Waziri Mkuu aagiza mafuta ya Kanda ya Kaskazini, Ziwa yachukuliwe Tanga

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Nishati iratibu ununuzi wa mafuta kutoka mikoa ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa ili yachukuliwe kutokea Tanga badala ya Dar es Salaam.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akifafanuliwa jambo na Meneja Mkazi wa Kampuni ya Maweni Limestone Limited (Huaxin Cement), Jing Changxi, wakati alipotembelea kiwanda hiko, akiwa katika ziara ya siku moja mkoani Tanga Julai 1, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Ametoa agizo hilo Julai Mosi, 2023 mara baada ya kukagua uboreshaji wa bandari ya Tanga na hifadhi ya mafuta kwenye matenki ya GBP, eneo la Raskazoni, jijini Tanga.

"Mikoa ya Mara, Mwanza, Manyara, Arusha, Kilimanjaro inafuata mafuta Dar es Salaam sababu ya mazoea lakini upatikanaji rahisi ni hapa Tanga, upatikanaji wa haraka sababu ya teknolojia ni hapa Tanga. Wizara ya Nishati watekeleze maelekezo haya ili wauzaji wa mafuta wayafuate Tanga," amesema.

Waziri Mkuu amesema endapo makampuni yote ya mikoa ya Kaskazini yatachukulia mafuta Tanga, uchumi wa mkoa huo utakua kwa haraka.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akitembelea na kukagua maendeleo ya uboreshaji wa shughuli za Bandari ya Tanga, akiwa katika ziara ya siku moja mkoani humo Julai 1, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
 
Akielezea kuhusu uwekezaji kwenye hifadhi hiyo, Waziri Mkuu amesema uwekezaji uliofanyika ni mkubwa kwani matenki yaliyopo yanaweza kupokea mafuta moja kwa moja kutoka bandarini na kuhifadhi lita hadi milioni 200. “Huu ni mkakati wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuendeleza uchumi wa nchi yetu. Wakati Serikali inaongeza uwezo wa kusimamisha meli zaidi bandarini, tutahakikisha kuwa uwekezaji huu unaleta faida kwa mwekezaji na unaongeza ajira kwa wanaTanga,” amesema.

Mapema, akitoa taarifa kuhusu hifadhi ya matenki ya GBP, Mkurugenzi Mtendaji wa GBP, Bw. Badar Sood alisema ujenzi wa matenki hayo ulianza mwaka 2002 yakiwa na uwezo wa kuhifadhi lita milioni 25 huku wakipokea meli zenye uwezo wa lita 6,000 tu.


"Hivi sasa tunaweza kuhifadhi lita milioni 200, tunaweza kupokea bidhaa mbili kwa wakati mmoja. Tunapokea hadi meli zenye ujazo wa lita 70,000 na tunaweza kupakia lita milioni tano hadi sita kwa siku kwenye malori na kupakia mabehewa 20 kwa wakati mmoja ndani ya saa tatu,” amesema Bw. Badar.


Akiwa kwenye bandari ya Tanga, Waziri Mkuu alipokea taarifa ya uboreshaji wa miundombinu na kuelezwa kuwa ujenzi wa gati mpya umekamilika kwa asilimia 99 na kwamba zimebakia kazi ndogo za kukamilisha mifumo ya umeme.

“Uboreshaji wa bandari ya Tanga hadi sasa umegharimu sh. bilioni 429.2. Awamu ya kwanza ulihusisha uchimbaji wa eneo la kuingilia meli na kugeuzia lenye urefu wa km.1.7 na upana wa mita 75 kwa kina cha mita 10 na awamu ya pili ni kujenga gati yenye urefu wa mita 450,” alisema Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Juma Kijavaro.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametembelea kiwanda cha saruji cha Maweni na kupokea taarifa ya ujenzi wake unafanywa na kampuni ya HUAXIN ya China.

Akizungumza na watumishi wa kiwanda hicho na wananchi waliofika kiwandani hapo ,Waziri Mkuu alimhakikishia Meneja Mkazi wa kampuni ya Maweni Limestone Ltd, Bw. James Jing kwamba atapata makaa ya mawe ya kutosha kadri ya mahitaji yake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news