Ufaransa yasitisha misaada yote kwa Niger

PARIS-Serikali ya Ufaransa imesitisha misaada yote ya maendeleo na ile ya kibajeti kwa Jamhuri ya Niger kufuatia mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Mohamed Bazoum.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron (kulia) akisalimiana na Rais wa Niger, Mohamed Bazoum jijini Paris mnamo Juni 23, 2023. (Picha na Ludovic Marin/AFP).

Hayo ni kwa mujibu wa tamko la Serikali ya Ufaransa lililotolewa Jumamosi ya Julai 29,2023 kupitia Wizara ya Mambo ya Nje.

Pia, Paris inataka kurejea mara moja kwa utaratibu wa kikatiba nchini Niger pamoja na kurejeshwa kwa Serikali ya Bazoum iliyochaguliwa kidemokrasia, wizara ilisema katika taarifa yake.

Niger ambayo ipo katikati mwa Sahel, ni nchi yenye watu milioni 26 ambayo theluthi mbili ni jangwa na ina moja ya mataifa yenye viwango vya juu zaidi vya ukuaji wa idadi ya watu duniani.

Shirika la Maendeleo la Ufaransa mwaka 2021 lilitoa euro milioni 97 kwa nchi hiyo, mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani, kulingana na takwimu zilizoonwa awali.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, alipokuwa akizuru Papua New Guinea siku ya Ijumaa, alilaani vikali mapinduzi hayo, na kuyataja kuwa hatari kwa eneo hilo na kutaka kuachiliwa kwa Rais Bazoum, ambaye amezuiliwa kwenye makazi yake rasmi tangu Jumatano.

Niger ni moja ya washirika wa mwisho wa Ufaransa katika Sahel, eneo ambalo limekumbwa na ukosefu wa utulivu, ukosefu wa usalama na mashambulizi ya kijihadi.

Aidha, Serikali ya Ufaransa ilimaliza operesheni zake dhidi ya itikadi kali na iliondoa vikosi vyake kutoka Mali mapema mwaka huu kujibu matakwa ya kiongozi wa Serikali ya Bamako.

Ufaransa ambayo maeneo hayo ina mizizi ya utawala wake enzi za ukoloni ina wanajeshi 1,500 nchini Niger ambao wanafanya kazi kwa pamoja na jeshi la Niger. (Mashirika/Diramakini)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news