Madaktari wazawa MNH Mlongazila wafanya kweli tena

DAR ES SALAAM-Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila jijini Dar es Salaam imefanya upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye sakafu ya ubongo kupitia pua (Endoscopic transphenoidal pituitary) bila kupasua fuvu la kichwa ambapo tangu kuanza kwa huduma hii takribani watu watano wamenufaika na matibabu hayo.
Upusuaji huo umefanywa na madaktari wazawa ikiwa ni mwendelezo wa utoaji wa huduma za kibingwa na kibobezi zinazotolewa katika hospitali hii ikiwa ni juhudi za kuunga mkono Serikali za kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Kaimu Mkurugenzi msaidizi wa huduma za upasuaji Muhimbili Mloganzila, Dkt. Godlove Mfuko, amesema upusuaji huo umefanywa kwa ushirikiano wa Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu pamoja na Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Pua, Koo na Masikio.

“Upasuaji huu umefanywa na madaktari wetu kwa mafanikio makubwa, leo tumemfanyia mgonjwa mmoja, mgonjwa huyu endapo angepelekwa nje ya nchi kutibiwa ingegharimu takribani shilingi milioni 40 kwa mgonjwa mmoja, lakini kwa hapa inagharimu taktibani shilingi milioni sita mpaka nane,”amesema Dkt. Mfuko.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu Muhimbili-Mloganzila Dkt. Raymond Makundi ameeleza kuwa wagonjwa wengi wanaofanyiwa upasuaji huo wanakuja wakiwa na dalili za uoni hafifu na wakifanyiwa uchunguzi wanagundulika kuwa na uvimbe ambao unasababisha athari kwenye mishipa ya uoni.

“Sababu zinazosababisha kupata uvimbe kwenye ubongo zipo nyingi ikiwemo suala la vinasaba ambavyo huchangia kwa kiasi fulani ila asilimia kubwa ya watu wanaokutwa na magonjwa haya huwa yanatokea bila sababu yoyote,” amesema Dkt. Makundi

Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Pua, Koo na Masikio kutoka MNH, Dkt. Edwin Liyombo amesema awali upasuaji huo ulikua ukifanyika kwa kufungua fuvu la kichwa lakini kutokana na mabadiliko ya teknolojia sasa unafanyika kwa kupitia pua ambapo mgonjwa anachukua muda mfupi kupona na upasuaji huo ni salama.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news