Imani na amani vinakwenda sambamba-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameendelea kuihimiza jamii juu ya umuhimu wa kudumisha amani.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akishiriki katika kuitikia dua ikisomwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kabi (kulia kwa Rais) baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid Mabuluu Mfereji wa Wima Ng’ambo Station Wilaya ya Mjini Unguja na kushoto kwa Rais ni Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Othman Ame Chum.(Picha na Ikulu).

Sambamba na kubeba imani ya dhati ndani ya mioyo yao kwa mustakbali wa taifa na ustawi wa jamii bora kwa maendeleo ya uchumi endelevu nchini.

Alhaj Dkt. Mwinyi ametoa nasaha hizo Agosti 4, 2023 kwenye Msikiti Mabuluu Mfereji wa Wima, Mkoa wa Mjini Magharibi, alikojumuika pamoja na waumini wa dini ya Kiislamu kwenye ibada ya sala ya Ijumaa.

Mheshimiwa Rais aliieleza imani na amani ni vitu viwili vinavyokwenda sambamba na kutegemeana wakati wote, hivyo aliisihi jamii kadri wanapokusanyika pamoja kwenye maisha yao ya kila siku, wasichoke kuamini na kuendelea kuhimiza amani ya nchi na kuidumisha muda wote katika kuyaendea mazuri yote kwa ustawi wa jamii njema na taifa kwa ujumla.

“Imani na amani vinakwenda sambamba, amani ndio dini yetu, Uislamu unatutaka tueneze amani wakati wote, amani ikikosekana mambo mengine yote hayawezekani na hili tunalijua kutokana na wenzetu wanayoyapitia huko kwenye mataifa ya wenzetu.

"Tunaona sehemu zenye vita hata ibada hazifanyiki, ili ipatikane amani lazima tuwe na imani ndani ya nyoyo zetu,”alisisitiza Alhaj Dkt.Mwinyi.

Alhaj Dkt.Mwinyi alieleza, kila mmoja anawajibu wa kuitunza na kueneza amani kwa mustakbali wa taifa na ustawi wa jamii iliyo bora.

Pia, aliwahimiza waumini hao kuendelea kuliombea taifa na viongozi kwa ujumla ili kuendelea kuwaongoza vyema na kuyatekeleza yote waliyowaahidi wananchi.

Rais Alhaj Mwinyi alieleza, viongozi wana majukumu makubwa na kubeba dhima kubwa hivyo, aliwasihi wanaumini hao na jamii kwa ujumla wasichoke kuwaombea mazuri na kuzidi kuwaombea kheir kwa Mwenyezi Mungu (S. W).

Akitoa nasaha za Ijumaa, Katibu Mtendaji kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume, alisifu juhudi za Rais Alhaj Dkt. Mwinyi kwa imani aliyoijenga kwa waumini wa dini ya kiislamu na taifa kwa ujumla ikiwemo kujumuika nao pamoja kwenye ibada katika misikiti mbalimbali nchini sambamba na kuwaboresha ustawi wa maendeleo na uchumi wananchi wote.

Alisema juhudi zote hizo ni imani yake kwa Wazanzibari na taifa lote, hasa jitihada za kuendelea kuimarisha huduma za jamii, uchumi na maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu imara na kuboresha mawasiliano.

Naye, Katibu wa sala ya Ijumaa msikitini hapo, Sheikh Abdul Karim Said Abdulla aliihusia jamii kuendelea kupendana na kutendeana mema kwa kujizuia kuudhiana na kutendea mabaya. Aliwashajihisha waumini hao kuendeleza mshikamo kwa kudumisha amani, umoja na upendo baina yao kwa ustawi wa jamii iliyo njema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news