NA MWANDISHI WETU
WIZARA ya Maliasili na Utalii imeamua kwenda na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwa kuanza kutangaza Utalii kidigitali katika Maonesho ya 47 Kibiashara ya Kimataifa Dar es Salaam, maarufu kama Saba Saba.
Mkurugenzi wa Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Thereza Mugobi (mwenye koti la kijani) akisikiliza maelezo kutoka kwa wataalamu ndani ya banda la Wizara ya Maliasili na utalii kwenye viwanja vya Saba Saba jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kutembelea banda la wizara hiyo, Mkurugenzi wa Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Thereza Mugobi amesema, hauwezi kuongelea utalii bila kuongelea mambo ya kidigitali na ndiyo maana wizara imeamua kwenda na mabadiliko hayo ya teknolojia yaliyopo duniani kwa taasisi na idara za wizara hiyo kutumia njia ya kidijitali kuonesha shughuli na huduma zao mbalimbali.
“Kwenye mabanda yetu Watanzania wataweza kuona utalii wetu kwa kupitia simu janja zao za mikononi (smartphone). Tuna QR Code kwenye kila banda ambazo watanzania wataskani kwa ajili ya kupata vivutio vilivyopo Tanzania nzima na kujua vivutio hivyo pamoja na huduma zinazotolewa na taasisi zetu,”amesema Dkt.Mugobi.
Katika maonesho hayo, wizara imejipanga vyema kuwahudumia wote wanaofika katika banda hilo kwa kasi zaidi kupitia njia hiyo ya kisasa tofauti na ilivyokuwa huko nyuma taarifa nyingi zilikuwa zikitolewa kwenye vipeperushi ambavyo ni mzigo kwa wageni.
Mkurugenzi wa Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Thereza Mugobi (kulia) akipokea zawadi kutoka kwa Meneja wa Masoko ya Ndani Bodi ya Utalii Tanzania, Bw. Felix John baada ya kutembelea Banda la Wizara hiyo kwenye Maonesho ya Saba Saba jijini Dar es Salaam.
Aidha, Dkt.Mugobi ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kujipatia huduma mbalimbali kwenye Banda la Maliasili na Utalii ambazo ni njia sahihi na rahisi ya kujipatia fursa mbalimbali kwenye sekta zilizopo chini ya wizara hiyo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii (TTB),Damasi Mfugale amefurahishwa na ufanisi wa kutangaza Utalii kidigitali katika maonesho hayo ya Sabasaba na kusema watahakikisha kila taasisi ya wizara itatangaza utalii kisasa zaidi.
Bw.Luca Hakili mkazi wa Jiji la Dar es Salaam licha ya kupendezwa na huduma zinazotolewa na taasisi mbalimbali za Wizara ya Maliasili na Utalii,amezipongeza kwa ufanisi wa taasisi hizo katika kutangaza maliasili zilizopo Tanzania kisasa zaidi.
Bw.Hakili ameongeza kuwa, kwake imekuwa ni fursa muhimu ya kujua rasilimali lukuki zilizopo nchini na fursa zilizopo kwenye Utalii, Misitu,Wanyamapori pamoja, Malikale na taasisi zingine.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii, Bw. Damasi Mfugale (mwenye miwani) akipokea maelezo kutoka kwa Mratibu wa Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii,Bw.Felix John baada ya kutembelea banda la wizara hiyo kwenye Maonesho ya Saba Saba jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine, katika banda la Wizara ya Maliasili na Utalii wakazi wa Dar es Salaam wamepata fursa ya kuangalia Filamu ya “Tanzania The Royal Tour” iliyosimamiwa na Mhe.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza baada ya kuangalia filamu hiyo mtoto, Feisal Seif amefurahishwa kupata fursa ya kuangalia filamu hiyo na kuwataka watoto wenzake kuja kuangalia na kujifunza mambo mengi kuhusu utalii, uhifadhi, maliasili na kuja kuona wanyapori.