Miradi yote itakamilika-Biteko

NA MATHIAS CANAL

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe ambaye pia ni Waziri wa Madini, Dkt.Doto Mashaka Biteko amewahakikishia wananchi wa Mkoa Geita kuwa, miradi yote mikubwa ya kimkakati iliyoanzishwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kutekelezwa na hakuna mradi utakaosimama ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Biteko ameyasema hayo katika wakati wa mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Geita na kufanyika katika Mtaa wa Kalangalala Jimbo la Geita Mjini uliowakutanisha wabunge wote wa mkoa huo kuelezea utekelezaji wa ilani ya CCM.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia kauli mbiu ya Kazi Iendelee amehakikisha miradi yote mikubwa ya kimkakati iliyoanzishwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kutekelezwa na hakuna mradi uliosimama wala mradi utakaosimama,”amesema Biteko.

MNEC Biteko amesema kuwa, Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa ya kupeleka fedha nyingi za maendeleo kote nchini kuanzia ngazi ya kijiji mpaka miradi ya kitaifa kama Ujenzi wa reli ya SGR na bwawa la kuzalisha umeme la Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambayo yote inaendelea kutekelezwa.
“Nawaomba wananchi wote na Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi tuendelee kumuunga mkono Rais na Mwenyekiti wa CCM, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kumwaga fedha za maendeleo kote nchini na ana maono makubwa ya kufikisha nchi yetu mahala pazuri,”amesisitiza.
Aidha, Biteko amewakumbusha Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kuendelea kuisimamia Serikali katika ngazi zote na kupaza sauti pale wanapoona watu wachache wanakwamisha utekelezaji wa Ilani ya CCM kupita miradi inayotekelezwa katika maeneo yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news