RC Chalamila afunguka mengi

DAR ES SALAAM-Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila ametoa ufafanuzi wa mambo 10 muhimu kwa mustakabali wa maendeleo na ustawi wa jamii katika mkoa huo na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Chalamila ameyabainisha ofisini kwake mkoani Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Akizungumzia uendelezaji wa masoko katika mkoa huo, RC Chalamila amesema, kumekuwa na changomoto kubwa katika masoko mengi ambapo yako makundi ya watu wachache wasiowaadilifu ambao wanaendesha masoko na Serikali haipati chochote.

RC Chalamila amesema, uamuzi wa Serikali ni kurudisha masoko hayo kusimamiwa na halmashauri ndio maana hivi karibuni amevunja uongozi wa Soko la Mabibo.

Hata hivyo, amesema tayari timu ya wataalam imeundwa kupita katika masoko yote ya mkoa na kuleta taarifa ya hali halisi ya masoko hayo.

Akizungumzia kuhusu migogoro ya ardhi Mkoa wa Dar es Salaam ambayo husababishwa na vikundi vya watu, makampuni ya uuzaji na kupima ardhi pia kufoji nyaraka mbalimbali tena wengine wanashirikiana na viongozi wa umma amesema, jambo hili halikubaliki Serikali iko timamu katika kuchukua hatua stahiki kwa wote wanaochangia migogoro hiyo.

Kuhusu usalama wa watu na mali zao, amesema hali ya usalama katika mkoa ipo shwari licha ya kuwa hivi karibuni kulitokea na vijana wachache Vingunguti ambao walidhibitiwa na vyombo vya ulinzi na usalama.

"Lazima tulinde amani ya mkoa kwa kuwa ndio kitovu cha biashara, diplomasia na ni mkoa wenye watu wengi, tusikubali amani itoweke,”amesema.

Pia, amesema huduma ya mabasi yaendayo kasi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ameendelea kuboresha miundombinu ya usafiri hususani mwendokasi.

Amesema, Rais Dkt.Samia ameshatoa fedha za kupanua barabara kutoka Ubungo kuungana na njia nane Kimara mwisho pia miundombinu imeendelea kuboresha katika maeneo mbalimbali ya mkoa na sasa utekelezaji wa awamu ya tatu unaendelea.

Wakati huo huo, akizungumzia usambazaji wa maji, amesema kumekuwa na mpango kabambe wa kuboresha miundombinu ya maji ili kuondoa changamoto ya maji mkoani humo.

Mheshimiwa Chalamila amesema,tayari Serikali inajenga bwawa kubwa la Kidunda na uchimbaji wa visima vya maji unaendelea Kigamboni na hivi karibuni ataanza ziara ya kukagua miradi ya maji katika mkoa huo.

Akizungumzia kuhusiana na wafanyabishara wadogo maarufu kama wamachinga kurudi katika maeneo yasiyo rasmi mfano eneo la Mbagala ameema, wamekuwa wakifanya biashara katika miundombinu ya mwendokasi hivyo amewataka viongozi wa machinga kuwahamasisha kufanya biashara kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na si vinginevyo.

Kuhusu wafanyabishara kulipa kodi za Serikali kila mfanyabiashara anayetakiwa kulipa kodi, amesema wanapaswa kulipa kodi.

Amesema, Serikali imekuwa ikitekeleza miradi mingi ya maendeleo hivyo namna pekee ya kukamilisha miradi hiyo ni kulipa kodi ili Serikali ipate mapato.

RC Chalamila amesema, migomo migomo sio njia sahihi ya kufikia suluhu za matatizo yetu, ”ebu jiulize endapo Daktari, Mwalimu au kundi lolote likigoma nini kitatokea? Nitoe rai njia ya mazungumzo ni njia sahihi kufikia suluhu ya matatizo yetu.”

Barabara eneo la Viwanda Kigamboni, amesema Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya barabara maeneo mbalimbali ya kimkakati ambapo barabara hiyo kuelekea Kisarawe II iko katika hatua ya tenda ili ijengwe kwa kiwango cha lami.

Kuhusu usafi, Mheshimiwa Chalamila amewataka wakazi wa mkoa huo na watu wengine wanaoingia na kutoka kila kukicha katika mkoa huo kuhakikisha mkoa unakua safi.

Pia, wafanyabishara,taasisi na watu wengine wanapaswa kuacha kutupa taka ovyo na amezitaka halmashauri kutenga bajeti za kuwa na dampo na kuwalipa wakandarasi wa taka kwa wakati.

Mheshimiwa Chalamila amesema, ataendelea kutoa taarifa kwa umma mara mara za utekelezaji wa miradi na mipango ya Serikali kwa masilahi mapana na ustawi wa jamii.

Aidha, kuanzia mwezi ujao, Mheshimiwa Chalamila amesema atafanya mikutano mikubwa katika kila wilaya kueleza dira na mwelekeo wa viongozi wa mkoa, kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news