa moja hata kumi hawezi kushukuru."