Serikali ina mipango mema kwa vijana-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema, itaendelea kutenga bajeti ya mikopo kuwasaidia vijana wanaokosa fursa ya kujiunga na elimu ya juu ili wafanikishe ndoto zao kwa ustawi wa maendeleo yao.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo kwenye maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa, viwanja vya Maisara Suleiman Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema, Serikali imejipanga kufanikisha lengo lake hilo licha ya ongezeko la kila mwaka la vijana wanaopata sifa za kujiunga na elimu ya juu.

Pia, amesema, Serikali imechukua jitihada mbali mbali kuimarisha ustawi wa vijana kwa kuwashirikisha kwenye sekta zote za maendeleo ikiwemo Afya, Elimu, Kilimo, Uvuvi, TEHAMA, Ujasiriamali na michezo kwa kuwawesha kujiajiri na kuajiriwa.

Aidha, Dkt.Mwinyi alieleza Serikali za SMZ na SMT zimeweka utaratibu maalum wa ajira, chini ya Sheria ya Utumishi wa Umma namba 2/2008 ambayo imetoa asilimia 21% ya Ajira kwa Vijana wa Zanzibar kwenye Sekta za Muungano.

Alisema, kwa mujibu wa taarifa ya muelekeo wa kiuchumi ya mwaka 2022 kupitia miradi ya fedha za ahueni za UVIKO 19, jumla ya vijana 13,870 walifanikiwa kupata ajira za muda kupitia miradi iliyowekezwa na Serikali kupitia sekta mbalimbali za maendeleo.

Alieleza, mbali na jitihada za kuanzisha Wizara na Idara Maalum ya kushughulikia Maendeleo ya Vijana ili kuimarisha usimamizi na uratibu wa shughuli za maendeleo yao nchini pia Serikali imeanzisha Sera ya Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2005 iliyoweka miongozo ya shughuli zote za Maendeleo na Ustawi wao.

Akizungumzia maendeleo ya Sekta ya Afya kwa vijana, Rais Dkt.Mwinyi alisema, Serikali kupitia Wizara ya Afya imekua ikishirikiana na wadau wa maendeleo wakiwemo shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) kwa pamoja wameanzisha na kuviendeleza vituo 13 vya huduma rafiki za Afya kwa Vijana kwa wilaya zote za Unguja na Pemba.

Pia, alieleza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilivyoanza mradi wa ujenzi wa vituo vya mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa Vijana kwa Unguja na Pemba ambavyo vitachochea maendeleo yao kwa kuitumia taaluma watakayoipata, ikiwemo kwenda sambamba na Ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia.

Hata hivyo, Rais Dkt.Mwinyi aliahidi kuanzishwa Sera mpya ya Maendeleo ya Vijana itakayozingatia mahitaji ya wakati wa sasa na ujao, alitoa wito kwa taasisi zote za umma na binafsi,washirika wa maendeleo, Mabaraza ya Vijana, na Asasi za Maendeleo ya Vijana, kushiriki kikamilifu kwenye utekelezaji wa Sera hiyo kwa vitendo ili kufikia lengo lililokusudiwa na Serikali.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita aliahidi Serikali kuendeleza fursa kwa vijana, kuwasimamia, kuratibu na kupunguza changamoto zinazowakabili.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Muhamed Kawaida alipongeza juhudi za Serikali ya Dkt.Mwinyi kwa mara ya kwanza amefanikiwa kuwaweka pamoja vijana wa vyama vya mbalimbali bila kujali tofauti za itikadi zao na kueleza kuwa hatua hiyo imeendelea kuimarisha amani ya Zanzibar iliyopo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Vijana, Yunus Juma Ali aliwaasa vijana kuendeleza heshima kwenye jamii, kuvumiliana na kuyasema mambo yenye uhakika kwa kufanyia utafiti na kujiridhisha kabla ya kuzungumza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news