NA MATHIAS CANAL
MBUNGE wa Jimbo la Ushetu lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, Dkt Emmanuel Cherehani amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi kwa wakati.
Amesema kuwa, Rais Dkt.Samia amekuwa kinara kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo ambapo ametaja mafanikio ya miradi mbalimbali ikiwemo kampeni ya kumtua ndoo mama kichwani ambapo upatikanaji wa maji safi na salama katika Jimbo la Ushetu umeongezeka.
Dkt.Cherehani ametoa pongezi hizo katika Kijiji cha Ulewe wakati akizungumza na wananchi kueleza utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Amesema kuwa, kwa mafanikio ya miradi mbalimbali Rais Samia anaenda kuandika historia kubwa katika Jimbo la Ushetu na nchi kwa ujumla wake.
Amesema kuwa, Jimbo la Ushetu katika uongozi wa Rais Samia imepokea shilingi bilioni 6.1 kwa ajili ya miradi sita ya maji ikiwemo mradi wa Sabasabini-Mpunze, Igwamanoni, Nyankende, na mradi wa maji wa Nyamilangano.
Kadhalika katika sekta ya elimu amesema kuwa, Jimbo la ushetu limepokea shilingi 2.89 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 108 ya sekondari ambayo wananchi hawajachangishwa kiasi chochote.
Amezitaja shule hizo ambazo ni pamoja na Eliasi Kuandikwa iliyojengwa kwa shilingi 470, Shule ya Sekondari Cherehani iliyoko Ubagwe ambayo imejengwa kwa shilingi 300, na zaidi ya shilingi bilioni 1.88 za mradi wa BOOST kwa ajili ya shule za msingi Nyankende na Ukune na nyumba ya mwalimu pamoja na nyumba ya mkurugenzi.
Kuhusu miundombinu ya barabara Mbunge Cherehani amesema kuwa, serikali inayoongozwa na Rais Samia imeendelea kuimarisha miundombinu ambapo katika kipindi cha muda mfupi barabara nyingi zinapitika ipasavyo.