Simba yazindua jezi, Mlima Kilimanjaro

NA LWAGA MWAMBANDE

"Simba itazindua jezi zake juu ya mlima Kilimanjaro, kwani hii inaendana na ukubwa wa Simba, kwani ni timu bora Afrika, hivyo juu ya Mlima Kilimanjaro ni sehemu sahihi, kwani ni sehemu ya juu zaidi Afrika. Pia tutasaidia jitihada za Serikali kutangaza utalii na Mlima Kilimanjaro;

Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula aliyabainisha hayo awali wakati akizungumza katika tafrija maalum ya kutambulisha uhusiano wao na Benki ya NMB ambapo Simba walizindua huduma tatu, NMB Simba Akaunti, NMB Simba Queens Akaunti na Akaunti ya Watoto ambazo gharama yake ni shilingi 5000.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, uamuzi uliofikiwa na Klabu ya Simba kwenda kuzindua jezi katika kilele cha Mlima Kilimanjaro ni ishara kwamba, msimu ujao wamedhamiria kwenda mbali zaidi. Endelea;


1.Jicho la Mgalilaya, linaamsha hisia,
Simba inafanya haya, kuienzi Tanzania,
Siyo kwa kumwayamwaya, ni vitendo yachangia,
Simba yazindua jezi, Mlima Kilimanjaro.

2.Ilishaanza zamani, kuinadi Tanzania,
Kwa wote wenye uoni, nchi inapigania,
Utajiri wa nchini, iutambue dunia,
Simba yazindua jezi, Mlima Kilimanjaro.

3.Ni utalii wa ndani, nchi tunajivunia,
Na wa nje waje ndani, yetu kuyaangalia,
Fedha zetu za kigeni, tuzidi kujipatia,
Simba yazindua jezi, Mlima Kilimanjaro.

4.Tembelea Tanzania, jezi zatutangazia,
Afrika na dunia, wote wanatusikia,
Haitoshi nakwambia, nchi yetu kusifia,
Simba yazindua jezi, Mlima Kilimanjaro.

5.Ni vitendo nakwambia, si mja kusimulia,
Nchi kututangazia, wafike kuangalia,
Ni uchumi yachangia, Royal Tour kujazia,
Simba yazindua jezi, Mlima Kilimanjaro.

6.Kilimanjaro sikia, Afrika yatambia,
Ni mrefu fwatilia, kwa milima ya dunia,
Simba ndivyo yapania, ubora kuufikia,
Simba yazindua jezi, Mlima Kilimanjaro.

7.Burudani twangojea, tuweze kufurahia,
Makundi yaendelea, chini hatutaanzia,
Supa Ligi nayo pia, Simba peke Tanzania,
Simba yazindua jezi, Mlima Kilimanjaro.

8.Hongera Simba hongera, nchi kututangazia,
Huo ubunifu bora, wafaa igilizia,
Ionekane taswira, watalii kutujia,
Simba yazindua jezi, Mlima Kilimanjaro.

9.Vile waliwasha mwenge, kilele kukifikia,
Simba kwa jezi tusonge, itutambue dunia,
Wengine khanga vitenge, mipasho mwafurahia,
Simba yazindua jezi, Mlima Kilimanjaro.

_@KiMPAB_

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. Tuna wapongeza mno viongozi wa simba ktk hili.kwa sisi tuliosomea Management in tourism tunawa kongole kwani watafaidika na kupanua wigo wa timu yao kwenye mambo makuu kama ifuatavyo.
    1.watachochea uwekezaji ktk timu yao na hata ktk mpira wa Tanzania 🇹🇿, why?kwa sababu mlima kilimanjaro hukusanya aina mbalimbali za makundi ya watu wa ulimwengu, na ktk hili naimani watakuwepo watarii wengi wakati wa tukio hili napengine wapo wenye fedha wakavutiwa zaidi kuijua simba sports club na mpira wa nchi yetu Tanzania.

    2.kuzarisha na kupata watu wapya ktk mahusiano ya kimataifa na kuendelea kuikuza brand ya simba ktk nyuso za wanadamu waliopo ktk sayari yetu hii na kupelekea simba kutambulika zaidi hata nje ya bara hili la Africa na kuvutia watu wengi kuja kuiona timu ya simba.

    3.Itasaidia mno kuiongezea thamani timu ya Simba na kuongeza mapato kupitia wageni,makampuni na tahasisi tofauti za kifedha ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

    4.wataimarisha sifa bora ya solidarity ya nchi yetu Tanzania 🇹🇿 na Dhamira bora ya serikali yetu ktk kuinua na kukuza mpira wa nchi yetu barani Africa na ulimwenguni,na hivyo tutegemee kupitia tukio hili pengine wapo wadau ktk mataifa yetu watajitokeza kuja kungana na serikali kuwekeza ktk mpira wa nchi yetu Tanzania 🇹🇿 hasa kwa vijana na Tanzania kukua zaidi kimpira.

    5.kupitia hili simba watawambia wanamichezo wote duniani na shilikisho la mpira duniani Fifa kuwa Tanzania 🇹🇿 ni pahara salama pa kila mwanamichezo kufika na kushiliki michezo yoyote iletayo amani,utulivu, upendo na umoja na mshikamano wa mabara yetu yote ya mataifa mbalimbali.

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news