NA VERONICA MWAFISI
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema moja kati ya mbinu ambazo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza kwa wananchi wote ni kushiriki katika kubuni mbinu mbalimbali zitakazowawezesha wananchi kujimudu na kuendesha maisha yao pasipokuwa na changamoto yoyote.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akitazama miti ya mbogamboga katika shamba darasa la kilimo cha kisasa kinachotekelezwa na kikundi cha walengwa wa TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.
Mhe. Kikwete ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi na walengwa wa TASAF wa Kata ya Janga, Mtaa wa Mwembebaraza katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.
Mhe. Kikwete amesema kuwa, Rais Dkt. Samia amekuwa akitoa fedha nyingi ili ziweze kutumika kupitia mbinu na ubunifu mkubwa wenye ubora ili kuweza kuwainua wananchi kiuchumi.
Mhe. Kikwete ametoa pongezi kwa wananchi na watendaji wakiwemo viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kwa kuhakikisha utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya miradi ya TASAF inatekelezeka kupitia kilimo cha kisasa.
Mhe. Kikwete amesema tangu aanze ziara za kikazi katika baadhi ya mikoa amekuwa akikutana na shuhuda na bunifu wa vitu mbalimbali hivyo ni dhahiri kuwa wananchi na walengwa wa TASAF wamekuwa wakifaidika kupitia bunifu za vitu mbalimbali.
Naye, Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Bi. Sijaona Muhunzi amesema katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha wanatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ajira za muda, mradi wa kuweka akiba na kukuza.
Katika hatua nyingine, Mhe. Naibu waziri Kikwete amefanya kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya Kibaha ambapo amewataka watumishi wa halmashauri hiyo kujiwekea malengo ya utendaji kazi ili kuboresha kazi zao kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete anaendelea na ziara ya kikazi ya wiki moja katika Mkoa wa Pwani kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao pamoja na kukagua utekelezaji wa Miradi ya TASAF.