NA MWANDISHI WETU
WATANZANIA kote nchini wamehamasishwa kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji zilizopo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Hayo yamesemwa Julai Mosi, 2023 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade),Bi.Latifa M. Khamis katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Iran iliyofanyika katika Uwanja wa Maonesho wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kipindi cha Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (almaarufu kama SabaSaba) yaliyoanza tarehe 28 Juni - 13 Julai, 2023.
Maadhimisho hayo yana lengo la kutangaza fursa za biashara na Uwekezaji zilizopo nchini Iran na Tanzania ambazo zipo katika sekta ya Utalii, elimu, Viwanda pamoja na sekta ya Afya.
Bi.Latifa ameendelea kusema kuwa, Tanzania imekuwa na mahusiano ya kidiplomasia na utamaduni na nchi ya Iran kwa zaidi ya miaka 40 hivyo, TanTrade inahamasisha Watanzania kutumia fursa za biashara na uwekezaji zilizopo nchini Iran ambazo zinapatikana katika sekta ya Afya, Viwanda na Kilimo.
Pia, wana huduma za wateja nzuri pamoja na uwezeshaji wa biashara na unafuu wa gharama za kuendesha biashara.
"TanTrade inaendelea kudumisha mahusiano ya biashara na Uwekezaji yaliyoanzishwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na Rais wa zamani wa Iran Mhe. Ayatollah Khamenei, hivyo katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha uchumi wa nchi unakuwa kwa kasi zaidi.
"Kwa kutangaza bidhaa za Tanzania na kuvutia uwekezaji katika viwanda vya ndani ya nchi ili kuchochea uzalishaji na kupata masoko ya ndani na nje ya nchi, natoa wito kwa Watanzania kutumia fursa za biashara na uwekezaji zilizopo nchini Iran ili kuongeza mapato kwa mfanyabiashara mmoja mmoja pamoja na kuchochea uchumi wa Taifa kwa ujumla,"alisema.
Pia aliongeza kuwa, kwa kipindi hiki cha maonesho watakuwa na mikutano ya kuunganisha wafanyabiashara mbalimbali, tutahakikisha uwekezaji wa sekta ya viwanda unakuwa na unafanikiwa kwa viwango vya juu.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TanTrade,Ulingeta O. Mbamba aliongeza kuwa,Iran kuna fursa za kiutalii, elimu na kilimo hivyo tunaweza kuzalisha mazao pamoja na madini na kupeleka katika soko la Iran.
Pia alisema, ni vyema Watanzania wakachamkia fursa ya biashara na uwekezaji zilizopo nchini Iran kwani bidhaa zao zina ubora wa viwango juu.
"Kwa kipindi hiki cha Sabasaba, Iran wamekuja kujitangaza na kuendelea kuunga undugu wa kibiashara na uwekezaji na Watanzania, hivyo nawaasa Watanzania waichukulie hii kama fursa ya kujifunza uzalishaji wa bidhaa zenye ubora viwango vinavyokubalika Kimataifa, pia Iran ni nchi wezeshi kwa wafanyabiashara wa viwango vya juu vya kati na vya kawaida,"amesema.
Ameongeza kuwa, baada ya maonesho hayo ya SabaSaba wanategemea kuwa na Maonesho ya Iran na Tanzania ambapo nchi hizo mbili zitaonesha bidhaa mbalimbali katika sekta ya kilimo, nafaka, pamoja na elimu.
Naye Balozi wa Iran nchini Tanzania, Mhe.Balozi Hussein Alvandi Behineh alitoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia TanTrade kwa kupata fursa nzuri ya kushiriki na kuazimisha siku ya Iran katika Maonesho ya 47 ya SabaSaba na kuitangaza nchi yao na bidhaa wanazozalisha.
"Tunatoa wito kwa Watanzania kutembelea Maonesho ya SabaSaba na pia kutembelea katika banda letu na kujionea bidhaa tofauti tofauti zenye ubora na viwango vya kimataifa pia waje wajifunze fursa za kibiashara zinazopatika nchini Iran,’’alisema.
Pia aliendelea kusema, Tanzania na Iran zinapaswa kuungana na kuwa kitu kimoja katika biashara ili kuleta uchumi endelevu na wenye afya pamoja na kujenga mahusiano mazuri pamoja na kuinuana katika biashara na uwekezaji.