NA FRESHA KINASA
WANAFUNZI wanaosoma katika shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara wamehimizwa kutoa taarifa bila kuogopa wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia bila kujalisha wanaowafanyia vitendo hivyo ni ndugu zao wa karibu ili kuwezesha Serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria wahusika wa vitendo hivyo.

Hayo yamebainishwa Julai 27, 2023 na Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Bunda,Maria Marco John wakati wa zoezi la utoaji wa elimu ya ukatili wa kijinsia katika shule za msingi Muungano, Busambara na Nakatuba zilizopo katika Halmashauri hiyo.

Maria amesema kuwa, watoto wengi wamekuwa wakikumbana na kadhia ya kufanyiwa vitendo mbalimbali vya ukatili ikiwemo kulawitiwa, kupigwa isivyotakiwa na kunyima haki zao hivyo wasiwafumbie macho wanaowafanyia vitendo hivyo bila kuogopa.
"Mila na desturi ni sababu za ukatili wa kijinsia, mfano ukeketaji na ulawiti hizo zinatokana na mila. Sababu nyingine ni uelewa mdogo wa jamii, malezi yasiyofaa na umaskini. Sababu hizi zimekuwa zikichangia aina nne za ukatili ambao ni ukatili wa kingono, Kimwili, kisaikolojia na kiuchumi," amesema Maria.

Kwa upande wake Restuta Malima kutoka Ofisi ya Elimu Wilaya ya Bunda amesema kuwa, ukatili una madhara mengi ikiwemo kuchangia kuzalisha ajira za utotoni, magonjwa ya kuambukiza, ulemavu, kuathirika kisaikolojia, kifo na kurudisha nyuma maendeleo ya Jamii na familia pia.
Naye Robnson Wangaso Mratibu wa mradi wa 'Funguka Paza Sauti kutokomeza ukatili wa Kijinsia kutoka Shirika la VIFAFIO lililopo Musoma mkoani Mara amesema, shirika hilo linatekeleza mradi huo kuhakikisha vitendo vya ukatili wa kijinsia vinatokomezwa na jamii yote inashiriki mapambano hayo kupitia elimu wanayoitoa.
"Mradi huu ambao awamu ya kwanza uliisha ukiwa na thamani ya shilingi milioni 37 na awamu ya pili FCS wametoa shilingi milioni 22 na mradi huu utaisha mwezi Oktoba mwaka huu nia yetu kupambana na ukatili tunashirikiana na Halmashauri ya Bunda na Musoma ambako mradi huu tunautekeleza kutoa elimu na Kuzindua mwongozo wa kitaifa wa dawati la ulinzi na usalama wa mtoto shuleni na nje ya shule. tumekuwa tukitumia matamasha, mikutano na wadau kutoa elimu ya ukatili."