Asante Mama Samia

NA LWAGA MWAMBANDE

LEO Agosti 6, 2023 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amenogesha Siku ya Simba (Simba Day) ambapo alikuwa mgeni rasmi huku akishuhudia mambo mazuri ya klabu hiyo kuelekea msimu ujao.

Kupitia tukio hilo muhimu ambalo baada ya shamrashamra mbalimbali, Simba SC wameumana na mabingwa wa Zambia, Klabu ya Power Dynamos, wageni hao waliambulia kichapo cha mabao 2-0.

Aidha, kikosi cha Simba SC kiliundwa na Ally Salim (1), Shomari Kapombe (12), Mohamed Hussein (15), Che Fondoh Malone (20), Henock Inonga (29), Sadio Kanoute (8), Willy Essomba Onana (7), Mzamiru Yassin (19), Kibu Denis (38), Said Ntibazonkiza (39), Clatous Chama (17).

Wachezaji wa akiba walikuwa ni Ahmed Feruzi (31), Israel Patrick (5), David Kameta (3), Kennedy Juma (26), Hussein Kazi (16), Fabrice Ngoma (6), Aubin Kramo (24), Abdallah Hamis (13), Jean Baleke (4), Moses Phiri (25), John Bocco (22), Peter Banda (11). Hussein Abel (30).

Ni kupitia mtanange wa kirafiki ambao umepigwa katika Dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam huku wafungaji wakiwa ni Leandre Willy Essomba Onana dakika ya tano na Fabrice Luamba Ngoma dakika ya 75.

"Ahsanteni wana Simba kwa kunialika kushiriki nanyi katika siku yenu muhimu hii leo. Hongereni kwa siku nzuri. Pongezi kwenu kwa kuendelea kutangaza utalii wa nchi yetu kwa kufikisha kibegi katika kilele cha Mlima Kilimanjaro."alibainisha mgeni rasmi Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema hii ni heshima kubwa kwa klabu hiyo na hivyo wana Simba wanamshukuru kwa kuwaunga mkono. Endelea

1.Asante Mama Samia, Rais wa Tanzania,
Umetukamilishia, siku tumefurahia,
Ni Simba ya Tanzania, salamu zetu sikia,
Tunakuunga mkono, kwa Visit Tanzania.

2.Afrika na dunia, Simba wametusikia,
Vile wameangalia, imetajwa Tanzania,
Hilo tunafurahia, nchi yetu kuchangia,
Tunakuunga mkono, kwa Visit Tanzania.

3.Simba hii Tanzania, nchi twaipalilia,
Kote tunakofikia, inasomwa Tanzania,
Ndivyo tulivyopania, kuinua Tanzania,
Tunakuunga mkono, kwa Visit Tanzania.

4.Leo umeangalia, yale tumejipangia,
Ujue tumepania, pazuri kupafikia,
Ni Simba ya Tanzania, ndivyo twaonesha njia,
Tunakuunga mkono, kwa Visit Tanzania.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news