Tuendelee kuiunga mkono Serikali-Sophia Mjema

NA PIUS NTIGA

KATIBU wa NEC, Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema, amewataka wananchi kuendelea kuiunga mkono serikali chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kuhusu suala la uwekezaji wa Bandari, akisisitiza kuwa yajayo yanafurahisha kupitia kampuni ya DP World.

Mjema ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Uhuru FM ikiwa ni sehemu ya kutoa elimu kuhusu upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa wa upinzani kuhusu majadiliano yanayoendelea ya uwekezaji katika bandari ya Dar es salaam kupitia kampuni inayoongoza duniani katika masuala ya Bandari ya DP World.

Akiwa ameambatana na Meneja wa Uendeshaji wa Bandari Tanzania, Josephat Lukindo, katika studio za Uhuru FM, Katibu huyo wa NEC, Itikadi na Uenezi Mjema, amesema suala la uwekezaji wa bandari ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025 na sio jambo la mtu mmoja kama inavyodaiwa na wapotoshaji.

Amesema CCM itaendelea kutoa elimu zaidi kuhusu suala hilo la uwekezaji wa Bandari kwa kuwa lina tija na manufaa makubwa katika taifa.

Mjema amesisitiza kuwa mapinduzi ya kiuchumi yanakuja kupitia kampuni ya DP World, hivyo wananchi waendelee kuunga mkono hatua inayoendelea kutekelezwa na serikali katika majadiliano ya uendeshaji wa kiuchumi wa Bandari kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai.

Majadiliano hayo yanaweka msingi imara wa yakayofikiwa hadi kuingia Mkataba kuhusu baadhi ya maeneo katika bandari ya Dar es salaam na kwamba nchi haijauzwa.

Aidha, Mjema amesisitiza kuwa uwekezaji huo unatarajiwa kuongeza mchango wa sekta ya bandari kwenye mapato ya nchi kutoka asilimia 37 za sasa hadi takribani Asilimia 70.

Jambo hilo litaipa serikali uwezo mkubwa zaidi wa kusaidia sekta muhimu kwa jamii kama Elimu, Afya, Maji na kuzimua sekta nyingine za uchumi na hivyo kuchochea upatikanaji wa ajira kwa watu wengi zaidi.

Kwa upande wake, Meneja uendeshaji wa Bandari Tanzania, Josephat Lukindo, amesema iwapo mkataba utasainiwa, DP World katika bandari atakuwa na asilimia nane tu katika uendeshaji wa bandari na baadhi ya gati hatohusika nazo likiwemo gati namba 8 hadi 11.

Aidha, amesema mwekezaji katika bandari hatomilikishwa ardhi ya Tanzania na badala yake atakodishwa ardhi, hivyo wananchi wapuuze upotoshaji kuwa nchi imeuzwa, kitu ambacho sio kweli.

Kuhusu suala la ajira kwa Watanzania amesema limewekewa kifungu kabisa kwenye IGA na hakuna mfanyakazi hata mmoja wa Bandari ambaye atapoteza ajira kutokana na shughuli za uendeshaji baada ya DP World kuanza.

Amesema inatarajiwa kuwa ufanisi na ubora wa huduma utakaoanza utasababisha kuwapo kwa ajira nyingi zaidi kuliko ilivyo sasa.

Aidha, amesema katika suala la bandari hakuna ukomo wa miaka 100 kama inavyodaiwa na wapotoshaji.

Amesema Dubai ni sehemu ya Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE), suala la uwekezaji si sehemu ya masuala ya Muungano na kwamba Katiba ya UAE imeeleza kuhusu masuala ya Muungano na yasiyo ya Muungano na suala la uwekezaji halimo.

Pia Lukindo amesema katika majadiliano yanayoendelea, uwekezaji utakuwa katika bandari ya Dar es salaam tu.

Kimsingi, mkataba unahusu uendeshaji ambao ni asilimia nane tu ya shughuli zote za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kwa miaka 22 iliyopita, kampuni ya TICTS ilikuwa ikifanya shughuli kama hizo na bandari haikuwa imeuzwa au kubinafsishwa.

Naye mmoja wa wananchi aliyezungumza na Uhuru FM, Amaly Temu, amesifu majadiliano hayo ya uwekezaji yanayoendelea akisema hatua hiyo itasaidia kukuza uchumi wa Tanzania na utasaidia nchi kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 200 zilizokuwa zikipotea kwa mwezi.

Fedha hizo hupotea kutokana na Mamlaka ya Bandari Tanzania kutumia bandari kavu kutunzia makontena.

Amesema uwekezaji utaongeza ajira kwa watanzania na wafanyakazi wataendelea kusomeshwa katika kuongezewa ujuzi kupitia kampuni ya DP World.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news