NA GODFREY NNKO
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Dkt.Angeline Mabula ameonesha kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa Mradi wa Samia Housing Scheme Kawe chini ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Mradi huo ambao unatekelezwa katika eneo la Tanganyika Packers lililopo Kawe ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, mbali na matarajio ya kuja kuwapa Watanzania makazi bora pia umefungua fursa za ajira kwa Watanzania kutoka ndani na nje ya jiji.
"Nitoe pongezi kwa National Housing, ongezeni kasi, lakini nitoe rai kwa wale wote ambao wanazo fursa za kuendeleza, uendelezaji wa nyumba bado ni mkubwa;
Dkt.Mabula ameyabainisha hayo Julai 12, 2023 baada ya kufanya ziara katika mradi huo wa nyumba 560 ili kujionea maendeleo yake huku akiwataka wafanyakazi wanaotekeleza mradi huo kufanya kazi kwa bidii, uaminifu na ubora kwani pindi nyumba hizo zitakapokamilika mchango wao utaonekana siku zote.
"Hizi nyumba tunazoziona hapa tayari watu wameshafanya booking, sasa uone ni jinsi gani kuna uhitaji wa nyumba, katika Jiji la Dar es Salaam. Na, kwa sensa iliyopita (Sensa ya Watu na Makazi 2022) mwaka 2022 tuna uhitaji wa nyumba zaidi ya milioni tatu na laki nane.
"Ambapo kama ni kwa kasi na spidi ya kawaida ya kujenga zinatakiwa zijengwe nyumba zisizopungua laki tatu kwa mwaka, sasa uwezo huo tunao? Hapa, National Housing wanajenga, nitoe rai kwa makampuni na taasisi zingine, uhitaji wa nyumba ni mkubwa sana.
"Kwa hiyo, tunahitaji kushirikiana na taasisi zote ambazo zinafanya kazi ya uendelezaji miliki, ili kuweza kuziba pengo hilo la nyumba ambalo lipo, na ukiangalia kwa Watanzania tupo milioni 61, wastani wa familia moja ni kama watu wanne.
"Lakini, ukiangalia ni wangapi ambao wanakaa na watu hao wanne na wana uwezo wakuwa na nyumba za kuweza kuwahifadhi wote, ni wazi kuna watu unakuta wanabanana kwenye vyumba vyao.
"Kwa hiyo, uhitaji wa nyumba bado ni mkubwa, lakini habari njema zaidi ni kwamba bajeti iliyoisha mwaka huu tuliomaliza mwezi wa sita, tayari kwa wale ambao wanakwenda kununua zile nyumba za gharama nafuu wameondolewa lile ongezeko la thamani la VAT.
"Kwa hiyo, kama ni nyumba ya milioni 50 kushuka chini, utainunua bila ongezeko la thamani, kwa hiyo tunachofanya ni kuhakikisha nyumba za aina hiyo zinajengwa nyingi ili Watanzania waweze kununua na waweze kupata makazi yao,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.
Mbali na hayo, Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kutumia teknolojia ya kisasa ili kuweza kuongeza nyumba za makazi ambazo zitasaidia kupunguza pengo la mahitaji ya nyumba nchini.
Pia, amewataka vibarua wanaofanya kazi katika mradi huo kuwa waaminifu na kujiepusha na vitendo viovu ukiwamo wizi wa vifaa kwani kwa kufanya hivyo kutasababisha wao kukosa uaminifu na hivyo kukosa kazi.
Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesisitiza kuwa, uaminifu ni nyenzo muhimu ambayo kila mtu anayehusika na utekelezaji wa mradi huo anapaswa kuwa nayo ili kuweza kutimiza malengo ya mtu binafsi, lakini pia malengo ya shirika ambayo yanatarajia mradi huo ukamilike kwa wakati katika ubora na kwa viwango vya hali ya juu.
“Tutekeleze mradi huo kwa uaminifu mkubwa kwani Rais wa Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan ameliridhia NHC kupata shilingi bilioni 176 kwa ajili ya kuiamsha miradi iliyokuwa imelala na kuianzisha mingine mipya,"amesema Waziri Dkt.Mabula.
NHC
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw.Hamad Abdallah akizungumza na waandishi wa habari waliotaka kujua maendeleo ya mradi wa nyumba za makazi 560 zinazotekelezwa na NHC katika eneo la Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam amesema, mauzo ya nyumba hizo yamefikia asilimia 82.
"Leo tulikuwa na ziara ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Dkt.Angeline Mabula kikubwa alikuja kuangalia progress ya Mradi wetu wa Samia Housing Scheme.
"Huu ni mradi ambao unafanyika maeneo ya Kawe zamani ukiitwa Tanganyika Packers, ni mradi wa nyumba za makazi takribani 560 na mpaka sasa hivi kuna maendeleo mazuri, tunaendelea na kazi na tunaelekea kwenye floor ya nne.
"Na tayari tumeshaanza kuweka tofali kuanzia ground floor, kwa maana ya floor ya sakafu, upande wa mauzo tayari mradi huu umechangamkiwa vizuri kabisa na Watanzania zaidi ya asilimia 82 ya mradi mpaka wiki iliyopita tulikuwa tumeshauza.
"Na matarajio yetu ni kuwa itakapofika mwezi Februari mwakani tutakuwa tumemaliza mradi huu, kwa asilimia 100 ili tuweze kuanza phase two kwa Dar es Salaam, lakini matarajio vile vile kuanzia mwezi ujao tutaanza mradi kama huu katika Jiji la Dodoma.
"Na ni mradi tunauita Samia Housing Scheme jumla una nyumba 5000, leo hii mnaziona hapa ni nyumba 560 ambazo ni zaidi ya asilimia 10, Dodoma tunakwenda kuanza nyumba 100.
"Lakini, wakazi wa Dodoma wakichangamkia mradi tutaenda nyumba 200 kwa mwaka huu wa fedha ambao tumeanza hii Julai, lakini mpango wenyewe ni wanyumba 5000 kama nilivyozungumza ambapo mradi utaifikia Tanzania nzima.
"Inategemea tu na soko lipo sehemu gani, kwa sababu sisi tunajiendesha kibiashara hivyo ni lazima tujenge sehemu ambayo mwisho wa siku tutapata wanunuzi wa mradi.
"Lakini hii ni sehemu tu ya miradi ambayo tunafanya, Dodoma tutakuwa na miradi mingine, kuna eneo linaitwa Medeli tutakuwa na Medeli Phase Three ambayo ni nyumba takribani 200 ambayo nayo tunakwenda kuanza mwaka huu wa fedha.
"Lakini vile vile tutakuwa na nyumba za gharama nafuu, katika Jiji la Dodoma vile vile na matarajio yetu tunaweza kufanya mradi katika Mji wa Serikali-Mtumba kwa takribani nyumba 100 kwa ajili ya wafanyakazi.
"Kwa hiyo, kwa ujumla tunakwenda vizuri na niwahakikishie Watanzania mradi huu tunaufanya na utakuwa ni mradi ambao una viwango vizuri kabisa.
"Na ndani ya miezi miwili tayari tutakuwa na nyumba za mifano, tutakuwa na nyumba ya mfano ya vyumba vitatu, nyumba ya mfano ya vyumba viwili na vile vile na ile tunaita studio apartment.
Mbali na hayo, Mkurugenzi Mkuu wa NHC amesisitiza kuwa, wanaendelea kutekeleza miradi yao kisasa ikiwemo kuzingatia teknolojia mbalimbali katika ujenzi.
"Bahati nzuri na sisi tumekuwa tunaenda na teknolojia mbalimbali katika ujenzi na tunazijaribu, sasa hivi tuna teknolojia ambayo tunaifanyia majaribio, lakini katika majaribio ambayo tunayafanya kuna vitu vitatu vikubwa mabavyo tunaviangalia.
"Kwanza ni gharama ya ile teknolojia, kwa sababu mwisho wa siku sisi tunajenga ili tupate wanunuzi au wapangaji, na wanunuzi maana yake wapate nyumba kwa gharama nafuu, kwa hiyo teknolojia ambayo tutaichagua ni ile ambayo itatupa gharama nafuu.
"Lakini vile vile itatupa quality nzuri ya kazi, unajua Watanzania au sehemu kubwa ya watu nyumba ni life commitment Wazungu wanasema, ni ndoa ya maisha, kwa sababu kuna watu ambao wanawekeza fedha zao na ana uwezo wa kumiliki nyumba moja tu.
"Kwa hiyo akimiliki hiyo nyumba, lazima umtengenezee nyumba ambayo ni madhubuti,na si nyumba ambayo amefanya life commitment halafu unampatia nyumba ambayo ataishi miaka mitano au sita halafu baada ya hapo anaingia kwenye matatizo.
"Kwa hiyo, ubora wa hiyo nyumba. Lakini, jambo la tatu ni tunaweza kuzalisha hizo nyumba kwa kiasi gani, tunaweza kuzalisha nyumba ngapi kwa wakati gani, ni jambo lingine ambalo tunaliangalia, kwa hiyo hizo teknolojia tunaziangalia.
"Tayari tumeshajaribu teknolojia mbalimbali, timu zetu za wataalamu wa ndani wameshaenda nchi mbalimbali mwezi uliopita kuna watu walikuwa Kenya wameangalia National Housing ya Kenya wanafanya nini.
"Kuna teknolojia wanaitumia, na sisi vile vile tunajifunza hiyo teknolojia kuangalia itatupatia nyumba za namna gani, kwa gharama gani, lakini vile vile teknolojia hiyo ina uwezo wa kujenga nyumba nyingi kwa muda mfupi.
"Lakini, cha mwisho teknolojia hiyo inakubalika kwa namna gani kwa wanunuzi wa nyumba, leo hii Watanzania wamezoea kuona nyumba ambazo lazima zijengwe na tofali la nchi sita.
"Teknolojia hiyo ambayo inatumika Kenya utaona siyo nchi sita ni nchi mbili ukuta, lakini katikati kuna kitu kinaitwa insulation kwa ajili kuzuia joto au baridi isiingie ndani, lakini madhubuti,ni ukuta madhubuti sana lakini ni nchi mbili au nchi tatu.
"Watu wetu ukimwambia hili ghorofa tunajenga na ukuta wake ni nchi mbili au tatu atasema mimi siwezi, lakini lazima tuwape elimu, tuwazoeshe na wazoee suala hilo, baada ya hapo mnaaza kuzalisha hizo nyumba.
"Hatutaki tuzalishe halafu zitudodee kwa sababu watu hawajazoe hiyo teknolojia, kwa hiyo kuna vitu ambavyo tunakwenda taratibu, lakini kuna vitu ambavyo tutakwenda haraka kwenye teknolojia.
'Bahati nzuri, Mheshimiwa Waziri amekua anaenda nchi mbalimbali, akienda nchi mbalimbali mbali na mambo ya sekta ya ardhi anakwenda vile vile kwenye nyumba kuangalia, na akiona tu teknolojia katika nchi fulani, anatuhimiza na sisi tuiangalie, tuisome halafu tuijaribu.
"Kwa hiyo, kuna teknolojia ambayo tunaijaribu, nyumba karibu 20 tutaangalia Dodoma, lakini ni hatua kwa hatua tuangalie teknolojia hiyo inakubalika, inapokelewa kwa namna gani, kwa gharama gani, ni madhubuti kiasi gani, baada ya hapo tunafanya maamuzi.
'Kwa hiyo, sisi ni watu ambao tupo flexible, lakini teknolojia ambayo inaitwa tunnel form, tunnel ni teknolojia maarufu sana, inatumika nchini Uturuki, timu zetu zilishakwenda Uturuki mara kadhaa kuisoma, unaweza ukajenga jengo la ghorofa 10 kwa muda mfupi sana.
"Chini ya miezi sita, miezi mitatu tayari una jengo la ghorofa 10 na umeshalimaliza na watu wanaishi, sasa hii ni teknolojia, kwa hiyo tunaziangalia teknolojia mbalimbali,lakini mwisho wa siku Watanzania wanahitaji nyumba ambazo ni nafuu, lakini ambazo zina ubora.Hivyo, ndivyo vitu vya msingi ambavyo tunaviangalia,"amefafanua kwa kina Mkurugenzi Mkuu wa NHC.