Waziri Tabia: Rais Dkt.Samia, Mwinyi ni walezi wetu katika lugha ya Kiswahili

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mheshimiwa Tabia Maulid Tabia amewapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa kuwa mstari wa mbele kukiendeleza Kiswahili nchini.

Ameyamesema hayo Julai 4, 2023 katika Kongamano la Wahariri lililoandaliwa na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) ambalo liliangazia juu ya nafasi ya wahariri katika kusimamia matumizi ya Kiswahili sanifu kwenye vyombo vya habari nchini.

Kupitia kongamano hilo, mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdullah ambapo limefanyikia Ukumbi wa Sheikh Idris Abdul Wakil uliopo Kikwajuni jijini Zanzibar.

Aidha, kongamano hilo ni maandalizi ya kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani ambayo yatafanyika Julai 7, 2023 huku kauli mbiu ikiwa ni “Kiswahili Chetu; Umoja Wetu”.

"Niwapongeze Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Dkt.Hussein Ali Mwinyi walezi wetu hawa wawili kwa kukiendeleza, kukilea na kukikuza Kiswahili katika mikutano yao mbalimbali.

"Nakumbuka mwaka jana tuliadhimisha siku hii ya Kiswahili kwa kuandaa makongamano, na kumwakilisha Mheshimwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania jijini Paris nchini Ufaransa pale UNESCO kuadhimisha siku hii ya Kiswahili.

"Niseme tu kwamba wizara zetu mbili zinayo mikakati ya kukiimarisha Kiswahili kiwe bidhaa, kitufaidishe sisi Watanzania katika mambo mbalimbali.

"Kupokea wageni mbalimbali kuja kujifunza Kiswahili na vile vile kuzuzungumza na balozi zetu ambazo zinaiwakilisha Tanzania kwenda kueneza Kiswahili kwa kuwapelekea kamusi na vitabu mbalimbali ambavyo vinaonesha matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili.

"Vile vile tunaendelea na mkakati wa kuhamasisha matumizi bora ya Kiswahili hatujafikia kupitia BAKITA, BAKIZA na niwapongeze sana kwa kutoa maana sahihi za maneno ikiwemo misamiati.

"Changamoto ya utandawazi inapelekea kwamba vijana wetu hawa ile maana inayotoka BAKITA na wao wanatolea maana yao, kwa hiyo ipo hiyo changamoto na tunaendelea kupambana kwa kweli tuombe wahariri kukemea hayo masuala ili lugha yetu iwe fasaha na sanifu iweze kuimarika.

"Maadhimisho haya ya Kiswahili itakapofika tarehe 7, Julai yataadhimishwa duniani kote, lakini kikawaida, watu wote na macho yao yako hapa Zanzibar au niseme Tanzania hata Dunia inajua huku ndiko Kiswahili kilipozaliwa.

"Mheshimiwa Makamu wa Rais tunakushukuru sana sana, unatutia nguvu sana. Shughuli hii ni muhimu sana kwa ajili ya kukuza lugha yetu.

"Tarehe 6, tutakuwa na kongamano kubwa sana na tarehe saba litafungwa kongamano hilo, lakini usiku wa tarehe 7 Mheshimiwa tutakuwa na vionjo vya lugha ya Kiswahili kutakuwa na taarabu kutoka Mombasa, Burundi na kwingineko,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Tabia Maulid Tabia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news