MOROGORO-Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Rufaa) Mhe. Jacobs Mwambegele amewataka wasimamizi wa uchaguzi nchini kufanya kazi kwa weledi ili chaguzi ziwe nzuri, zenye ufanisi na amani.
Jaji Mwambegele ameyasema hayo leo tarehe 08 Agosti, 2023 Mkoani Morogoro, wakati akifungua mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbarali lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya na kata sita za Tanzania Bara.
Uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kisheria ambazo hupaswa kufuatwa na kuzingatiwa, hatua na taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi kuwa mzuri, wenye ufanisi na hivyo kupunguza kama siyo kuondoa kabisa malalamiko au vurugu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi, amesema Jaji Mwambegele.
Amewaasa watendaji hao kuwa pamoja na uzoefu ambao baadhi yao wanao katika uendeshaji wa uchaguzi, wanatakiwa kuhakikisha kwamba wanazingatia maelekezo watakayopewa na Tume badala ya kufanya kazi kwa mazoea.
“Wakati wote wa mchakato wa uchaguzi huu, ni vema mkavishirikisha kwa karibu vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi katika maeneo yenu kuhusu masuala ya kiuchaguzi ambayo wanastahili kushirikishwa kwani jambo hilo litawarahisishia utekelezaji wa majukumu yenu," Jaji Mwambegele amewaeleza watendaji hao.
Amewasisitiza juu ya umuhimu wa kuhakikisha kuwa wanayatambua na kuyajua vyema maeneo ambayo uchaguzi utaendeshwa ikiwemo miundombinu ya kufika katika jimbo, kata na vituo vya kupigia kura.
Aidha, aliwataka watendaji hao kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalum ya vituo husika kwa lengo la kuhakikisha mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani.
Jaji Mwambegele pia amewakumbusha watendaji hao kuhakikisha siku ya uchaguzi wanaweka utaratibu utakaowezesha kila kituo cha kupigia kura kufunguliwa saa 1:00 asubuhi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Ramadhani Kailima aliwataka watendaji hao wa uchaguzi kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na kuwasiliana na Tume wakati wowote wanapopata changamoto ya kiutendaji.
Kailima amewaasa watendaji hao kuhakikisha kwamba wanazingatia viapo vyao ikiwa ni pamoja na kutopendelea upande wowote wakati wote wa uchaguzi.
Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbarali na kata sita za Tanzania Bara utafanyika tarehe 19 Septemba, 2023, wagombea watachukua fomu kuanzia tarehe 13 hadi 19 Agosti, 2023, siku ya uteuzi itakuwa tarehe 19 Agosti, 2023 na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 20 Agosti, 2023 hadi tarehe 18 Septemba, 2023.
Kata zitakazofanya uchaguzi mdogo ni; Nala iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma, mkoani Dodoma, Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza, Old Moshi Magharibi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi na Marangu Kitowo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, Mtyangimbole iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba na Mfaranyaki iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma.