Boli kutoka Tanzania linatembea hatari Afrika

DAR ES SALAAM-Watanzania wamekiri wazi kuwa, bado wana matumaini makubwa na wawakilishi wao katika michuano mbalimbali ya Kimataifa hususani Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Kwa nyakati tofauti wameieleza DIRAMAKINI jijini Dar es Salaam kuwa, licha ya changamoto za hapa na pale katika michuano hiyo, bado mbeleni kuna nuru kwa klabu kutoka nchini.

Hayo yanajiri ikiwa Agosti 18, 2023 timu ya KMKM ilijikwaa katika Ligi ya Mabingwa barani Afrika baada ya kuchapwa mabao 2-1 na St George ya Ethiopia.

Ni kupitia mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali uliopigwa katika Uwanja wa Azam Complex uliopo Kata ya Chamazi ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Timu hizo zitarudiana Agosti 27, 2023 Uwanja wa Abebe Bikila jijini Addis Ababa, Ethiopia na mshindi wa jumla atakutana na mabingwa watetezi, Al Ahly ya Misri.

"Ulikuwa ni mchezo mzuri, lakini kama inavyojulikana mara zote, mpira wa miguu huwa na matokeo ya aina mbili ambayo yanaweza kuwa ya kikatili au ya furaha, hivyo kupata au kukosa ni neema tu, kikubwa ni kujiandaa kwa safari ijayo,"amefafanua Said Khamis mkazi wa Mabibo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na DIRAMAKINI.

Aidha, wakati KMKM ikitoka kinyonge, wao Singida Fountain Gate (Big Stars) imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kusogea mbele kwenye Kombe la Shirikisho barani Afrika.

SFG vs JKU

Ni baada ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya JKU ya Zanzibar usiku wa Agosti 18, 2023 ndani ya Uwanja wa Azam Complex uliopo Kata ya Chamazi Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Mabao ya Singida Fountain Gate yalifungwa na viungo Marouf Tchakei dakika ya nne na 39 yote kwa penalti,Maurice Chukwu dakika ya 44 na Duke Abuya dakika ya 47.

Pia, kwa upande wa bao la JKU lilifungwa na Saleh Abdullah kwa penalti pia dakika ya 63 ya mtanange huo wa nguvu dimbani hapo.

Baada ya matokeo hayo, pande hizo zitarudiana Agosti 27, 2023 ndani ya Azam Complex na mshindi wa jumla atachuana na na Future ya Misri.

"Singida Fountain Gate imekuja kwa kasi sana katika soka la Tanzania na pengine, ikipata upenyo kidogo tu, hata watani wa jadi wataisoma namba, hii ni timu kubwa ambayo inaonekana ina maono mazuri na mikakati mizuri kuanzia kikosi, benchi la ufundi, walimu na uongozi kwa ujumla.

"Hivyo, huenda mechi ijayo ya marudio wakasonga mbele na wakapata nafasi ya kwenda kumenyana na Future, haya mageuzi ya kisoka yanapaswa kuungwa mkono na wadau wote nchini,"amebainisha John Julius mkazi wa Tandika Temeke katika mahojiano na DIRAMAKINI.

Azam FC vs Bahir Dar

Mbali na hayo, Azam FC nayo Agosti 20, 2023 iliambulia kichapo mabao 2-1 kutoka kwa wenyeji, Bahir Dar katika mchezo wake wa kwanza Raundi ya Awali Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Mtanange huo wa nguvu ulipigwa katika Uwanja wa Abebe Bikila jijini Addis Ababa, Ethiopia huku Fitsum Gebremariam dakika ya 20 na 60 akiwapa raha wenyeji hao.

Aidha,bao pekee la Azam FC lilifungwa na mshambuliaji wa wake, Idris Ilunga Mbombo dakika ya 72 ya mtanange huo.

Pande zote zitarudiana Agosti 25,2023 katika dimba la Azam Complex lililopo Kata ya Chamazi Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam na mshindi wa jumla atakwenda kumenyana na Club Africain ya Tunisia kuwania kuingia hatua ya makundi.

Yanga SC VS ASAS

Wakati katika michuano hiyo, baadhi ya timu zikionekana kupambana kufa na kupona, kwao mabingwa wa Tanzania, Yanga SC wameicharaza ASAS ya Djibouti mabao 2-0.

Kupitia mtanange huo uliopigwa Agosti 20,2023 ikiwa ni wa kwanza wa Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Uwanja wa Azam Complex Kata ya Chamazi ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, Yanga SC walionekana kuwa na furaha zaidi.

Stephane Aziz Ki dakika ya 22 na mshambuliaji Kennedy Musonda dakika ya 53 ndiyo walipeleka maumivu kwa ASAS ya Djibouti.

Hata hivyo, baada ya matokeo hayo, pande hizo zitarudiana Agosti 26, 2023 katika dimba hilo la Azam Complex jijini Dar es Salaam.

Matokeo ya mtanange huo yataamua mshindi wa jumla ambaye atakutana na mshindi wa jumla kati ya Otoho ya Kongo Brazzaville na El Mereikh ya Sudan kuwania tiketi ya makundi ya michuano hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news