NA MATHIAS CANAL
Jimboni Ushetu
MBUNGE wa Jimbo la Ushetu, Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga, Dkt.Emmanuel Cherehani amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi kwa wakati.
Amesema kuwa Rais Samia amekuwa kinara kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo ambapo ametaja mafanikio ya miradi mbalimbali ikiwemo kampeni ya kumtua ndoo mama kichani ambapo upatikanaji wa maji safi na salama katika jimbo la Ushetu umeongezeka.
Dkt.Cherehani ametoa pongezi hizo katika Kijiji cha Bulungwa wakati akizungumza na wananchi wakati wa mbio za mwenge wa uhuru.
Amesema kuwa kwa mafanikio ya miradi mbalimbali Rais Samia anaenda kuandika historia kubwa katika Jimbo la Ushetu na nchi kwa ujumla wake.
Amesema kuwa, Jimbo la Ushetu katika uongozi wa Rais Samia imepokea Bil 6.1 kwa ajili ya miradi sita ya maji ikiwemo mradi wa Sabasabini-Mpunze, Igwamanoni, Nyankende, na mradi wa maji wa Nyamilangano.
Ameitaja miradi mbalimbali ya maendeleo inayofanyika katika jimbo la Ushetu ambapo serikali imetoa zaidi ya shilingi milioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa kilomita moja na nusu za lami na taa za barabarani katika kijiji cha Bulungwa.
Kadhalika katika sekta ya elimu amesema kuwa Jimbo la ushetu limepokea Bil 2.89 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 108 ya sekondari ambayo wananchi hawajachangishwa kiasi chochote.
Amezitaja shule hizo ambazo ni pamoja na Eliasi Kuandikwa iliyojengwa kwa shilingi milioni 470, Shule ya Sekondari Cherehani iliyoko Ubakwe ambayo imejengwa kwa shilingi milioni 300, na zaidi ya shilingi bilioni 1.88 za mradi wa BOOST kwa ajili ya shule za msingi Nyankende na Ukune na nyumba ya mwalimu pamoja na nyumba ya mkurugenzi.