NA GODFREY NNKO
"Ni matarajio yetu Ofisi ya Msajili wa Hazina mtatekeleza majukumu yenu kwa kuzingatia weledi, uadilifu na kufuata sheria na kanuni katika kuleta tija na ufanisi katika maendeleo ya makampuni hayo na shirika letu la TPDC;
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Huduma za Kimenejimenti wa Ofisi ya Msajili wa Hazina,Neema Musomba kwa niaba ya Msajili wa Hazina, Nehemiah Kyando Mchechu leo Agosti 31, 2023 jijini Dar es Salaam.
Ni katika hafla ya uzinduzi wa bodi za kampuni tanzu mbili za Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) ikiwemo Kampuni ya Gesi Tanzania (GASCO) na Kampuni ya Mafuta (TANOIL).
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Balozi Ombeni Sefue.
Ofisi hiyo imeagiza bodi hizo kufanya kazi kwa ufanisi ili kuhakikisha kampuni hizo zinaleta matokeo bora ndani ya kampuni, shirika na Taifa.
"Naomba kuwapongeza wajumbe wote na wenyeviti kwa kuteuliwa na kupewa dhamana hii ya kuongoza na kusimamia menejimenti hizi katika kuziwezesha kutekeleza majukumu yake ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na Serikali.
"Tunaamini mna uzoefu mkubwa na hivyo, malengo yatafikiwa vyema kabisa. Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia taasisi 248.Hizo taasisi zimo zile ambazo Serikali ina umiliki wa zaidi ya asilimia 51.
"Pia kampuni 56, Serikali ina umiliki wa hisa ambazo ni chini ya asilimia 51 huo ni uwekezaji wa serikali kwenye makampuni, lakini taasisi hizi zimekuwa na mchango mkubwa katika kuchochea ukuaji wa sekta mbalimbali.
"Kama sekta za mafuta, gesi, elimu masuala ya afya, biashara na kilimo na pia kukuza pato la Taifa na Mfuko Mkuu wa Serikali.
"Taasisi hizo zimekuwa chachu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kukuza ajira, huduma na bidhaa na ubora wake na bei stahiki,"amefafanua Neema kwa niaba ya Msajili wa Hazina.
Ameendelea kufafanua kuwa, "Kwa mujibu wa sheria zilizoanzisha taasisi hizo, taasisi hizo ziko pia chini ya Wizara za Kisekta na hivyo zinapaswa kuwajibika kwa Wizara za Kisekta katika majukumu ya kisera.
"Ofisi yenu itakuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kuna hayo mabadiliko ya reporting structure, kwa hiyo tutaendelea kutekeleza majukumu katika sekta za masuala ya nishati hatujatoka huko kwenye nishati na gesi asilia
"Hizi taasisi ambazo ziko chini ya Msajili wa Hazina kisheria, kiutendaji kwa mujibu wa sheria ya Mamlaka na Msajili wa Hazina sura ya 370 lakini na Sheria ya Mashirika ya Umma sura 257.
"Zinasimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina katika masuala ya kiutendaji kiujumla ambayo yanajumuisha utawala bora, udhibiti wa gharama za uendeshaji wa taasisi na kupima ufanisi wa taasisi kwa kuangalia malengo ya kuanzishwa kwake.
"Tumeyaona malengo ya kuanzishwa kwa TPDC na inavyo-oparate kwa muda ikaona malengo haya tukikaa tu kama TPDC hatuwezi kuyafikia, ikaanzisha kampuni tanzu mahususi kutekeleza majukumu yake.
"Kwa hiyo Ofisi ya Msajili wa Hazina inaingia hapa kupima haya malengo ya kiutendaji yaliyowekwa kwenye hizi sekta yanafikiwa.
"Tumesikia jukumu la miundombinu kwa GASCO na jukumu la kibiashara kwa TANOIL, lengo kuhakikisha kwamba huduma zinaboreshwa, biashara ya kampuni inafanyika na kuleta faida na kuhakikisha ufanisi unapatikana.
"Kwa hiyo, Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC kiutendaji itapaswa kuka-scade yale malengo yake mahususi kwenye bodi ya Wakurugenzi ya TANOIL, kwenye zile shughuli za TANOIL na kwa GASCO kwa zile za GASCO na pia itapima kuona hizi bodi za Wakurugenzi kuona kama zinafaa na kutelekeza malengo ambayo yamekasimiwa na kampuni mama ya TPDC ili kuhakikisha yanafikiwa.
"Vile vile bodi za Wakurugenzi za Kampuni tanzu mtawajibika kutoa taarifa za kiutendaji kwa kampuni mama ili waweze kupokea taarifa zenu za maendeleo, changamoto, na bodi ya kampuni mama ina mamlaka ya kusimamia utendaji kazi wenu.
"Pia bodi ya kampuni mama itatumia hizo taarifa katika kufanya maamuzi mbalimbali yanayohusiana na hizo kampuni tanzu.
"Pia, kampuni tanzu zitakuwa na menejimenti ambazo zitaundwa kwenye mfumo na zitakuwa na majukumu ya uendeshaji wa taasisi, kwa hiyo bodi za kampuni tanzu zitakuwa chombo cha usimamizi wa taasisi.
"Sisi Ofisi ya Msajili wa Hazina tutapata wapi taarifa ya kampuni tanzu? Sisi tutapata taarifa zenu za utendaji kazi kupitia zile taarifa ambazo zinawasilishwa kwa kila kipindi cha robo mwaka na kampuni mama ya TPDC.
"Kwa hiyo tutategemea pale watatuelezea wao kama kampuni wamefikia wapi na hizi kampuni tanzu utekelezaji wake ukoje kulingana na yale malengo ambayo yatakuwa yamewekwa kwenu,"imesisitiza Ofisi ya Msajili wa Hazina.