DODOMA-Serikali ya Tanzania imepokea ugeni wa watu 10 kutoka nchini Afrika Kusini waliofika nchini kwa lengo la kujifunza juu ya ufugaji nyuki hasa kwenye uanzishwaji wa Manzuki na Hifadhi za nyuki, maandalizi na ukaguzi wa Manzuki pamoja na kuzuia na kudhibiti wadudu kwenye ufugaji nyuki.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Deusdedith Bwoyo amesema wageni hao kutoka nchini Afrika Kusini wamehamasika kuja hapa nchini kujifunza namna shughuli za ufugaji nyuki zinavyofanyika.
“Kule Afrika Kusini tumeambiwa wana uwezo wa kuzalisha tani 2000 kwa mwaka wakati asali inayohitajika ni tani 4000 kwa mwaka, Sisi huku tuzalisha tani 32,691 kwa mwaka na tunatumia asali hiyo ndani ya nchi karibia asilimia 90,” amesema Bwoyo.

Naye, Kiongozi wa Wajumbe hao ambaye ni Mkuu wa Idara ya Kilimo na Maendeleo Vijijini Kaskazini Magharibi mwa Afrika Kusini, Zakaria Thupi Mokgathlha, amesema Tanzania ni nchi ambayo imepiga hatua kubwa kwenye eneo la ufugaji nyuki, hivyo wamekuja kujifunza ili waweze kupata ujuzi utakao wasaidia kujiimarisha kwenye neo hilo.
“Tumekuja kuangalia Tanzania inavyofanya kwenye eneo hili ili tutakavyorudi kwetu tukaweke mikakati ya kuimarisha sekta hii,” amesema Zakaria.
Katika ziara hiyo, Wataalamu hao watatembelea Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki kilichopo mkoani Tabora uongozi wa mkoa huo pamoja na vikundi vya wafuga nyuki vya mkoa huo.