NA LUSUNGU HELELA
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amewataka Watanzania kuendelea kushirikiana na Serikali katika vita dhidi ya rushwa huku akisisitiza kuwa athari zitokanazo na rushwa zina madhara kwa watu wote.
Akizungumza Julai 9,2023 kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi katika ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Rushwa Barani Afrika ambayo hufanyika kila mwaka Julai 11, ambapo mwaka huu 2023 maadhimisho hayo yanafanyika hapa Tanzania, Jijini Arusha, amesema rushwa ni adui wa haki na inamnyima mwenye haki huku ikimpendelea asiye na haki.
Amesema mapambano dhidi ya rushwa sio jukumu la Taasisi pekee za kupambana na rushwa ambazo ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa hapa nchini (TAKUKURU), Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu uchumi Zanzibar (ZAECA) bali ni jukumu la kila Mwananchi.
Amesema kila Mwananchi kwa nafasi yake ayatumie Maadhimisho hayo katika kufanya tathmini kwa hatua ambazo nchi za Afrika na mtu mmoja mmoja imezichukua katika kupambana na rushwa.
Akizungumzia lengo kuu la maadhimisho hayo, Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amesema ni kutathmini mafanikio, changamoto na mikakati ya kuzuia na kupambana na rushwa kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, Kujenga uhusiano na ushirikiano baina ya nchi za Afrika katika kuzuia na kupambana na rushwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene akizungumza kabla ya kumkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Hemed Suleiman Abdulla kufungua Maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Rushwa Barani Afrika ambayo kwa mwaka huu yanafanyika nchini Tanzania, Jijini Arusha, kwa lengo la kutathmini mafanikio, changamoto na mikakati ya kuzuia na kupambana na rushwa kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika.
Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene amesema Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa za Tanzania Bara na Visiwani zitaendelea kushirikiana na wadau katika mapambano dhidi ya rushwa.
Ameongeza kuwa Maadhimisho hayo ni fursa adimu kwa Taasisi za Kuzuia na kupambana na Rushwa Barani Afrika kuweza kubadilishana uzoefu na kuhakikisha kuwa rushwa inatokomezwa kabisa.
Ili kupeleka ujumbe ulimwenguni kuwa Bara la Afrika linapinga rushwa, mkutano huo ulitanguliwa na matembezi ya hiari yanayofahamika kwa jina la 'Ant-Corruption Work'.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ambayo yanatarajia kufikia tamati Julai 11, 2023 ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi, inasema "Ni Mafanikio Baada ya Miaka 20 ya Utekelezaji wa Mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Matarajio Yake".