DODOMA-Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo chini ya Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mussa Sima amepongeza mkakati uliopo wa kutangaza na kubidhaisha lugha ya Kiswahili Kimataifa.
Akiwasilisha mkakati huo wa kutangaza Kiswahili Kimataifa kwenye kamati hiyo Agosti 23, 2023 kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi, Dkt. Pindi Chana, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania, Consolatha Mushi amesema mkakati huo tayari umesaidia kuanzishwa kwa vituo vya kufundisha Kiswahili katika Balozi za Tanzania nje ya nchi pia kuwa na vituo katika Mikoa ya Dodoma, Arusha na SAUT Mwanza.
“Mafanikio ya mkakati huu ni pamoja na upatikanaji wa Siku ya Kiswahili Duniani, kuongezeka kwa Idadi ya wazungumzaji wa Kiswahili hadi kufikia Milioni 500 Duniani, kuridhiwa kwa kiswahili kitumike kama lugha ya Mawasiliano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC na Umoja wa Afrika,”amesema Consolatha Mushi.
Kwa upande wake Waziri Dkt. Pindi Chana amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kukikuza Kiswahili ikiwemo kukizungumza katika mikutano ya Kimataifa pamoja wadau wa Utamaduni na Sanaa kukitumia katika kazi zao.
Naye Mwenyekiti wa kikao Mussa Sima ameelekeza wizara kupitia BAKITA kukitumia kiswahili katika kutangaza Utamaduni, mila na desturi za Tanzania ambazo ili kuvutia watalii wengi zaidi kufanya utalii wa kitamaduni nchini.