Mabadiliko ya mitaala ni chachu ya maendeleo-Prof.Bisanda

PWANI-Mabadiliko katika jamii ni kitu ambacho kinatokea kila siku na hivyo mabadiliko ya mitaala ya elimu nchini ni muhimu ili kuendana na mabadiliko yanayotokea ulimwenguni kote na kwenye jamii yetu.
Hayo yamesemwa na Prof. Elifas Tozo Bisanda Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) wakati wa mafunzo ya uandaaji na ukuzaji wa mitaala kwa wakuu wa vitivo, wakurugenzi; udhibiti ubora na Taasisi ya Elimu Endelezi.

Sambamba na wakuu wa Idara zote za kitaaluma kutoka vitivo vyote vya OUT yaliyofanyika Agosti 24-26, 2023 katika Shule Kuu ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo kwa Mfipa Kibaha mkoani Pwani.

"Nchi yetu ipo katika kufanya mabadiliko ya mitaala katika katika ngazi za elimu ya msingi na sekondari ambayo kwa sasa imefika mahali pazuri. 

"Na sisi watu wa vyuo vikuu OUT ikiwemo tupo katika kuimarisha mitaala yetu ili iendane na mabadiliko hayo pamoja na hali ya soko na mahitaji ya ajira katika jamii. 

"Ndiyo maana leo tupo hapa Kibaha kwa ajili ya kuwanoa wakuu wote wa Idara ili nao wakawanowe wahadhiri katika idara zao. 
"Ni lazima tuhakikishe tunakuja na mitaala ambayo itazalisha wataalamu wenye uwezo wa kujiajiri na kubuni miradi ambayo itaajiri wenzao,"amesema Prof.Bisanda.

Akimshukuru Makamu Mkuu wa Chuo kwa hotuba nzuri ya ufunguzi wa mafunzo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof.Deus Ngaruko amesema kwamba, katika kipindi tulichopo tunahitajika kuwa ni mitaala yenye kulenga kutoa ujuzi yaani Competence Based Curriculum.

Ni ili wahitimu waweze kutoka na maarifa, nyenzo na kubadili mtazamo wa kusubiri kuajiriwa bali kujiajiri. 

"Ujuzi ndiyo jambo la msingi kwa sasa, tunatakiwa tuhakikishe wahitimu wetu wanaweza kufanya nini kipya na siyo kujua nini peke yake. 

"Kujua tu halafu kushindwa kufanya kitu kipya haikubaliki katika ulimwengu huu ambapo sasa elimu na maarifa imekuwa ni jambo mtambuka. 
"Tunakushukuru sana Makamu Mkuu wa Chuo kwa kuwezesha mafunzo haya muhimu katika kipindi hiki tupo kwenye mapitio ya mitaala,"aliongeza Prof.Ngaruko.

Naye mbobezi mahiri wa masuala ya mitaala, Prof. Paul Mushi alishiriki katika kutoa mafunzo kwa wakuu hao wa Idara katika eneo la usanifu wa mitaala ama Curriculum Design. 

Miongoni mwa mambo mengi mazuri aliyofundisha ni pamoja na kuwataka waandaji hao wa mitaala kuhakikisha kwamba wanafanya utafiti wa kutosha ili kuja na mitaala ambayo inakidhi mahitaji ya jamii yetu ya sasa na baadae. 

Alisisitiza kufahamu malengo na mipango ya serikali, sera za serikali, misingi ya taifa, utamaduni wa jamii ya Kitanzania, miiko na maadili katika nchi ya Tanzania na ulimwengu kwa jumla. 

Mitaala ambayo itazingatia mambo haya kwa hakika itasaidia katika kuzalisha wahitimu mahiri na wabobezi katika nchi yetu.

Mafunzo hayo yaliratibiwa na Kigoda cha UNESCO cha Elimu kwa Walimu na Ukuzaji wa Mitaala cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania chini ya Mwenyekiti wa Kigoda hicho Prof. Elifas Bisanda na Dkt. Edefonce Nfuka pamoja na Dkt. Janeth Kigobe ambao ni waratibu wa kidoga hicho. 

Kwa hakika, wamesimamia vema mafunzo hayo na kuwashukuru washiriki na watoa mada wote kwa kazi nzuri ambayo itasaidia katika kuimarisha mitaala ya elimu ya juu, ya kati, msingi na sekondari nchini Tanzania kupitia Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. 

"Tumetaja maeneo haya kwa sababu OUT inafundisha walimu katika ngazi mbalimbali na walimu hao watakuwa ni zao la mitaala iliyoimarishwa na wao watakuwa walimu wazuri katika ngazi hizo za elimu,"alihitimisha Dkt.Nfuka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news