Dhunubu, ahitaji kutubia

NA LWAGA MWAMBANDE

REJEA Mwanzo 6:9...Nuhu alikuwa mtu wa haki, mkamilifu katika vizazi vyake; Nuhu alikwenda pamoja na Mungu”.

Aidha, kwa kuwa Nuhu alikuwa mnyenyekefu na alitenda mambo yaliyompendeza Mungu, basi akapata neema machoni pake, rejea Mwanzo 6:8.

Hivyo, Mungu akamwinua atengeneze safina ili akomboe kizazi chake; hilo lilitokea kwasababu Nuhu alikuwa mkamilifu mbele ya Mungu (alitenda mema).

Vivyo hivyo, rejea Tito 3:14...Watu wetu nao wajifunze kudumu katika matendo mema, kwa matumizi yaliyo lazima, ili wasiwe hawana matunda”.

Pia ukirejea, 1 Timotheo 6:18...“Watende mema, wawe matajiri kwa kutenda mema, wawe tayari kutoa mali zao, washirikiane na wengine kwa moyo”.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, si afya kuwa Dhunubu (wingi wa dhambi) bali ni afya kuwa mtenda mema, kwa kuwa kunakupa kibali mbele za Mungu na wanadamu. Endelea;

1.Anao wingi wa dhambi, ndiyo chetu Kiswahili,
Mtu mdhambi mdhambi, mwizi mzinzi jahili,
Kweli haitii kambi, mabaya ayajadili,
Ni mtu mwenye dhunubu, ahitaji kutubia.

2.Mfitini mchochezi, muuaji na jangili,
Mwongo mwongo na mlozi, kweli huzima kandili,
Kuishi naye ni kazi, akukatilia mbali,
Ni mtu mwenye dhunubu, ahitaji kutubia.

3.Kutenda dhambi hajali, tena anazo akili,
Na yeye kila mahali, uovu una kibali,
Kuziacha hakubali, angoja kifo kamili,
Ni mtu mwenye dhunubu, ahitaji kutubia.

4.Kwa sura kama atiki, ukimkuta mahali,
Lakini haaminiki, watu wanamjadili,
Kumzaa si riziki, wazazi tazama mbali,
Ni mtu mwenye dhunubu, ahitaji kutubia.

5.Juzi alikoswakoswa, ngemfyekelea mbali,
Wakati aliponaswa, akiufanya ucholi,
Tadhani alivyoteswa, jinai tatupa mbali,
Ni mtu mwenye dhunubu, ahitaji kutubia.

6.Njoni kwangu ninyi nyote, ambao mwatanga mbali,
Mwakumbata dhambi zote, kudhani hizo ni mali,
Yupo Muweza wa yote, tubu mpate kibali,
Ni mtu mwenye dhunubu, ahitaji kutubia.

7.Wewe mwingi wa dhunubu, usiangalie mbali,
Kuzitafuta sababu, uwe hiyohiyo hali,
Urudi kwa kujaribu, hauwezi ukafeli,
Ni mtu mwenye dhunubu, ahitaji kutubia.
(Mathayo 11:28)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news