ZAWA kuwafikishia wananchi hawa maji bure Unguja

ZANZIBAR-Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Mhe.Shaaban Ali Othman amesema, wizara hiyo kupitia taasisi yake Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) wanajipanga kusambaza huduma ya maji safi na salama kwa njia ya gari la maji katika maeneo ambayo wananchi wamekosa huduma hiyo ikiwemo eneo la Kilimani, Maisara, Michenzani jumba (block) namba kumi na kwingineko.

Kauli hiyo imekuja kufuatia malalamiko ya wananchi wa maeneo hayo kulalamikia ukosefu wa huduma hiyo tangu kuanza kwa ujenzi wa Mradi wa barabara ya Mnazi mmoja hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Unguja.

Akizungumza katika ziara maalumu iliyoandaliwa na wizara yake katika eneo hilo la mradi wa barabara hiyo, Mhe.Othman amesema katika kipindi hiki atahakikisha ZAWA wanawafikishia wananchi huduma hiyo kwa njia ya gari la maji bila ya kuwatoza fedha.

“Tutatoa maji bure katika kipindi hichi,narudia tena bure kwa maana ya bure hatutomchangisha mtu pesa, maji tunayo na magari yapo. kwani wizara zote mbili zinafanya kazi kwa mashirikiano makubwa na muda sio mrefu huduma ya maji itarudi kama kawaida, hivyo tutasambaza maji bure,"amesema Othman.

Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Joseph Kilangi amesema ukosefu wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo hayo umetokana na kuathirika kwa miundombinu ya maji wakati mradi wa barabara ukiendelea hivyo kupitia ziara hiyo imelenga kutafuta majibu ya kujua wapi mabomba ya maji yatapitishwa ili huduma hiyo irudishwe kwa wananchi.

Amesema, wizara yake imekubaliana na Wizara ya Mawasiliano na Ujenzi kupitisha mabomba ya maji pembezoni mwa barabara (walk way) hivyo, muda sio mrefu mradi huo utakamilika na huduma ya maji itarudishwa kwa wananchi kama kawaida.

Aidha,Katibu Mkuu Kilangi amewaomba radhi wananchi waliokosa huduma ya maji safi na salama katika kipindi hichi kwani Serikali ya Mapinduzni Zanzibar (SMZ) imejikita katika kuwaletea maendeleo wananchi wake, hivyo barabara ni muhimu na maji ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na wananchi wake.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Ujenzi, Khadija Khamis Rajab amesema, wizara yake inafanya kazi kwa mashirika makubwa na Wizara ya Maji, Nishati na Madini hiyo watahakikisha wanarudisha miundombinu ya maji na umeme yote iliyoathirika wakati wa ujenzi wa barabara.

Pia amesema, miundombinu ya umeme itakayoathirika itarudisha na taasisi husika Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) ili wananchi waendelee na harakati zao za maisha ya kila siku.

Wakati huo huo, akizungumza Mkurugenzi Mkuu ZAWA, Mhandisi Dkt.Salha amesema, maji yamejaa tele katika tenki la maji la Mnara wa mbao Kilimani, lakini hakuna jinsi ya kuwafikishia wananchi kutokana na miundombinu ya maji kuathirika, hivyo taasisi yake inajipanga kuwafikishwa wananchi huduma hiyo kama walivyotoa katika kipindi cha Mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Bomba la Maji safi na salama ambalo limekatwa kwaajili ya ujenzi wa barabara na kupelekea ukosefu wa huduma hiyo katika maeneo ya Kilimani, Maisara na maeneo ya Michenzani jumba namba kumi, Unguja.

“Taasisi yangu imeshatoa maelekezo dizaini na dayamita (design na diameter) ya mabomba ya maji ambayo Wizara ya Mawasiliano na Ujenzi watalazimika kununua kwa ajili ya kurudisha huduma hiyo kwa wananchi kama kawaida,”amesema Mhadisi Dkt.Salha.

Kwa upande wa wananchi akizungumza Mkaazi wa Kilimani, Bi. Luluwa Salum Ali (36) ameiomba Serikali mara tu mradi wa barabara utakapo kamilika warudishiwe huduma hiyo kwani hivi sasa wanalazimika kununua gari la maji kwa bei ya sh. 15,000 kwa kujaziwa tenki la lita 1500 au kwenda kukaa foleni kwa jirani ambaye amechimba kisima huko bei ya kujaziwa tenki la maji la lita 1500 bei ni sh. 5000, lakini watu ni wengi lazima mtu apange foleni.

“Siwezi kuilamu Serikali najua tunatengenezewa barabara, lakini ninachokiomba kwa mamlaka husika barabara itakapokamilika tu, basi turudishiwa huduma hiyo kwani tumekabiliwa na kipindi kigumu hasa ukiangaliwa tofauti ya kipato kwa wananchi,”amesema Luluwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news