Maziwa ya mama yalivyobeba hatima bora ya mtoto wake

NA GODFREY NNKO

SERIKALI imeendelea kusisitiza kuwa, maziwa ya mama ni chakula bora kwa mtoto, kwani humpatia virutubishi vyote na maji anayoyahitaji kwa ukuaji bora.

Hayo yamebainishwa Agosti 3, 2023 na Mkurungezi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Dkt. Germana Leyna wakati wa semina elekezi kwa waandishi wa habari Mkoa wa Dar es Salaama kuhusu umuhimu wa kuandika, kuhabarisha na kuelimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na lishe na afya.

Semina hiyo ni mwendelezo wa shughuli mbalimbali zinazofanyika katika kuadhimisha Wiki ya Unyonyeshaji wa Maziwa ya Mama Duniani.

Kwa hapa nchini,maadhimisho ya wiki hiyo kuanzia Agosti Mosi hadi 8,2023 huambatana na shughuli mbalimbali zinazolenga kufikisha taarifa, jumbe na hamasa kwa wananchi kuanzia ngazi za chini hadi juu.

Dkt.Leyna amesema, kwa kutambua hilo ndiyo maana Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kulinda, kuimarisha na kuendeleza unyonyeshaji nchini bila vikwazo.

"Kwa kutambua umuhimu wa unyonyeshaji wa mama katika kuimarisha afya ya mtoto, Serikali ya Tanzania imechukua hatua mbalimbali katika kulinda na kuimarisha na kuendeleza unyonyeshaji.

"Hatua ya kwanza ni kutunga Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 ambayo inatambua kuwa unyonyeshaji ni haki ya mtoto na hivyo hutoa mafao mbalimbali ya uzazi ili kumuwezesha mwanamke kumlea mtoto hususani kumyonyesha ipasavyo.

"Mama mwajiriwa anayejifungua mtoto, ana haki ya kupata likizo ya siku 84 iwapo amejifungua mtoto mmoja au siku 100 endapo amejifungua mtoto zaidi ya mmoja bila kuathiri malipo yake.

"Aidha, baba pia hupata likizo ya ubaba ya siku tatu, katika wiki moja ya kwanza, lengo lote ni kwa ajili ya kuhakikisha mama anaweza kutekeleza jukumu lake la kunyonyesha na baba anamsaidia mama ili aweze kutekeleza azma yake na jukumu lake hilo.

"Pia, kwa mujibu wa sheria hii, mwajiri haruhusiwi kumpangia mama mjamzito au mama anayenyonyesha kazi ngumu, au za hatari ambazo zinaweza kuathiri afya yake mwenyewe au ya mtoto.

"Vile vile kumpangia kazi za usiku au kumyanyapaa au kumyany'asa kwa aina yoyote ile kutokana na hali yake hiyo aliyona nayo, changamoto tunayoiona za kutekeleza sasa sheria hii ni wanawake wengi wanafanya kazi katika sekta isiyo rasmi kama kilimo ambayo haina huu mfumo.

"Kwa hiyo,mfumo huu mara nyingi hawafaidiki nao kwa asilimia 100 kama ambavyo wenzao waliopo katika ajira rasmi, hivyo ni jukumu letu sisi wanajamii kuliangalia suala hili kwa umakini,

"Ili wanawake wenye watoto wachanga wapewe fursa ya kuweza kupumzika na kuwanyonyesha watoto wao kikamilifu hususani katika miezi sita ya kwanza, ambayo tunasema maziwa ya mama yanampa huyu mtoto nishati na virutubishi kwa asilimia 100.

"Kwa hiyo kipindi hiki kwa wale ambao hawako katika mfumo rasmi, naomba tukumbushane na kuhamasishana ili tuweze kumuwezesha huyu mama aweze kunyonyesha."

Pia, Dkt.Leyna amebainisha kuwa, vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kutoa taarifa sahihi kuhusu unyonyeshaji na ulishaji wa watoto kwa ujumla.

Sambamba na kusaidia kupambana na imani potofu kuhusu unyonyeshaji na taarifa zisizo sahihi zinazolenga maslahi ya kibiashara ya maziwa mbadala na vyakula vya watoto wachanga na hivyo kuchangia uboreshaji wa lisha na afya ya mama na mtoto ili kujenga taifa lenye nguvu imara na yenye tija.

Mkurugenzi Mtendaji huyo amesisitiza kuwa, vyombo vya habari vina wajibu wa kuendelea kutoa taarifa na kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kufuata taratibu sahihi za unyonyeshaji wa maziwa ya mama.

Amesema,vyombo hivyo ni miongoni wadau wakuu wa mawasiliano yanayolenga kubadili mitazamo na tabia za jamii kuhusu masuala ya lishe na afya nchini.

“Vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kutoa taarifa, kuelimisha na pia kuburudisha na miaka ya hivi karibuni dhima hiyo imepanuka na kujumuisha masuala ya ufuatiliaji.

"Kupaza sauti za watu wasio na sauti katika jamii, kusaidia kulinda maslahi katika jamii na mambo mengine,"amesisitiza Mkurugenzi Mtendaji huyo.

Mdau mwingine

Naye Afisa Lishe  Mtafiti TFNC,Fatma  Mwasora amefafanua kuwa, "Waajiri wakubali kuwaruhusu wale akina mama ule muda wa saa mbili ambao wamepewa kwenda kunyonyesha watoto.

"Lakini pia kwa wale kina mama wanaonyonyesha watoto wale vizuri kwa kuhakikisha wanapata vyakula mchanganyiko kutoka katika makundi yote ili iwawezeshe kupata maziwa ya kutosha na kuweza kuwaachia yale maziwa nyumbani na kuendelea kuwanyonyesha.

"Lakini pia, tunawaomba waajiri wote waweze kutenga vyumba maalumu ambavyo vitawawezesha hawa kinamama ambao wananyonyesha waweze kuja na watoto wao na watoto wao wanyonyeshwe katika sehemu za kazi.

"Huwa tunayaita maeneo maalum kwa ajili ya kunyonyeshea watoto, kuna baadhi ya taasisi ambazo tayari wameshaanzisha ambapo wao ninawapongeza, kwa zile ambazo bado hazijatayarisha maeneo hayo, tunawaomba sana wafanye hivyo, kwa ajili ya kina mama kunyonyeshea.

"Kwa nini maeneo hayo, faida yake ya kwanza inampunguzia mama ule msongo wa mawazo, wa kukaa na kufikiria mtoto wangu yupo mbali anataka kunyonya,lakini pia itaongeza tija kwa ile taasisi ambayo anafanyia kazi pale.

"Kwa sababu atakuwa muda mwingi yupo na mtoto wake, kwa hiyo hatakaa na mawazo ya kufikiria mtoto wangu, labda analia, labda anatamani kunyonya, kwa hiyo tunahamasisha kuanzishwa kwa vyumba maalumu kwa ajili ya kunyonyeshea watoto.

CMA

Naye Mwamuzi kutoka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Yohana Massawe amefafanua kuwa, mwajiri haruhusiwi kumuachisha kazi mwanamke kutokana na sababu zinazohusiana na ujauzito au kujiufungua.

"Pia inapobidi mwanamke kubadilishwa kazi kutokana na hali ya uzazi, hairuhusiwi kupewa kazi inayompunguzia kipato au marupurupu aliyokuwanayo awali."

Massawe akizungumzia kuhusiana na utatuzi wa migogoro ndani ya taasisi au sehemu ya kazi amefafanua kuwa, sheria inamtaka mwajiri kuweka utaratibu wa utatuzi wa migogoro mahala pa kazi ili kuzuia kukuza kutokuelewana katika eneo la kazi.

"Uwepo wa taratibu hizo husaidia kuondoa au kupunguza migogoro ya aina yoyote katika sehemu ya kazi na hivyo kujikita zaidi katika uzalishaji na utoaji huduma."

Akizungumzia utatuzi wa migogoro nje ya taasisi au sehemu ya kazi, Massawe amefafanua kuwa, iwapo mfanyakazi mwanamke mjamzito au anayenyonyesha atapata changamoto katika kupata haki zake za msingi anayo haki ya kufungua mgogoro wake katika Tume ya Usuluhisi na Uamuzi kwa ajili ya utatuzi kwa mujibu wa sheria za kazi za nchi.

"Vile vile Idara ya Kazi huweza kutatua changamoto mbalimbali kupitia ukaguzi unaofanyika katika sehemu za kazi kuhakikisha kuwa matakwa ya kisheria yanazingatiwa."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news