DAR ES SALAAM-Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imetangaza kutumia ndege zake za kisasa za abiria na mizigo kwa wafanyabiashara, wanafunzi, wagonjwa na watalii wanaposafiri nchini India.
Mkurugenzi Mtendaji, Mhandisi Ladislaus Matindi amesema hayo baada ya ziara yake jijini Mumbai iliyolenga kuboresha huduma za usafiri wa anga ndani na nje ya Bara la Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Matindi amesema Soko la Mumbai, India linaangaliwa kwa wingi wa watu na uwezo wake kiuchumi ambapo linakadiriwa kuwa na watu takribani bilioni 1.4.
Kutokana na ukosefu wa ndege ya mizigo hapo awali, ATCL ililazimika kutumia ndege zake za abiria kulihudumia soko hilo hali iliyolazimu kuacha fursa nyingi za biashara zilizopo kwenye jiji hilo.
“India ni soko jipya la utalii kwa Tanzania, ambapo ATCL kwa kutumia ndege zetu za abiria tulifanikiwa kumiliki asilimia 80 ya abiria wote wanaosafiri kati ya Tanzania na Mumbai sawa na wastani wa abiria 66,080 kwa mwaka. Idadi hii ni ndogo sana ukilinganisha na abiria wote wanaosafiri nje ya nchi hiyo kila mwaka hususan watalii,”amesema Mhandisi.
Kwa upande wa watalii, Matindi amebainisha kuwa ATCL itaendelea kutumia ndege zake kubwa mpya za kisasa Boeing 787- 8 Dreamliner zenye utulivu angani kwa kiutilia maanani idadi kubwa ya abiria wanaoweza kusafirisha ili kuwezesha abiria kupata uzoefu wa pekee wa safari iliyojaa furaha na yenye kukumbukwa.
Amefafanua kuwa kwa kiasi kikubwa abiria wakiwemo watalii kutoka India wameendelea kufurahia huduma bora zinazotolewa na Kampuni hiyo ikiwemo huduma ya mtandao “Wifi” angani, vyakula vya asili kwa wasafiri pamoja na viburudisho.
Kwa upande wa ndege mpya ya mizigo Boeing 767- 300F, Matindi amesema ndege hii ya kisasa imeanza safari zake na imeendelea kusafirisha mizigo ya aina mbalimbali ikiwemo bidhaa zinazoharibika kwa muda mfupi na zile zenye uhitaji wa hali ya hewa ya kiwango fulani kama vile madawa.
Uwepo wa ndege hii yenye uwezo wa kubeba tani 54 kwa mara moja imewezesha Kampuni ya Glenmark Pharmaceutical, mojawapo ya makampuni makubwa ya utengenezaji wa madawa ya binadamu nchini India, kukubali kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usambazaji wa madawa ya Kampuni hiyo barani Afrika kwa kutumia ndege za ATCL.
Kampuni nyingine kubwa iliyokubali kuingia makubaliano na ATCL ni pamoja na MakeMyTrip inayohusika na uuzaji wa tiketi za ndege na uwezeshaji wa safari za kitalii nchini humo. MakeMyTrip ambayo inatumia tovuti yake kuuza tiketi za Air Tanzania ndani na nje ya India pia imekubali kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania kupitia tovuti hiyo.
Ameongeza kuwa wamefanikiwa pia kuanzisha mazungumzo ya mashirikano ya kibiashara ya kubebeana abiria (Interline Agreement) na Kampuni ya Ndege ya Vistara. Kampuni hiyo ina mtandao mkubwa kwa safari za ndani nchini India hivyo itarahisisha uunganishaji wa safari za ndani kwa abiria wa ATCL wanapofika jijini Mumbai.
Mhandisi Matindi amesema ziara hiyo vilevile imeanzisha mazungumzo na hospitali mbili (2) zilizopo jijini Mumbai kwa ajili ya kuingia makubaliano ya kibiashara.
Makubaliano hayo yatawezesha wagonjwa wanaotoka Tanzania kupata punguzo la gharama za matibabu wanapotumia ndege za ATCL. Kwa sasa ATCL ina mahusiano ya kibiashara na hospitali ya Kokilaben iliyoko Mumbai ambapo wasafiri wa ATCL hupata punguzo la gharama za matibabu wanapotibiwa katika hospitali hiyo.
Matindi pia amemshukuru Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Balozi Anisa Mbega kwa juhudi anazozifanya kutangaza fursa na vivutio vilivyopo Tanzania ikiwemo Maonesho nchini India ambapo ATCL inajipanga kushiriki katika maonyesho hayo.
ATCL yenye ndege za masafa ya mbali, kati na mafupi imeongeza safari za India kutoka siku nne (4) hadi tano (5) kwa wiki kuanzia Oktoba 2023 ili kukabiliana na ongezeko la abiria kwa safari zake za India.