NHC yaja na utaratibu mpya, wadaiwa sugu wa kodi mguu nje, mguu ndani

NA GODFREY NNKO

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limesema, kuanzia sasa mpangaji yeyote mpya hawezi kupangishwa nyumba zake bila kulipa amana ya pango (security deposit) ya miezi mitatu.
Hayo yamebainishwa leo Agosti 15,2023 na Meneja Habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa, Bw. Muungano K. Saguya wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya shirika hilo jijini Dar es Salaam.

Saguya alikuwa akielezea kuhusiana na jitihada za shirika hilo za kuendelea kukusanya madeni ya kodi kutoka kwa wapangaji wake nchini.

“Hii itasaidia shirika kuzitumia amana (deposits) hizo pale wanapoacha madeni na kuondoka kwenye nyumba.

“Kwa wapangaji waliopo kwenye nyumba na ambao hawajakamilisha kulipa amana ya pango inayotakiwa wameandikiwa barua na kupewa muda mpaka Desemba 31, 2023 ili wakamilishe kulipa amana za pango (security deposit) vinginevyo shirika litalazimika kusitisha mikataba yao ya upangaji,”amefafanua Saguya.

Pia amesema kuwa, shirika hilo limeanzisha makubaliano na CREDIT INFO BUREAU ili kupeleka majina ya wadaiwa sugu katika taasisi mbalimbali zikiwemo za fedha na ili wadaiwa hao wasiweze tena kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha.

Amesema,ili kuepusha madeni ya mara kwa mara, kuanzia sasa shirika hilo halitampa mkataba mpya mpangaji ambaye anakuwa na rekodi mbaya ya kulipa kodi kwa wakati.

“Watanzania wengi wamekuwa wakiomba upangaji katika nyumba kuwa wapangaji wa NHC.

“Wadaiwa sugu watakaokaidi maelekezo haya ya shirika, watakuwa wameruhusu shirika kuwatangaza katika vyombo vya habari.

“Ni ili mashirika na makampuni mengine yasiingie kwenye makubaliano ya kibiashara na mtu au kampuni inayodaiwa.”

Saguya amefafanua kuwa,ili kuhakikisha kodi na malimbikizo ya madeni yanalipwa, Mkurugenzi Mkuu wa NHC,Bw.Hamad Abdallah ameunda Kamati ya Menejimenti ambayo itaanza kazi rasmi wiki hii ya kufuatilia madeni yote yanayodaiwa na shirika.

Wakati huo huo, Saguya amesema kuwa,shirika limeingia mikataba na wapangaji ya kuwaruhusu kulipa madeni yao kwa awamu kila mpangaji anayodaiwa.

Kwa mujibu wa mkataba huo kutoka shirika unaelekeza kuwa,kama mpangaji ana sababu maalum ahakikishe anaweka utaratibu madhubuti wa kulipa madeni yake anayodaiwa.

“Kwa wapangaji waliopo kwenye nyumba (active tenants) ambao watashindwa kulipa kodi na malimbikizo yao ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kuanzia sasa, atakuwa ameonesha kuwa haihitaji nyumba anayopanga.

“Na shirika litavunja mikataba yao ya upangaji na kuwaondoa kwenye nyumba kwa mujibu wa sheria.

“Aidha, kwa wapangaji ambao walishapewa notisi mbalimbali za kulipa kodi wanayodaiwa, utekelezaji wa notisi hizo unaendelea kama notisi hizo zinavyoelekeza.

“Hivyo, shirika linawasihi watekeleze wajibu wao ili kuepuka usumbufu utakaoweza kujitokeza kwa kushindwa kutimiza wajibu huo,”amefafanua Saguya.

Mbali na hayo, NHC limewashukuru wapangaji wote wanaotimiza wajibu wao wa kulipa kodi ya nyumba kwa wakati kama mikataba ya upangaji inavyoelekeza.

“Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), tunawashukuru wapangaji walioitikia wito wetu kwa kulipa madeni yao.”

Aidha, Saguya amebainisha kuwa, kampeni hii ya mwezi mmoja itaongozwa na kauli mbiu ya Lipa Madeni yako kwa Maendeleo ya Shirika na Taifa Letu.

Shirika la Nyumba la Taifa limekuwa katika jitihada za kukusanya madeni kwa wapangaji wa nyumba zake waliopo na waliohama katika nyumba zake.

“Hapo awali, tuliwafahamisha kuwa shirika limekuwa likidai madeni ya kodi ambayo awali yalikuwa shilingi bilioni 28 na tuliwaeleza mbinu mbalimbali zinazotumika kukusanya madeni hayo ambazo zimelisaidia kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 5.

“Kutokana umuhimu wa shirika kuwa na fedha za kutekeleza miradi yake, pamoja na maelekezo aliyoyatoa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) wakati akiahirisha Kikao cha Bunge Julai 2023 na kuagiza wadaiwa wote wawe wamelipa madeni yao ndani ya miezi mitatu.

“Shirika limeamua sasa kuanza Kampeni ya Lipa Madeni yako kwa Maendeleo ya Shirika na Taifa Letu ili kukusanya madeni hayo,”amefafanua.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news