NA MWANDISHI WETU
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umetoa tahadhari kwa wanachama wake kwa kuwataka kutumia vizuri kadi zao za matibabu na kuacha kutoa kadi zao kutumika na ndugu zao kwa kuwa kosa na kadi hizo zikikamatwa na kufungiwa kupata huduma.
Tahadhari hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juu ya zoezi la uhakiki wa wanachama na huduma linaloendelea katika vituo mbalimbali vya matibabu nchini.
“Naomba niwape tahadhari wanachama wetu, tumebaini wapo wanaowapatia ndugu zao vitambulisho ili wakapate huduma za matibabu, hiyo ni matumizi mabaya ya kadi na katika zoezi hili ambalo tunalifanya tukikukamata tunafunga matumizi ya kadi na kutaka kurejeshwa kwa fedha ambazo zimetumika kwa matibabu isivyo halali,” alisema Mkurugenzi Mkuu Konga.
Akizungumzia mambo makubwa yaliyobainika katika zoezi la uhakiki vituoni ni pamoja na matumizi mabaya ya kadi kwa wanachama kutoa kadi zao kwa wasio wanachama wa Mfuko na hivyo kupata huduma kinyume cha Sheria na utaratibu wa mfuko.
"Wapo baadhi ya wanachama wanaacha kadi zao vituoni ambapo jumla ya kadi 2,490 zimepatikana vituoni. Wanachama wanakumbushwa kuondoka na kadi zao mara baada ya kupata huduma na si kuziacha kwani ni kinyume cha utaratibu, niwaombe sana watoa huduma kutoa taarifa ya uwepo wa kadi kupitia Ofisi zetu za Mfuko,” alisema Bw. Konga.
Kwa upande wa utoaji wa huduma, imebainika kuwa baadhi ya vituo kutozingatia utaratibu wa uhakiki wa wanachama kabla ya huduma hivyo kuruhusu watu wasiostahili kupata huduma kwa gharama za Mfuko kitendo ambacho hakipaswi kufanyika.
Kutokana na hayo, amesema kwamba hatua zinazochukuliwa kukabiliana na changamoto hizo ni pamoja na kuzuia matumizi ya kadi 3,589 za wanufaika zilizokuwa na taarifa zenye shaka na kuwataka kufika kuhakiki taarifa zao kama ilivyoelekezwa awali na Mfuko.
“Tunafanya uchambuzi wa matumizi ya kadi zote zilizobainika kutumika kinyume cha utaratibu na kuchukua hatua stahiki, tunazuia malipo ya huduma zote za matibabu zilizobainika kuwasilishwa kinyume na utaratibu uliowekwa na Mfuko, tunaongeza wigo wa kuweka watumishi wa Mfuko vituoni ili kuimarisha zoezi la uhakiki wa wanachama na utoaji wa huduma pamoja na kuongeza matumizi ya utambuzi wa wanachama kwa kutumia alama za vidole na sura kwa vituo vya kimkakati ikiwemo Kliniki za Kibingwa, Hospitali ngazi ya Rufaa, Kanda na Taifa,” alisema Bw. Konga.
Kutokana na hayo, ametoa wito kwa wanachama, watoa huduma na wadau wote wa Mfuko kuhakikisha kila mmoja anaulinda mfuko.