Mizaa ya wana Simba yaiponza klabu

DAR ES SALAAM-Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS) kwa pamoia na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wamelaani vikali kitendo kilichofanywa Agosti 6,2023 kwenye Simba Day.

Ni kwa kumtumia mtu mwenye ualbino mithili ya mtu aliyekuwa katika hali ya nusu utupu na aliyevaa nepi ya mkojo jukwaani, mbele ya kadamnasi ya maelfu katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo wameutaka uongozi wa Simba SC uombe radhi.

Kupitia taarifa yao ya pamoja Mwenyekiti Taifa wa TAS, Godson Mollel na Mkurugenzi wa LHRC, wakili Anna Henga wamesema,tukio hilo linafuatia tukio jingine lililofanywa na klabu hiyo Agosti 8,2022 kwenye Simba Day.

Wamesema, katika tukio hilo kulitokea kitendo cha kutumia jeneza, msalaba na kumnasibu mtu mwenye ualbino kama msukule.

“Vitendo hivi vinatweza utu wa watu wenye Ualbino nchini na vinapelekea kuwepo kwa mijadala mingi katika jamii ikiwemo mitandaoni inayoonesha dhihaka kwa watu wenye ualbino kinyume na haki za binadamu.

“Tunautaka Uongozi wa Simba uombe radhi kwa watu wenye Ualbino na umma wa Watanzania kwa vitendo hivi vya kutweza utu wa uatu wenye ualbino na tunaiomba Serikali na TFF wasimamie jambo hili.”

Henga alisema kuwa, kwa miaka mingi jitihada kubwa zimekuwa zikifanyika katika utetezi kwa watu wenye ualbino kutokana na historia ya watu hao kupoteza maisha na idadi kubwa ya wahanga wa vitendo vya ukatili na unyanyapaa.

Alisema kuwa, kwa Mujibu wa lbara ya 12(2) ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kila mtu anastahili heshima, kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake."Ibara hii inaakisi Ibara ya 8 ya Mkataba wa watu wenye ulemavu inayokomesha vitendo vya ukatili."

Naye Godson amesema kuwa, ni vyema taasisi zenye ushawishi kwenye jamii kuepuka vitendo vya udhalilishaji dhidi ya watu wenye ualbino nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news