DODOMA-Waziri wa Viwanda na Biashara,Mheshimiwa Dkt.Ashatu Kijaji (Mb) amesema, Serikali itaenda hatua kwa hatua kuhakikisha changamoto wanazopata wenye viwanda zinatatuliwa na kushughulikiwa kwa wakati.
Dkt.Kijaji amesema hayo leo Julai 26,2023 alipotembelea Kiwanda cha Mbolea ITRACOM kilichopo Nala jijini Dodoma kujionea uzalishaji wa mbolea katika kiwanda hicho.
Aidha, amekipongeza kiwanda hicho kwa utengenezaji wa mbolea usiokua na mchanganyiko wa asilimia 100 ya madini, bali asilimia 50 ni samadi na asilimia 50 ni madini ambao unaleta uhai wa ardhi kwa uasili na ubora wake
Amesema, baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda hicho kwa awamu ya kwanza, kitaweza kuzalisha tani millioni 1.2 kwa mwaka huku matumizi ya ndanj ya nchi ni tani 650,000 hivyo hakuna sababu ya kuagiza mbolea nje ya nchi.
Dkt.Kijaji amesema, amezikaribisha nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla ikiwemo Kenya ambayo tayari imeshanunua tani 3000 za mbolea kununua mbolea kutoka ITRACOM kutoka Dodoma Tanzania.