NA FRESHA KINASA
MJUMBE wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) Mkoa wa Mara ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Uwezo wa Mshirika Tanzania, Rhobi Samwelly ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani humo (NGOs) kuzingatia utoaji wa taarifa juu ya utekelezaji wa kazi yanazofanya na taarifa za fedha zilizokaguliwa serikalini kwa wakati.
Rhobi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania ameyasema hayo Agosti 11, 2023 wakati akitoa maagizo ya NaCoNGO katika mkutano mkuu wa mwaka wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yaliyowakutanisha viongozi wa mashirika hayo Mkoa wa Mara.
Mkutano huo ulikuwa na lengo la kupata taarifa za mafanikio na changamoto kwa kuzijadili na kuweka mikakati ya utatuzi na mahusiano baina ya Serikali na NGOs mkoani humo chini ya Mwenyekiti wa kikao hicho, Mheshimiwa Said Mohamed Mtanda mkuu wa mkoa huo.
"Wadau wa NGOs zote mnawajibu wa kutoa taarifa za utekelezaji wa shughuli zenu za kazi na taarifa za fedha zilizokaguliwa, kwani tayari tunayo mashirika 96 hayajatoa taarifa na yako katika hatari ya kufutwa awamu ya pili na mashirika 60 tu ndio yako hai ambayo yanakidhi vigezo." amesema na kuongeza kuwa.
"Si vyema mashirika haya 96 yakafutwa ni vyema yakazingatia sheria, kanuni na matakwa ya Serikali kusudi yaendelee kutoa huduma kwa wananchi.
"Hata kama hauna fedha za kufanya shughuli zako, lakini unashirikiana na wadau au shirika jingine tolea taarifa kusudi zifahamike jambo hili ni muhimu sana likazingatiwa,"amesema Rhobi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Said Mohamed Mtanda akifungua mkutano huo amesema, mashirika mkoani humo yamekuwa yakifanya kazi kubwa ya kuisaidia Serikali kuleta maendeleo kwa wananchi. Hivyo atatoa ushirikiano kwa mashirika yote ili kufikia malengo.
Pia amesema, mashirika yanayokwenda kinyume cha sheria na taratibu ikiwemo kukiuka utu kwa kupokea fedha za nje ambazo hazizingatii mila, desturi na maadili ya kitanzania yaache na pia amesisitiza mashirika kufanya kazi bila Kona kona yazingatie weledi na uadilifu.
"Zipo pia NGOs ambazo zinajigeuza kufanya kazi za kisiasa ziache badala yake majukumu ya kisiasa waviachie vyama vya siasa na wao watekeleze majukumu kulingana na jinsi walivyosajiliwa kukidhi matakwa ya jamii. Tukigundua lazima sheria itachukua hatua ikiwemo kutafuta,"amesema RC Mtanda.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mara, Neema Ibamba ameyataka mashirika yote mkoani humo kuendelea kushiriki katika makongamano mbalimbali ikiwemo maadhimisho na kushirikiana na serikali.