Simba SC yamrejesha Jose Luis Miquissone

DAR ES SALAAM-Uongozi wa Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam umemsajili kiungo mshambuliaji Jose Luis Miquissone.

Kiungo huyo anarejea tena Simba baada ya kuitumikia klabu yao kwa mafanikio makubwa kabla ya kuuzwa kwa miamba ya Afrika Al Ahly ya Misri miaka miwili iliyopita

Hatua hiyo inafikiwa baada ya fununu za muda mrefu kuhusu usajili wa kiungo mshambuliaji Jose Luis Miquissone raia wa Msumbuji kutoka Al Ahly ya Misri kwa mkataba wa miaka miwili.

Simba SC wamemchukua Miquissone kama mchezaji huru baada ya kuvunja mkataba na klabu yake hiyo.

Kurejea kwa Miquissone kunatajwa kuwa ni faida kubwa kwa Simba SC, kwani tayari ana uzoefu mkubwa na soka la Afrika, lakini kubwa zaidi analijua vema soka la Tanzania.

Aidha, tayari Miquissone ameshawasili Tanzania kwa ajili ya maandalizi ya safari ya kwenda nchini Uturuki.

Miquissone anatarajiwa kuondoka mapema wiki ijao kuelekea Uturuki ambapo atajiunga na wenzake kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa 2023/2024.

Mbali na hayo, Luis Jose Miquissone anakamilisha idadi ya wachezaji tisa wapya Simba SC katika dirisha hili, kati yao watani wa kigeni wakiwemo Wacameroon wawili, beki wa katí Che Fondoh Malone Junior kutoka Cotton Sport ya kwao na kiungo mshambuliaji, Leandre Essomba Willy Onana kutoka Rayon Sport ya Rwanda.

Pia, wageni wengine waliosajiliwa Simba SC ni kiungo Mkongo Fabrice Luamba Ngoma kutoka Al Hilal ya Sudan, winga wa kushoto na Aubin Kramo Kouamé kutoka ASEC Mimosas ya Ivory Coast.

Wazawa ni beki wa kulia, David Kameta (Duchu) kutoka Mtibwa Sugar, beki wa kati, Hussein Kazi kutoka Geita Gold, kiungo Abdallah Hamisi Riziki kutoka Orapa United FC ya Botswana na mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Shaaban Iddi Chilunda. Aidha, klabu hiyo inaendelea na maandalizi kupitia kambi yake nchini Uturuki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news