DP World ni binti mrembo wa Kiarabu mwenye fursa nyingi, hapaswi kuachwa aondoke-Askofu Ouma

NA FRESHA KINASA

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la New Life Gospel Community Church-Tanzania (Bonde la Baraka) nchini lenye makao makuu yake Kigera bondeni Manispaa ya Musoma mkoani Mara, Daniel Ouma amewaomba Watanzania kuondoa mashaka na hofu kuhusiana makuabaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu uendeshaji na uendelezaji wa bandari.
Askofu Ouma amesema, Serikali inapaswa kuongeza nguvu katika utekelezaji wa mkakati wa mawasiliano na utoaji elimu ili kuufahamisha umma kuhusu makubaliano na manufaa yake kwa nchi. 

Hayo ameyasema Agosti 6, 2023 wakati akihubiri kanisani hapo ambapo pamoja na mengine amesema itakuwa vyema Serikali kuuweka mkataba huo katika Gazeti ili watu wausome na kuufahamu kuondoa maneno ambayo wakati mwingine yamekuwa yakileta ukakasi na chuki miongoni mwa Watanzania. 

Amesema, wapo watu wamekuwa wakitoa lugha mbaya mfano 'nchi imeuzwa' na hivyo kuwapa hofu wananchi wa kawaida ambao amesema, wanahitaji kuelimishwa zaidi wajue manufaa, huku akitolea mfano kuwa DP World ni binti mrembo Mwarabu na mwenye fursa nyingi hapaswi kuachwa kutokana na uzuri na umuhimu wake katika kukuza uchumi na maendeleo nchini. 

"Kwangu mimi yapo mambo matatu ya muhimu ya kimtazamo katika suala la DP World hapa Tanzania, mtazamo wa kisiasa, kiuchumi, na mtazamo wa Wana wa Mungu,"amesema Askofu Ouma na kuongeza kuwa. 
"Kelele zinapokuwa nyingi kama zilivyo sasa nchini, huwa kwa muda mbingu zinanyamaza kimya, zinatazama na kushangaa, kwa wanasiasa wao hugawanyika. 

"Akiongea Lissu wanasema mwanasiasa, Chongolo mwanasiasa, lakini Mimi mtumishi wa Mungu naomba niseme kuwa jambo hili ni jema kwa nchi wala hakuna haja ya kupigizana kelele wakati mwingine ambazo zinaweza kutugawa,"amesema Askofu Ouma. 

"Linapokuja suala la watu wote linakuwa siyo suala la chama fulani bali la Watanzania wote, kwa ufupi Bandari ya Dar es Salaam ni lango muhimu kwa biashara nchini na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. 

"Bandari hii hutumika kama kitovu kikuu cha usafirishaji kwa nchi zisizo na bandari kama vile Zambia, Malawi, Rwanda, Burundi na Uganda ni matumaini yangu DP World itaongeza kiwango cha biashara na kuongeza tija na maendeleo ya uchumi wa Tanzania,"amesema Askofu Ouma. 

Amebainisha kuwa, ushirikishwaji wa jamii na mashaurinao yanapaswa kupewa kipaumbele ili kushughulikia masuala na malalamiko yote ambayo yanaweza kutokea wakati wa mchakato wa utekelezaji sambamba na kuzingatia uendelezaji wa muda mrefu wa mradi na atahari zake kwa vizazi vijavyo. 

Aidha, Askofu Ouma ametoa rai kwa viongozi wa dini nchini, kuwa sehemu ya utoaji wa elimu kwa wananchi na kutoogopa kulisema jambo hilo, kwani linalenga kugusa maendeleo ya watu na uchumi wa taifa la Tanzania. 

Aidha, ametoa ushauri kwa Serikali kuchanganua faida na vikwazo vinavyowezekana vya muda mrefu vya makubaliano na ni muhimu kuhusisha washika dau wote katika mchakato wa kufanya maamuzi na kuzingatia mashaka yoyote yanayoweza kutokea. 

Pia, ameshauri kuwa ni muhimu kufuatia na kutathimini athari za makubaliano kabla na baada ya muda wa shughuli kuanza, kufanya marekebisho yanayohitajika ili kudumisha ufanisi wake. 
Na wakati wa kufikiria jinsi makubaliano yanaathiri shughuli za baadaye za bandari ni muhimu kuzingatia mabadiliko yanayoweza kutokea katika teknolojia na mahitaji ya soko. 

Kuhusiana na hofu ya Watanzania, Askofu Daniel Ouma amewaomba wachumi nchini waone umuhimu wa kuweka kipaumbele kwa uwazi na ushirikiano katika mchakato mzima ili kukuza uhusiano mzuri na wenye tija kati ya bandari na wadau wake.

Pia, patekelezwe mkakati wa mawasiliano ili kuifahamisha umma kuhusu makubaliano na manufaa yake ili kuweza kusaidia kujenga ufahamu na uaminifu katika shughuli za bandari. 

"Mimi naona kuna umuhimu mkubwa kuwa na mipango ya dharura iwapo kutatokea mabadiliko yoyote yasiyotarajiwa ambayo yanaweza kuathiri utekelezaji wa makubaliano na kutuacha kitanzi mikononi mwa wageni hao. 

"Mama Samia ruhusu tujadili mabadiliko yoyote yanayoweza kutokea ambayo yanaweza kuhitajika kufanywa kwa makubaliano katika siku zijazo,"amesema Askofu Ouma. 

Jackson Genya na Jumapili Misana ni viongozi wa kanisa hilo wamesema kuwa, Serikali haiwezi kuwa na nia mbaya na wananchi wake, hivyo Watanzania watambue kwamba Serikali inadhamira njema ikiwemo kuwaletea maendeleo wananchi wake. 
Katika ibada hiyo, Askofu Ouma ameongoza maombi maalumu kwa ajili ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Dkt.Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya, wabunge na Watanzania wote wadumishe upendo na umoja wa kitaifa kwani nchi inahitaji amani kupiga hatua mbele zaidi kimaendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news