NA MWANDISHI WETU
WANANCHI wamepongeza huduma za usajili wa wanachama kupitia Mpango wa Vifurushi zinazotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) katika Maonesho ya 47 ya Sabasaba.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliofika katika banda la NHIF kupata huduma, wamesema,Mpango wa Vifurushi vya Bima ya Afya ni mkombozi kwa kuwa unamuwezesha kila mwananchi kujiunga na kunufaika na huduma za matibabu.
"Huduma za matibabu kwa sasa ni gharama kubwa, NHIF mnastahili pongezi kwa kuanzisha mpango huu ambao ni nafuu na unamuwezesha kila mtu kuwa na fursa ya kujiunga, unapokuwa na kitambulisho cha matibabu unakuwa na ujasiri wa maisha," alisema Bw. Donald Nyamba aliyefika bandani hapo.
Akizungumzia kuhusu usajili wa watoto kuunganishwa na wazazi alisema ni jambo zuri ambalo linahamasisha kila mwananchi na familia yake kujiunga na Bima ya Afya.
"Huu utaratibu ni mzuri japokuwa umechukuliwa kwa mtazamo hasi na jamii lakini mnazo sababu nzuri kabisa hivyo ni vyema mkaendelea kutoa elimu zaidi ya dhana ya bima ya afya ili kila mwananchi aone umuhimu wa kujiunga na kuulinda Mfuko," alisema Bw. Nyamba.
Naye mkazi wa Pugu Kajiungeni Bi. Marietha Ngasa alitoa wito kwa wananchi kujiunga na NHIF kwa kuwa ni njia rahisi ya kujihakikishia huduma za matibabu wakati wowote.
"Ukiumwa au familia yako ikapatwa na maradhi ndio utajua umuhimu wa bima ya afya, mimi ni shuhuda mzuri ambaye nimeona kwa macho yangu kadi ya NHIF ikiokoa uhai wa mwanangu ambapo bila kadi nisingeweza kumtibia kutokana na gharama yake kuwa kubwa hivyo tumieni fursa hii kujiunga," alisema Bi. Ngasa.
Kwa upande wa Mfuko umewahakikishia wananchi kuwa umejipanga kuwahudumia wananchi kwa huduma bora na za haraka.
Akizungumzia hill Meneja Masoko wa NHIF, Bw. Hipoliti Lello amewaomba wananchi kutembelea banda la NHIF ili waweze kujisajili na hatimaye wanufaike na huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha.