Ahadi za Mwana TANU

NA LWAGA MWAMBANDE

CHAMA cha Tanganyika African National Union (TANU) ni chama kilichosaidia zaidi katika harakati za kuikomboa nchi yetu katika mikono ya ukoloni chini ya uongozi thabiti wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Rais wa TANU Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa na Kiongozi wa Wanawake Bibi Titi Mohamed katika moja ya Mikutano ya Kampeni za TANU wakati huo.(File/VPO).

Aidha, malengo makubwa ya chama hicho ambacho kilianzishwa Jumatano ya Julai 7, 1954 ilikuwa ni ukombozi wa nchi yetu, lengo ambalo kwa kiasi kikubwa lilitimia kwa mafanikio makubwa tena bila kumwaga damu.

Hiki ni chama ambacho kinaonesha namna ambavyo wakati huo, viongozi walikuwa na dhamira ya dhati kwa ustawi bora wa chama na Taifa kwa ujumla ndiyo maana wakajiwekea ahadi.

Miongoni mwa ahadi hizo ni pamoja na kutambua wazi kuwa, binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja, nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote.

Pia, nitajitolea nafsi yangu kuondoa umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma.Rushwa ni adui wa haki. Sitapokea wala kutoa rushwa.

Ahadi nyingine ni cheo ni dhamana. Sitakitumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu.Nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na kutumia elimu yangu kwa faida ya wote.Nitashirikiana na wenzangu wote kuijenga nchi yetu.

Mbali na hizo kuna ahadi ya nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.Nitakuwa mwanachama mwaminifu wa TANU na raia mwema wa Tanganyika na Afrika. Na, nitakuwa mtiifu na mwaminifu kwa Rais wa Serikali ya Tanganyika.​

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, bado kila mmoja wetu ana nafasi ya kuzirejea ahadi hizo katika kizazi za sasa na kuzitafakari na pale ambapo unabaini kuna mahali unahitaji kujisahihisha, basi fanya hivyo kwa manufaa ya familia, jamii na Taifa. Endelea;


1.Taifa moyoni mwako, siyo mdomoni mwako,
Chemchem moyo wako, waleta heshima kwako,
Mwenendo matendo yako, yachagiwe toka huko,
Ahadi za Mwana TANU, hebu kazisake huko.

2.Binadamu wote sawa, iwe ni ahadi yako,
Na Afrika tuko sawa, wa tofauti hawako,
Utumike sawasawa, kwa weledi wote wako,
Ahadi za Mwana TANU, hebu kazisake huko.

3.Ya kwamba unaelewa, maadui zetu wako,
Wala usije kulewa, kwa kufanyafanya yako,
Ujinga sio uzawa, hebu piga vita huko,
Ahadi za Mwana TANU, hebu kazisake huko.

4.Ushinde umasikini, magonjwa yasiwe huko,
Dhuluma weka kapuni, rushwa isiweko huko,
Haki iwe mkononi, katika maisha yako,
Yanayotoka moyoni ndiyo yanayoshibisha.

5.Kwa wewe kutoa rushwa, isiwe tabia yako,
Wala kupokea rushwa, kuwa ni adui kwako,
Bali uzidi kukoshwa, uonevu usiweko,
Ahadi za Mwana TANU, hebu kazisake huko.

6. Nafasi uliyopewa, ni ya umma si ya kwako,
Ni dhamana umepewa, fanya utumishi wako,
Siyo kwa ndugu kugawa, kamba kuvutia kwako,
Ahadi za Mwana TANU, hebu kazisake huko.

6.Kote kasake elimu, iwe ni jukumu lako,
Na ukipata elimu, japo ni kwa nguvu zako,
Matumizi na yadumu, wafaidi wote kwako,
Ahadi za Mwana TANU, hebu kazisake huko.

7.Tena kidole kimoja, chawa watabaki kwako,
Upendelee umoja, kuijenga nchi yako,
Shirikiana pamoja, mtafanya ya mashiko,
Ahadi za Mwana TANU, hebu kazisake huko.

8.Useme kweli daima, fitina iwe ni mwiko.
Uwe ni raia mwema, wa nchi ya baba zako,
Usije ukasimama, kusaliti nchi yako,
Ahadi za Mwana TANU, hebu kazisake huko.

9.Ahadi za mwana TANU, hebu kazisake huko,
Zibakie kwako tunu, katika maisha yako,
Kusitokee fununu, kufanya vingine huko,
Ahadi za Mwana TANU, hebu kazisake huko.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news