BoT:Tanzania ina akiba ya fedha za kigeni dola bilioni 5.44 kufikia jana

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imebainisha kuwa, hadi kufikia Agosti 21, 2023 ilikuwa na akiba ya fedha za kigeni dola bilioni 5.44 ambazo zinatosheleza miezi 4.9 kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi.

Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Suleiman Missango (katikati kulia), akitoa wasilisho lake kuhusu masuala ya fedha za kigeni kwenye kikao na wahariri, waandishi wa habari na wadau wa sekta ya fedha nchini, makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam Agosti 22, 2023. (Picha na K-VIS Blog).

Hayo yamebainishwa leo Agosti 22, 2023 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tafiti za Uchumi BoT, Dkt.Suleiman Misango wakati akiwasilisha wasilisho kuhusu mwenendo wa hali ya fedha za kigeni nchini.

Ni mbele ya wahariri na waandishi wa habari nchini ambapo, Dkt.Misango alikuwa akizungumza kwa niaba ya Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba.

"Pamoja na kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa fedha za kigeni nchini hususani dola ya Marekani, hali ya upatikanaji wa fedha za kigeni imeendelea kuwa himilivu.

"Uhimilivu huo unatokana na kuendelea kuwepo kwa akiba ya kutosha ya fedha za kigeni nchini, hadi kufikia Agosti 21, 2023 akiba hiyo ilikuwa dola za Marekani milioni 5,441 (zaidi ya dola bilioni 5.44), ambayo inatosheleza miezi 4.9 mimi ninaweza kusema miezi mitano ya uagizaji wa huduma na bidhaa kutoka nje,"amefafanua DktMisago kwa niaba ya Gavana wa BoT.

Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa, kiasi hicho kinalingana na kipindi kabla ya changamoto za uchumi wa Dunia zilizopelekea kuwepo upungufu wa fedha za kigeni.

Aidha, miongoni mwa changangamoto hizo ni pamoja na vita kati ya Urusi na Ukraine, UVIKO-19,utekelezaji wa Sera ya Fedha ya kupunguza ukwasi katika uchumi wa nchi mbalimbali duniani ili kukabiliana na ongezeko la mfumuko wa bei hususani Marekani na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

"Benki Kuu inatarajia kuendelea kutumia akiba hiyo kuongeza ukwasi katika soko la fedha za kigeni nchini,"amebainisha Dkt.Misango.

Pia, amefafanua kuwa, kuanzia mwezi Julai hadi Agosti 21, 2023 BoT imeuza katika soko la fedha za kigeni dola milioni 100.5 ikilinganishwa na dola milioni 62 katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2022.

Katika hatua nyingine, Dkt.Misango amesema kuwa, tokea kuanza kwa vita vya Ukraine na Urusi mwezi Machi 2022, BoT imeuza katika soko la fedha za kigeni dola milioni 518.5.

Wadau
 
Akizungumza katika mkutano huo,Deogratius Marandu kutoka Duka la Kubadilishia Fedha za Kigeni la Kadoo ambalo linatoa huduma mikoa mbalimbali nchini amewataka wananchi kuondoa hofu kuhusu changamoto ya uhaba wa fedha za kigeni, kwani hapa nchini kuna uhimilivu mkubwa tofauti na maeneo mengine duniani.

"Tanzania tuna bahati kubwa, siyo nchi zote zenye bahati kama hii, kwa hiyo tunawza kusema sisi (Tanzania) tuna bahati ya kuwa na vyanzo vingi vya kuingiza fedha za kigeni ukilinganisha na nchi nyingine.

"Hiyo inamaanisha nini, hiyo inamaanisha kwanza kwamba hofu au taharuki kwamba kuna siku tunaweza tukawa hatuna fedha za kigeni, kwanza hilo halipo kabisa, na haliwezi kutokea.

"Kwa sababu ili Tanzania ikose fedha za kigeni inatakiwa tusiwe na madini kabisa, tusiwe na utalii kabisa, bandari nayo isiwepo, yaani ninaamini vitu kama hivyo, kamwe haiwezekani.

"Kwa hiyo,hofu au taharuki iliyowakumba baadhi ya wananchi kwamba fedha za kigeni zimekauka si kweli, kwa sababu zilizopo zinaendelea kutumika na zingine zinaendelea kuingia, kwa hiyo fedha za kigeni kwa Tanzania kukauka haiwezekani, wananchi na wafanyabiashara wawe na amani kabisa."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news