NA GODFREY NNKO
LICHA ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kupitia milima na mabonde ndani ya miaka zaidi ya 50 tangu kuanzishwa kwake, ubunifu mpya umeonesha kurejesha hadhi ya shirika hilo la umma ambalo limeaminiwa na Serikali katika kuwezesha mabadiliko ya sekta ya madini nchini.
STAMICO ambalo ni shirika la Watanzania linalomilikiwa na Serikali lipo chini ya Wizara ya Madini, lilianzishwa kwa Sheria ya Mashirika ya Umma sura 257 kupitia Agizo la Uanzishwaji wa Shirika la Madini la Taifa Na.163 la mwaka 1972 lililofanyiwa marekebisho mwaka 2014.
Aidha, STAMICO ilianzishwa upya mwaka 2015 kupitia Agizo la Marekebisho ya Mashirika ya Umma (Uanzishwaji) (Marekebisho), 2015 kwa lengo la kuongeza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa Taifa na kutengeneza fursa za ajira kwa Watanzania.
Agosti 28, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, katika mwendelezo wake wa kuzikutanisha taasisi na mashirika ya umma kwa pamoja na wahariri wa vyombo vya habari nchini, Ofisi ya Msajili wa Hazina chini ya Nehemiah Kyando Msechu iliwakutanisha na STAMICO kuelezea walipotoka, walipo na wanakoelekea.
Kwa nini OMH?
Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) ilianzishwa kama Shirika Hodhi chini ya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 418 ya Mwaka 1959 na Sheria ya Msajili wa Hazina (Mamlaka na Majukumu) Sura 370 ya Mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa.
Lengo kuu la kuanzishwa kwa OMH ni kusimamia uwekezaji wa Serikali pamoja na mali zingine za Serikali katika taasisi, mashirika ya umma na makampuni ambayo Serikali ina umiliki wa hisa au kuna maslahi ya umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.
Mwaka 2010, Sheria ya Msajili wa Hazina ilirekebishwa ambapo, pamoja na mambo mengine, iliifanya OMH kuwa huru na kujitegemea kimuundo.
Aidha, mwaka 2014 kufuatia kufutwa kwa lililokuwa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC), OMH ilirithi majukumu ya iliyokuwa shirika hilo.
Kufuatia mabadiliko hayo, OMH ikawa na jukumu la kusimamia ubinafsishaji wa mali za umma, usimamizi na ufuatiliaji, ukusanyaji wa madeni ya Serikali yaliyorithiwa kutoka CHC, na urekebishaji na ufilisi wa mali zisizozalisha faida katika makampuni au mashirika yaliyobinafsishwa.
Hivyo, STAMICO ni miongoni mwa mashirika ya umma ambayo yanasimamiwa na OMH ambapo mwelekeo mpya wa Msajili wa Hazina wakati wa kuelekea kwenye maboresho makubwa, anataka wamiliki wa mashirika na taasisi hizo ambao ni Watanzania wazifahamu kwa kina kupitia vyombo vya habari.
STAMICO wanasemaje?
Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, CPA Dkt.Venance Mwasse anawaeleza wahariri hao kuwa, STAMICO ilianzishwa mwaka 1972 kwa lengo la kuwekeza kimkakati katika miradi ya madini na uvunaji wa rasilimali madini kwa niaba ya umma kwenye mnyororo wote mwanzo hadi mwisho (unique-setup).
CPA Dkt.Mwasse anafafanua kuwa, majukumu makuu ya shirika hilo ni kuwekeza kwenye miradi ya kimkakati ya utafutaji na uchimbaji madini,uchenjuaji, uongezaji thamani na uuzaji madini.
Pia, kutoa huduma za kibiashara za uchorongaji na ushauri,kutoa huduma za ushauri wa kitaalam na kiufundi katika sekta na kuratibu uendelezaji wa wachimbaji wadogo nchini.
Mwezi Machi, 2015, CPA Dkt.Mwasse anafafanua kuwa, Hati ya Uanzishwaji wa Shirika ilifanyiwa marekebisho kadhaa yaliyohusisha kimuundo ambapo nafasi ya Meneja Mkuu kuwa Mkurugenzi Mtendaji.Sambamba na kimajukumu ambapo yalihusisha kuendeleza Sekta ya Uchimbaji mdogo nchini (Unique setup).
Aidha, anasema, mwaka 2019 Serikali ilifanya marekebisho mengine ambayo yalihusisha mabadiliko ya kiuongozi na kimuundo, kuandaa na utekelezaji wa turn around strategy.
"Mtaona huko nyuma shirika liliyumbayumba sana. Kuna watu walitaka kukata tamaa, lakini Serikali kwa hekima yake ikalirudisha na mwaka 2015 likabadilishwa muundo nafasi ya mkuu wa shirika ikabadilishwa ikawa Mkurugenzi Mtendaji, lakini ikaongezewa jukumu la kuwalea na kuwaendeleza wachimbaji wadogo.
"Na mwaka 2019 shirika likayumba tena, likataka kurudi kwenye wimbi la kufutwa na Serikali ikachukua hatua Wizara ya Madini pamoja na Msajili wa Hazina (TR) wakafanya mabadiliko, na leo tunalitolea matokeo yake.
"Shirika kwa ufupi linafanya majukumu yake kupitia njia kuu tatu, kwanza ni miradi yetu wenyewe ambayo ni ya asilimia 100, lakini pia miradi ya ubia na kimkakati.
"Kuna baadhi ya leseni na sisi tumekuwa kama ngazi au daraja la kupitia kwa wewekezaji na leseni ambazo tunakuwa nazo tunazi-protect wanaleta mitaji pamoja na teknolojia."
Katika kipindi cha miaka mitatu, CPA Dkt.Mwasse anasema, shirika limefanya mageuzi makubwa na kufanya kuwa chombo madhubuti katika sekta ya madini.
Mapato
CPA Dkt.Mwasse amesema, mageuzi hayo makubwa yameliwezesha shirika hilo kuongeza mapato kutoka shilingi bilioni 1.3 mwaka 2018/19 hadi shilingi bilioni 61.1 kwa mwaka 2022/23 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 4425.
Mafanikio hayo, amebainisha kuwa, yameliwezesha shirika hilo kupata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo kutokana na ukaguzi wa mahesabu.
Pia amesema, mafanikio hayo yameliwezesha shirika sasa kuanza kutoa gawio serikalini, kwani tangu lianzishwe mwaka 1972 lilikuwa halijawahi kupeleka kitu chochote serikalini.
Mkurugenzi Mtendaji huyo amefafanua sababu zilizowawezesha kufikia mafanikio hayo kuwa, ni kwa kubadili fikra,ushirikishwaji, nidhamu, kujiwekea malengo na kuyatekeleza.
“Kwa ujumla, tulifikia mahali ikabidi tubadilike kifikira, kuna mashirika ya umma yanayotoa huduma na kuna mashirika ya umma yanayotakiwa yajiendesha kibiashara.
“Kwa hiyo tulipoamua kujiendesha kibiashara, tukaamua sasa kwenda kuzitafuta fursa, tulipobonyeza hiyo button tukaona mambo yamekwenda. Viongozi kwa kulitambua hili ni shirika la umma nikaona lazima tuumize vichwa.
"Pamoja na kuongeza morali ya wafanyakazi kwa kuona wanajaliwa na mipango iwe inanyooka, " amesema na kuongeza STAMICO litaendelea kusimamia shughuli zake kikamilifu ili kuongeza tija katika shughuli zinazotokana na madini.
CPA Dkt. Mwasse amesema, STAMICO limetoka kuwa shirika linalotengeneza hasara hadi kutengeneza faida na wamelipa gawio kwa Serikali jumla ya shilingi bilioni 8, hivyo wameondoa utegemezi wa ruzuku kutoka serikalini.
Benki ya Wachimbaji
Katika hatua nyingine, CPA Dkt.Mwasse amebainisha kuwa,STAMICO kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) pamoja na wadau wengine wako mbioni kukamilisha mchakato wa uanzishwaji wa Benki ya Wachimbaji Wadogo.
Lengo anasema ni kuhakikisha, benki hiyo inasaidia kundi hilo kupata mitaji kupitia mikopo na hatimaye kujikwamua kiuchumi pamoja na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini katika pato la taifa.
CPA Dkt.Mwasse amesema kuwa, wazo hilo liliasisiwa kwenye Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) uliofanyika jijini Mwanza mwezi Mei 2023, na baadaye kuundiwa kamati kwa ajili ya kushughulikia mchakato huo jijini Arusha.
Amesema kuwa,uanzishwaji wa benki hiyo umelenga kutatua changamoto ya ukosefu wa mitaji inayowakabili wachimbaji wadogo nchini, jambo linalowasabisha washindwe kufanya uchimbaji wenye tija na kufikia malengo yao.
“Tuliingia makubaliano ya mashirikiano na taasisi nyingine za fedha kwa ajili ya kukopesha wachimbaji wadogo, lakini niseme kuwa uzoefu unaonyesha kuwa sekta hii ya madini ina sifa zake ambazo taasisi zingine zinashindwa kukubaliana na taratibu na hizi benki za kawaida,”amesema CPA Dkt.Mwasse.
Kwa nini wachimbaji wadogo?
Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, CPA Dkt.Mwasse anafafanua kuwa, "Wote mnafahamu wachimbaji wadogo ni wale ambao wanapewa primary mining license na zile leseni wanapewa wazawa.
"Lakini kutokana na ukubwa wa sekta kukawepo na hekima kwamba chombo hiki cha Serikali kiwasaidie wachimbaji hawa nao waweze kuvuna rasilimali hizi.
"Lengo ni kusitawisha maisha yao na maendeleo kwa ujumla, Afrika mashirika ya madini yako mengi, lakini shirika letu set-up yake lenyewe limepewa jukumu la kuwekeza kwenye mnyororo mzima wa sekta ya madini na kwenye madini aina zote."
CPA Dkt.Mwasse ameeleza kuwa, STAMICO imeweka lengo la kuwaendeleza wachimbaji hao wadogo kwa kuwarasimisha kabisa ili wafanye shughuli zao bila usumbufu kwa kuwa wengi wao wanachimba madini ili wajipatie kipato cha kuendeleza familia zao.
Amesema, katika kuhakikisha wanafikia lengo hilo, shirika litaendelea kuwapa mafunzo ambako tayari wanazunguka nchi nzima kuwafikia, kuendelea kuwajengea uwezo kwa upande wa teknolojia mpya kwa kuwaletea vifaa vya kisasa zaidi sambamba na kuanzisha benki hiyo.
"Tulifanya utafiti kwa wachimbaji wadogo na kubaini wana changamoto mbalimbali zikiwemo, elimu ya uchimbaji, ukosefu wa taarifa sahihi za mapato.
"Teknolojia duni, kutokuwa na mitaji au kutokukopesheka, na ukosefu wa masoko ya bidhaa zao, hivyo basi shirika limeanzisha vituo vya mfano vya kujifunzia teknolojia vyenye tija ya uchimbaji katika maeneo ya Lwamgasa, Katente na Itumbi.
"Pia tumeongeza uwezo wa kutoa huduma katika vituo hivyo na kutekeleza makubaliano (MOU) na taasisi za kifedha CRDB, NMB, AZANIA na KCB ili ziweze kuwakopesha mitaji wachimbaji wadogo na kuwawezesha safari za kujifunza ndani na nje ya nchi,"amefafanua CPA Dkt.Mwasse.
Wakati huo huo, CPA Dkt.Mwasse amebainisha kuwa, STAMICO kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) wameingia makubaliano ya awali na Kampuni za GF Truck na Apolo ili kuwawezesha kupata vifaa kutoka kwa kampuni wauzaji wa mitambo ya uchimbaji madini.
"Tunalo jukumu la kuendeleza wachimbaji wadogo, ni jukumu muhimu sana, katika kuona mchimbaji mdogo anachimba hizo rasilimali kwa tija.
"Ili aweze kuyafanya hayo anachotaji aweze kusaidiwa, kuendelezwa lakini tuliona mchimbaji mdogo anakabiliwa na changamoto zipi?.
"Tukakuta kwenye maeneo matano ikiwemo elimu ya uchimbaji na ukosefu wa taarifa sahihi za mashapo, pia anatumia teknolojia duni na hana mtaji.
"Sasa kupitia changamoto hizo tukatengeneza mkakati kuhusiana na suala la elimu na ulizinduliwa tarehe 30 wakati wa mkutano wetu tuliofanya na wadau wa madini na ulizinduliwa na Mheshimiwa Waziri mwenyewe."
"Lakini kwenye suala la mashapo tumeshawasiliana na Taasisi ya Jiolojoa Tanzania wao ndio wanataarifa kwa vile sisi ndio wenye jukumu la kumsaidia mchimbaji mdogo tumeshawasiliana nao kuweza kuwasaidia wachimbaji wadogo."
"Lakini vile vile tukaona tutafute suluhisho la kudumu la kumsaidia mchimbaji mdogo ni kumpatia mashine za kuchoronga, kwa hiyo tayari tumeshaagiza mashine tano za kuchoronga na zitafika mwishoni mwa mwezi huu na tuliziagiza tukishirikiana na wachimbaji wadogo ambao ndio watumiaji."
Mikakati yao
"Mkakati ni kwamba ifikapo mwakani mwezi Machi tuwe tumeagiza mashine 15 na hizi tutaziweka kwenye kila zone ili mchimbaji mdogo azifikie kwa urahisi hatutailipia hiyo huduma tutawapa hiyo huduma walipie zile gharama ambazo zitawezesha kufanya kazi ya utafiti.
"Mtaona hayo ni mageuzi katika tasnia ya uchimbaji wa madini ili aone ni wapi achimbe badala ya kuchimba kwa kubahatisha na hivyo kupoteza mtaji, kupoteza muda na kupoteza fedha, lakini jambo hili litakuja kumsaidia kuchoronga ajue hapa kuna hiki na hapa kuna hiki ajue."
"Tunataka mchimbaji apate tija na awe na usalama pia kupitia teknolojia, anaweza kuanzisha kiwanda kupitia shamba darasa ambalo linatoa mafunzo."
"Suala la mitaji tuna makubaliano na taasisi nyingi za fedha katika kumsaidia tuliona tuingie makubaliano na taasisi za fedha kuweza kumsemea, kwa hiyo benki tumeshaingia nazo makubaliano na tayari wameshaanza kuwaamini kuwakopesha wachimbaji wadogo.
"Suala la masoko tunafanya mpango kuwakutanisha wachimbaji wa madini mbalimbali pamoja na watumiaji wa madini hayo, mwezi wa nne tulifanya mkutano huo walikutana na tayari mambo yanaendelea vizuri na wenye viwanda pia walikuwepo kuona namna gani ya kununua madini hayo."
"Kwa hiyo mchango wa sekta, Shirika la Madini la Taifa latika kuwasaidia wachimbaji ni mkubwa sana na tunaendelea kufanya hivyo kuweza kuwainua wachimbaji wetu."
Miradi mbalimbali
CPA Dkt.Mwasse amebainisha kuwa, kwa sasa STAMICO inasimamia miradi mbalimbali ikiwemo, Mradi wa Kiwira wa uchimbaji, uchakataji na uuzaji wa makaa ya mawe mkoani Songwe.
"Na miradi yetu kuna Kiwira, ni mradi ambao ulisimama kwa muda mrefu tangu urudishwe serikalini, lakini kupitia mkakati niliousema ndio tumebadilisha sasa hivi.
Amefafanua kuwa, uchimbaji, uchakataji na uuzaji wa makaa ya mawe kwa wingi (massive coal mining) unaendelea Kiwira mkoani Songwe.
"Mgodi umekamilisha ukarabati wa miundombinu ikihusisha underground mine,barabara pamoja na daraja hivyo kuutoa mradi kwenye cost center kuwa revenue center.
"Mradi wa makaa ya mawe uko busy, ajira zipo, mapato yapo mwanzo mradi huu ulikuwa unachukua hela serikalini. Vile vile, kwenye mkakati huu wa kuendeleza huu mradi tumeweza kupata eneo la namna ya ku-exploit haya makaa ya mawe tunafanya maandalizi.
Aidha ameeleza kuwa,miradi mingine inayosimamiwa na shirika hilo ni pamoja na Mradi wa Mkaa Mbadala wa kupikia kwa kutumia makaa ya mawe.
"Tunao mradi wa makaa na huu ni ubunifu mwingine wa Shirika la Madini la Taifa tulifanya utafiti tangu mwaka 2018 kuona nmna gani yake mabaki yanayotokana na mchakato wa makaa.
"Badala ya kuwa uchafu tukafanya utafiti kwa kushirikisha COSTEC, TIRDO na vyuo vikuu, nataka kuwaambia kwamba utafiti umekamilika.
"Mpaka sasa hivi tumeshapata cheti toka TBS na mradi huu ulizinduliwa mwaka jana wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya shirika na alizindua Makamu wa Rais mwenyewe."
Katika kuongeza ufanisi kupitia mradi huo wa kuzalisha mkaa (nishati) ya kupikia ya makaa ya mawe yaliyopo Kiwira-Kabulo tayari mitambo mikubwa miwili yenye uwezo wa kuzalisha tani 20 kwa saa imeshawasili na inaendelea kusimikwa mikoa ya Pwani na Songwe. Huku mingine ikitarajiwa kuwasili mwaka huu wa fedha.
Dhahabu
Mradi wa Dhahabu STAMIGOLD unaomilikiwa na STAMIGOLD kwa hisa asilimia 99 na Msajili wa Hazina hisa asilimia moja.
Anabainisha kuwa, STAMIGOLD kwa sasa una jumla ya watumishi wazawa 544 na umeunganishwa na Gridi ya Umeme, hivyo kuachana na matumizi ya dizeli.
Kuhusu Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu Mwanza ambachp kinamilikiwa na shirika kwa asimia 25 na Mbia asilimia 75, CPA Dkt.Mwasse anafafanua kuwa,eneo la kiwanda ni la shirika na ujenzi umekamilika huku ukihusisha kiwanda,benki mbalimbali,Soko la Madini na ofisi za taasisi.
Amesema, usafishaji wa dhahabu ni kwa kiwango cha Kimataifa cha 999.9 purity na kiwanda hicho kina Ithibati ya Kimataifa (ISO).
"Tuna kiwanda cha kusafisha dhahabu cha mkoani Mwanza wengi mnakifahamu na mlishiriki mwaka 2021 wote mnakumbuka Sheria ya Madini imebadilika mwaka 2017.
"Katika kuunga mkono mapato hayo ya Serikali, Shirika la Madini la Taifa likapata wawekezaji, likaingia nao ubia ni kiwanda cha kisasa chenye uwezo mkubwa.
"Kiwanda hiki kinafaida kubwa sana, sote tunatambua kuna ajira pia teknolojia, lakini pia ni kiwanda ambacho kimekuja kutoa soko la uhakika.
"Hapa kuna wachimbaji wote wakubwa na wa kati na wadogo, kwa hiyo kiwanda hiki kinanunua dhahabu, mchimbaji na uhakika wa soko.
"Uanzishwaji wa kiwanda hicho umesaidia, kusafisha dhahabu na mazao ambatano, uhaulishaji wa teknolojia, kuongeza huduma kwa Jamii (CSR), mapato kwa Serikali, STAMICO, na Serikali za mitaa, kuongeza ajira, kupunguza utoroshaji wa dhahabu,kutambulika Kimataifa na kuimarisha shilingi ya Tanzania na uchumi,"amefafanua CPA Dkt.Mwasse.
Bucreef
Katika Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef, CPA Dkt.Mwasse amebainisha kuwa, shirika hilo lina hisa asilimia 45 na
TANZAM2000 ina hisa ya asilimia 55.
Amesema, mradi huo unaendeshwa chini ya Kampuni ya ubia ya Buckreef Gold Company (BGC) ambapo uzalishaji kupitia mtambo wa kuzalisha tani 45 kwa saa unaendelea.
"Mgodi kwa sasa umeanza kuongeza ukubwa wa mtambo wake uwe na uwezo wa kuzalisha tani 90 kwa saa,"amesisitiza CPA Dkt.Mwasse.
Mkurugenzi Mtendaji huyo pia amebainisha kuwa, kwa sasa shirika hilo limeongeza thamani yake na kuwezesha taasisi mbalimbali zilizo chini yake kuendelea kufanya vyema kutokana na usimamizi mzuri wa sera na miongozo mbalimbali ya serikali kuhusiana na sekta ya madini.
Tuzo
Mbali na mafanikio hayo, CPA Dkt.Mwasse anabainisha kuwa,shirika hilo pia limepata tuzo mbalimbali zikiwemo tano kwa mwaka 2023.
Tuzo ambazo ni pamoja na ya taasisi ya umma iliyofanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji na yenye tija kwa mwaka 2023,shirika la umma ambalo limetoa gawio kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali,
Mshindi wa Tuzo ya Kampuni ya Madini Bora ya Mwaka 2023 (ACOYA), Tuzo ya Uwezeshaji Wachimbaji Wadogo pamoja na Tuzo ya Mdhamini wa Maonesho.
Mbali na hayo, STAMICO imejipanga kuhakikisha kuwa ifikapo 2024/2025, inaongeza gawio lake serikalini, kuzalisha kwa wingi mkaa mbadala wa Rafiki briquettes unaotokana na Makaa ya Mawe.
Pia, kuimarisha uchimbaji mkubwa wa makaa ya mawe, kuongeza uwekezaji wake kwenye tasnia ya uchorongaji, kuendeleza leseni za shirika na kuzitangaza kwa lengo la kupata wawekezaji wa madini ya kimkakati ya Lithium, Graphite, REE na Copper.
Wakati huo huo, Dkt.Mwasse amebainisha kuwa, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limezidi kufanya vizuri katika shughuli za uchorongaji madini nchini.
Amesema, ufanisi wao ndiyo umewawezesha kusaini mkataba mnono wa kuchoronga na mgodi mkubwa na Geita Gold Mine (GGML) uliopo mkoasni Geita.
Mkataba huo ambao una thamani ya bilioni 55.2 na ulitiwa saini Machi 27,2023. Dkt.Mwasse amesema, mkataba huo ni uthibitisho kuwa watanzania wanaweza kushiriki kikamilifu katika kandarasi zinatokea katika mnyororo wa thamani wa madini nchini.
CPA Dkt.Mwasse anasema, pia wataendelea kutekeleza mpango wa mafunzo (training calendar) kwa ajili ya kuelimisha wachimbaji mikoa yote nchini.
TEF
Aidha, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile mbali na kulipongeza shirika hilo kwa uzalishaji mageuzi makubwa ndani ya muda mfupi, pia ameshauri shirika kuweka mipango Mikakati na kipaumbele kwenye maslahi ya wafanyakazi kwa kuwaongezea mishahara pale shirika linapokua ili kuwapa ari mpya ya utendaji.
Pia, Balile ameshauri Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kupeleka ujuzi wake katika mashirika mengine ya serikali kutokana na mafanikio yake makubwa.