Waziri Simbachawene asisitiza tafiti za kimkakati

NA LUSUNGU HELELA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameitaka Taasisi ya UONGOZI (UONGOZI Institute) kufanya tafiti za kimkakati zitakazoweza kuibua masuala mbalimbali ya kiuongozi kwa lengo la kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Taasisi ya UONGOZI jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao. Wa pili kulia waliokaa ni Naibu Waziri wake, Mhe. Ridhiwani Kikwete na wa pili kushoto waliokaa ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo.

Waziri Simbachawene amesema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Taasisi ya UONGOZI jijini Dar es Salaam, ikiwa ni muendelezo wa kuzungumza na Watumishi kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.


Amesema tafiti hizo zinatakiwa zilenge katika kuibua mijadala ambayo itachagiza dhana ya utawala bora kwa kujikita zaidi kuibua changamoto zinazosababishwa na viongozi wenyewe Barani Afrika.

"Tunataka mje na tafiti zitakazosomwa duniani kote ambazo zitaleta ukombozi kwa wananchi wa Bara la Afrika hususan katika masuala ya uongozi mfano kwenye suala la rushwa," amesema Mhe. Simbachawene.

Amefafanua kuwa kwenye masuala ya uongozi bado kunahitajika tafiti nyingi ambazo zitatoa dira ya kuwaandaa viongozi vijana wenye mtazamo wa kimapinduzi.

Katika hatua nyingine Mhe. Simbachawene ameipongeza Taasisi hiyo kwa kazi kubwa inayofanya ya kuwaandaa viongozi wa ndani na nje ya nchi pamoja kukutana na kuzungumza na viongozi mbalimbali.

"Ninajivunia kwa kazi zenu kwani huko nje taswira yenu ni kubwa mno na ya kimataifa kutokana na jitihada zenu mnazofanya za kuhakikisha Afrika inakuwa na viongozi wenye kuwahudumia wananchi " amesisitiza Mhe. Simbachawene.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwan Kikwete ameihimiza Taasisi hiyo kuendelea kuandaa viongozi wa baadae watakaoweza kuendeleza mazuri yanayofanywa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. 
Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi yake, amesema atatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa ikiwa pamoja na kutoa tafiti zitakazoleta matokeo chanya katika jamiii na taifa kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news