Kasulu yafanya vema miradi ya maendeleo

NA RESPICE SWTU

MBIO za Mwenge wa Uhuru zimeipitisha pasipo mashaka yoyote miradi minane iliyotembelewa,kuzinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu (mwenye scurf) akiwa katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mvugwe Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, kushoto kwake ni mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kasulu, Abdallah Mbelwa na mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Eliah Kagoma.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mwenge huo kati ya Halmashaurti ya Wilaya ya Kasulu na mji wa Kasulu kwenye eneo la Nyumbigwa mjini Kasulu, kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2023, Abdallah Kaim ameonesha kuridhishwa na ufanisi.

Kaim ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kwa kazi nzuri ya kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali na ile iliyopitiwa na mwenge na kuifanya halmashauri hiyo kukamilisha mbio za mwenge ikiwa na hati safi.

“Nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isack Mwakisu,mkurugenzi, madiwani, Chama Cha Mapinduzi, wakuu wa idara,

"Vitengo pamoja na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kwa kazi iliyotukuka, tumeoina miradi katika maeneo mbalimbali tuliyopita na kuridhika nayo, nami kwa dhati kabisa niseme kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mmeupiga mwingi,”alisema.

Aliongeza pia kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi shupavu wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imekuwa ikitoa pesa nyingi kwa ajili ya kupeleka huduma mbalimbali kwa wananchi hivyo ni jambo la faraja kuona kuwa pesa hizo mmezisimamia na kuzitendea haki.

Awali baada ya mapokezi yaliyofanyika katika Kijiji cha Mvugwe, mwenge wa uhuru ulianza mbio zake kwa kuzindua majengo ya vyumba viwili vya madarasa na ofisi ya walimu katika Shule ya Msingi ya Kumganza mradi uliotekelezwa kwa thamani ya shilingi 80,750,000 kwa ufadhili wa World Vision.

Miradi mingine iliyotembelewa na mbio za mwenge wa uhuru na thamani ya miradi hiyo ikiwa kwenye mabano ni pamoja na kikundi cha waendesha bodaboda wa Kijiji cha Makere (40,000,000/=), mradi wa bustani ya kuzalisha miche ya miti kijiji cha Kalimangoma (250,000,000/=) na mradi wa maji safi na salama kwenye kijiji cha Mkesha (253,400,272/=).

Aidha, katika eneo la hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru aliweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa nyumba nne za watumishi wa hospitali hiyo (460,000,000/=) na kuzindua barabara ya lami yenye urefu wa nusu kilometa inayoelekea kwenye hospitali hiyo (500,000,000/=).

Kabla ya mkesha, msafara wa mbio za mwenge ulizindua klabu ya wapinga rushwa katika shule ya sekondari ya Rungwampya ambapo pia ulipofanyika mkesha wa mwenge huo.

Sanjari na kuzindua, kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, mwenge wa uhuru umetoa ujumbe wenye kauli mbiu ya kupiga vita uharibifu wa mazingira, rushwa,matumizi ya dawa za kulevya na kujikinga na maambukizi mapya ya VVU na Ukimwi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news