Hatua za BoT zaongeza nguvu upatikanaji wa fedha za kigeni

NA GODFREY NNKO

SERIKALI pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaendelea kutekeleza hatua mbalimbali kukabiliana na upungufu wa fedha za kigeni nchini.
Hayo yamebainishwa Agosti 22, 2023 na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tafiti za Uchumi BoT, Dkt.Suleiman Misango wakati akitoa wasilisho lake kuhusu masuala ya fedha za kigeni kwenye kikao na wahariri, waandishi wa habari na wadau wa sekta ya fedha nchini.

Dkt.Misango kupitia kikao hicho ambacho kilifanyika makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam alikuwa anayabainisha hayo kwa niaba ya Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba.

Amesema, miongoni mwa hatua hizo ni kuongeza kiwango cha kuuza fedha za kigeni katika soko la fedha za kigeni, kuongeza vyanzo vya upatikanaji wa fedha za kigeni ikiwemo ununuzi wa dhahabu.

"Serikali na Benki Kuu ya Tanzania zimeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kukabiliana na changamoto za upungufu wa fedha za kigeni katika soko la fedha za kigeni.

"Hatua hizo ni pamoja na Benki Kuu kuongeza kiwango cha kuuza fedha za kigeni katika soko la fedha za kigeni, kuongeza vyanzo vya upatikanaji wa fedha za kigeni ikiwemo ununuzi wa dhahabu,"amebainisha Dkt.Misango.

Dkt.Misango amefafanua kuwa, hatua nyingine ni kuongeza mauzo nchi za nje na kuzalisha bidhaa mbadala wa zile zinazoagizwa nje ya nchi.

"Aidha, Benki Kuu inaendelea kushirikisha mabenki, maduka ya kubadilisha fedha za kigeni, pamoja na wadau wengine katika kusimamia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya fedha za kigeni nchini."

Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tafiti za Uchumi BoT, Dkt.Misango amefafanua kuwa, hatua hizo zimeanza kuleta mafanikio ikiwemo kupunguza kasi ya mabadiliko katika thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani katika soko la rejareja.

Amesema, pia kiasi cha LCs ambacho kilikuwa hakijalipwa na kubadilishwa kuwa mikopo (post-import loans) kimeendelea kupungua.

Uagizaji mafuta

Mbali na hayo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pamoja na kuelezea kuhusiana na mikakati mbalimbali inayoendelea ya kukabiliana na upungufu wa fedha za kigeni unaoikabili dunia imeeleza kuwa, imekuwa ikishirikiana na benki mbalimbali nchini kushughulikia changamoto ya upatikanaji wa mafuta kutokana na uhaba wa dola.

Meneja Masoko ya Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),Lameck Kakulu amesema kuwa,"Benki Kuu imekuwa ikishirikiana kwa karibu sana na Taomac (Jmuiya ya Waagizaji na Wasambazaji Mafuta Tanzania) tumekuwa pamoja sana kwenye suala hili,kilichotokea ni kwamba crisis imekuwa prolonged, tunakabiliana na suala hili.

"Moja wapo ni ya kuongeza supply, kwa maana kwamba supply ndiyo issue kubwa wakati uchumi wa Dunia ukiimarika na Tanzania kwa ujumla focus tuliyoiweka ni kuongeza mzigo. Kwa maana kwamba sapoti, hasa ku-focus kutoa hizo PIL (Post-Import Loans) na kushughulikia mengineyo,"amefafanua Meneja huyo.

Naye Mkuu wa Mauzo Idara ya Hazina Benki ya NMB, Jeremiah Lyimo amesema kuwa, "Si mafuta tu,wameanza labda na waagiza wa mafuta, na sisi mabenki (benki mbalimbali) tutawasaidia kwenye hizo sekta zingine.

"Si mmoja tu, wateja wengi kwenye sekta ya mafuta hawana Backlog ya zile PIL ya zile LCs, ambazo alikuwa anatakiwa alipe,lakini alichelewa kulipa ameshamaliza zote na bado tunashughulika na mengineyo.Hii yote ni mwingiliano ambao Benki Kuu wameweza kutusaidia."

Kuhusu ya madai ya baadhi ya wananchi katika taasisi za fedha kuwekewa ukomo wa kiasi cha kubadilishia fedha za kigeni, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema, hakuna ukomo.

Akizungumzia kuhusiana na madai hayo, Mhazini wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),Sadati Mussa amebainisha kuwa, hawana mgawo.

"Hatuna mgawo, labda tu kama umeenda kwenye duka la kubadilishia fedha za kigeni au benki, inategemea tu na siku hiyo wana kiasi gani cha akiba ya fedha za kigeni.

"Lakini, kimsingi hakuna mgawo na kama alivyosema Mwenyekiti (Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tafiti za Uchumi Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt.Suleiman Misango) tumeona sasa hivi hali imeendelea kuimarika.

"Na benki tunapata takwimu za kila siku kuhusiana na ununuzi na uuzaji wa fedha za kigeni kwenye soko letu la rejareja, kwa hiyo tunaamini kabisa tunavyozidi kwenda mbele hali itazidi kuimarika.

"Pengine ile hali ambayo inaonekana kuwa ni mgawo itaendelea kuondoka, lakini kwa sasa hivi hatuna kiasi ambacho kimewekwa rasmi kisheria,"amefafanua Mhazini wa BoT,Saddati Mussa. 

Uchumi kuimarika

Vile vile,Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tafiti za Uchumi BoT, Dkt.Suleiman Misango ameeleza kuwa, uchumi wa Dunia umeanza kuimarika baada ya kupitia changamoto mbalimbali, na hivyo kuashiria kuanza kuwepo kwa ongezeko la fedha za kigeni nchini.

Dkt.Misango amesema, ukuaji wa uchumi wa dunia unatarajiwa kufikia asilimia 3 mwaka 2023 tofauti na matarajio ya awali ya ukuaji wa asilimia 2.8.

Pia, amesema bei za bidhaa katika soko la Dunia zimeendelea kupungua, na mfumuko wa bei umeendelea kupungua katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.

Ameeleza pia kwamba, benki kuu za nchi mbalimbali duniani, ikiwemo Marekani zimeanza kupunguza kasi ya kuongeza riba katika kukabiliana na mfumuko wa bei.

“Mwenendo huu wa kuridhisha katika uchumi wa dunia, unaashiria kupungua kwa changamoto ya upungufu wa dola ya Marekani nchini."

Amesema, pamoja na maendeleo hayo duniani, uchumi wa Tanzania unaendelea kuimarika na kuna viashiria vya kupungua kwa changamoto za upungufu wa fedha za kigeni nchini, hivyo wananchi na wafanyabiashara hawapaswi kuwa na hofu ya upatikanaji wa fedha za kigeni.

Akiba

Mbali na hayo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imebainisha kuwa, hadi kufikia Agosti 21, 2023 ilikuwa na akiba ya fedha za kigeni dola bilioni 5.44 ambazo zinatosheleza miezi 4.9 kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi.

Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tafiti za Uchumi BoT, Dkt.Suleiman Misango amesema,"Pamoja na kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa fedha za kigeni nchini hususani dola ya Marekani, hali ya upatikanaji wa fedha za kigeni imeendelea kuwa himilivu.
"Uhimilivu huo unatokana na kuendelea kuwepo kwa akiba ya kutosha ya fedha za kigeni nchini, hadi kufikia Agosti 21, 2023 akiba hiyo ilikuwa dola za Marekani milioni 5,441 (zaidi ya dola bilioni 5.44), ambayo inatosheleza miezi 4.9 mimi ninaweza kusema miezi mitano ya uagizaji wa huduma na bidhaa kutoka nje."

Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa, kiasi hicho kinalingana na kipindi kabla ya changamoto za uchumi wa Dunia zilizopelekea kuwepo upungufu wa fedha za kigeni.

Aidha, miongoni mwa changangamoto hizo ni pamoja na vita kati ya Urusi na Ukraine, UVIKO-19,utekelezaji wa Sera ya Fedha ya kupunguza ukwasi katika uchumi wa nchi mbalimbali duniani ili kukabiliana na ongezeko la mfumuko wa bei hususani Marekani na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

"Benki Kuu inatarajia kuendelea kutumia akiba hiyo kuongeza ukwasi katika soko la fedha za kigeni nchini,"amebainisha Dkt.Misango.

Pia, amefafanua kuwa, kuanzia mwezi Julai hadi Agosti 21, 2023 BoT imeuza katika soko la fedha za kigeni dola milioni 100.5 ikilinganishwa na dola milioni 62 katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2022.

Katika hatua nyingine, Dkt.Misango amesema kuwa, tokea kuanza kwa vita vya Ukraine na Urusi mwezi Machi 2022, BoT imeuza katika soko la fedha za kigeni dola milioni 518.5.

Matumizi ya shilingi

Pia, wafanyabiashara na wananchi wametakiwa kuzingatia sheria, miongozo na kanuni za fedha za kigeni kama zilivyoanishwa katika tamko kuhusu matumizi ya fedha za kigeni kulipia huduma na bidhaa nchini.

Aidha,wanapaswa kutambua kuwa,fedha zitokanazo na mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi kuwekwa katika benki mbalimbali hapa nchini.

Juni 20,2023 BoT iliukumbusha umma kwamba Serikali ilishatoa tamko kuhusu katazo la matumizi ya fedha za kigeni kwa wakaazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kulipia bidhaa na huduma nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),Emmanuel Tutuba ilifafanua kuwa, tamko la kwanza lilitolewa mwezi Agosti 2007 na la pili mwezi Desemba 2017.

"Hata hivyo, katika siku za karibuni imebainika kuwepo kwa ukiukwaji wa tamko hilo. Hivyo, Benki Kuu inapenda kuukumbusha umma kwamba maagizo yaliyotolewa hapo awali kuhusu matumizi ya fedha za kigeni yanapaswa kuendelea kuzingatiwa kama ifuatavyo:

i. Bei zote hapa nchini zitangazwe kwa shilingi ya Tanzania. Bei hizi zinajumuisha kodi za kupangisha ardhi, nyumba na ofisi; gharama za elimu; huduma za afya,vifaa tiba na vitendanishi; gharama za usafiri, lojistiki na bandari; vifaa vya kielektroniki na huduma za mitandao ya mawasiliano, n.k.

ii. Bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja wasio wakaazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni.

"Bei hizi zinajumuisha gharama za hoteli, usafiri, gharama za viwanja vya ndege na viza kwa wageni, usafirishaji kwenda nchi za nje kupitia Tanzania na gharama za mizigo bandarini. Walipaji wanaotumia fedha za kigeni watambuliwe kwa vitambulisho vyao kama pasi za kusafiria na nyaraka za usajili kwa makampuni.

iii. Viwango vya kubadilisha fedha vitakavyotumika katika kuweka bei hizo viwekwe wazi na visizidi vile vya soko. Ifahamike wazi kuwa ni benki na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni pekee yanayoruhusiwa kupanga viwango vya kubadilisha fedha kutokana na ushindani katika soko la fedha za kigeni.

iv. Mkaazi yeyote wa Tanzania anapaswa kufanya malipo kwa kutumia shilingi ya Tanzania pekee na hivyo asilazimishwe kulipia bidhaa au huduma yoyote hapa nchini kwa kutumia fedha za kigeni.

"Benki Kuu inapenda pia kuukumbusha umma kuwa kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006 kinaelekeza kuwa shilingi ya Tanzania ndiyo fedha pekee ambayo inaruhusiwa kutumika nchini, hivyo hakuna mtu au kampuni yoyote inayoruhusiwa kuikataa kwa malipo yoyote halali (legal tender). 

"Kitendo cha kukataa malipo kwa shilingi ya Tanzania ni kuvunja Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006,"amefafanua Gavana Tutuba kupitia taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news