MWANZA-Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimekuwa ni chuo kikuu pekee ambacho kinatoa elimu kwa wafungwa waliopo katika Magereza mbalimbali hapa nchini kwa miaka kadhaa sasa na wapo ambao wamefanikiwa kuhitimu masomo yao wakiwa gerezani.
Hayo yamesemwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Tozo Bisanda alipokutana na kufanya mazungumzo na ndugu Machera Sijaona Chacha aliyehitumu Diploma ya Ualimu wa Shule ya Msingi (DPTE) ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania mwaka 2015.
"Leo nimepata furaha sana kukutana na ndugu Machera ambaye alisoma OUT kuanzia mwaka 2010 na kuhitimu masomo yake mwaka 2015 akiwa ni mfungwa katika Gereza la Butimba jijini Mwanza.
"Mhitimu huyu alisoma na kufanya mitihani yake akiwa gerezani na akafanikiwa kuhitimu masomo yake kwa ufaulu mzuri sana.
"Hii ndiyo azma ya OUT kuwafikia na kutoa fursa kwa kila mtu kupata elimu ya juu popote pale alipo,"amesema Prof.Bisanda.
Prof. Bisanda aliendelea kueleza kwamba OUT imeendelea kutekeleza dira na azma yake ya kuwafuata wanafunzi kule walipo na siyo wanafunzi kukifuata chuo.
Huu ni msingi na mhimili mkubwa wa OUT, kwani kwa kufanya hivyo kinawawezesha wanafunzi kujiendeleza kielimu bila kuacha kazi zao na kwa wale wa magereza kuendelea kutumikia vifungo vyao na wakimaliza wanatoka na elimu pamoja na mafunzo ambayo wamepewa na magereza.Naye Alumni wa OUT, ndugu Machera Sijaona Chacha ameeleza kufurahishwa kwake kukutana na Prof. Bisanda katika viwanja vya OUT Mwanza tarehe 10 Agosti 2023 ikiwa ni katika shamrashamra za Wiki ya Utumishi wa Umma kwa OUT zilizofanyika nchi nzima kwa kushirikisha wafanyakazi wote wa OUT.
"Nimepata heshima kubwa kukutana na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Prof. Bisanda na amenipokea vizuri sana.
"Mimi nilijiunga kusoma Diploma ya Ualimu wa Shule ya Msingi mwaka 2010 nikiwa natumikia kifungo katika gereza la Butimba jijini Mwanza.
"Nilisoma nikiwa gerezani ambapo nililetewa vitabu vya kozi yangu na wahadhiri wa OUT akiwemo Dkt. Ancfrida Prosper na Mr. Bernard Kapaya miongoni mwa wahadhiri wengine wa OUT Mwanza na Makao Makuu.
"Nilikuwa najisomea na wakati wa mitihani ukifika napelekwa na maafisa askari magereza kufanya mitihani OUT katika kila kipindi cha mitihani. Nilifanya mitihani yangu na kufanikiwa kuhitimu Diploma hiyo mwaka 2015 nikiwa bado natumikia kifungo."
Hakika, huu ni ushuhuda tosha wa kwamba OUT ni Chuo kinachowafuata wanafunzi kule kule walipo.
Anaendelea kueleza kwamba, "baada ya kupata vitabu na vitini vya kujisomea nilikuwa nasoma peke yangu na pale nilipopata ugumu wapo wafungwa wenzangu waliokuwa na elimu zaidi yangu niliwauliza na walinisaidia katika maeneo yaliyokuwa magumu kwangu.
"Walimu wa OUT walipokuja kuniona na kuniletea vitabu pia nilipata muda wa kuwauliza katika maeneo niliyopata ugumu katika masomo yangu na walinifafanulia na kunifundisha vizuri."
Wakati anaendelea na masomo yake hayo ya OUT alikuwa na darasa ambapo alikuwa akiwafundisha wanafunzi wengine wa OUT wa ngazi za chini gerezani hapo pamoja na wale ambao walikuwa hawajui kusoma na kuandika ndani ya gereza.
Baada ya kuhitimu Diploma alipata mbinu nyingi na bora zaidi za ufundishaji na ujifunzaji akaendelea kufundisha wafungwa wenzake mpaka alipoachiwa huru tarehe 10 Juni, 2023 yaani miezi mwili iliyopita.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa OUT Mwanza Dkt. Ancyfrida Prosper amemwelezea mhitimu huyo kuwa ni mfano wa kuigwa katika jamii mwenye jitihada na asiyekata tamaa. Dkt. Ancyfrida amesema:
"Machera ni mfano mzuri wa kuigwa na wanajamii wote wa rika zote kutokata tamaa katika maisha.
"Hapa tunapozungumza ndugu Machera amebakiza _Units_ chache tu kumaliza Shahada ya Elimu katika Elimu Maalumu ya OUT aliyojiunga mwaka 2016 mara tu alipohitimu Diploma akiwa bado ni mfungwa katika gereza la Butimba.
"Ni matumaini yetu kwamba siku chache zijazo atahitimu Shahada hiyo ya kwanza ya Elimu ya hapa hapa OUT na kutunukiwa,"amebainisha Dkt.Ancyfrida.
Haya ndiyo matunda ya OUT yakienda sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika kuanzia tarehe 07 Agosti na kukamilika 14 Agosti 2023.
Utumishi katika OUT ni kuwahudumia Watanzania wote na wanaulimwengu wote popote pale walipo wakiendelea na kazi zao, biashara zao, vifungo vyao na wakiwa katika shughuli zao na katika hali mbalimbali.